ASKOFU MKUU KANISA KATOLIKI JIMBO LA DAR ES SALAAM AENDELEZA MSIMAMO MKALI JUU YA KATIBA INAYOPENDEKEZWA.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema msimamo wake kuhusu Katiba Inayopendekezwa uko pale pale na ametaka wanaoamini alichosema, wasambaze ujumbe wake kwa wengine.
Akizungumza na Chama cha Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) hivi karibuni, Askofu Pengo alitoa wito kwa waumini kuachwa huru wafanye maamuzi yao wenyewe juu ya kuipigia kura ya ndiyo au hapana Katiba Inayopendekezwa badala la kushinikizwa na viongozi wa dini kuipigia kura ya ‘hapana’ katiba hiyo.
Aidha, amesema kamwe hawezi kubadili kile alichosema kwani ni ukweli anaouamini na alishaweka hilo wazi.
Askofu Pengo alisema hayo jana wakati wa ibada Maalumu ya Shirikisho la Kwaya Katoliki (Shikwaka ) iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Kipawa, jijini Dar es Salaam ambako kwaya zaidi ya 100 zilishiriki.
“Jana (juzi) baada ya ibada kule Kurasini walikuja waandishi wa habari na tukaanza kujadiliana na baadaye nilipomaliza wengine kisirisiri walijadili kwa nini sikusema chochote kuhusu Katiba Inayopendekezwa; Sasa ndugu zangu niseme mara ngapi,” alihoji.
“ Hivi ni nani anaweza kufikiria naweza kubadili maneno niliyosema, leo niseme kweli na kesho hapana. Nitakuwa mtu wa aina gani wa kubadili maneno na misimamo,”alisema.
Alifafanua kuwa alishasema ukweli anaoujua hivyo hana sababu ya kuurudia na kwamba kufanya hivyo ni kutafuta ugomvi. ‘’Yale niliyosema kuhusu suala hilo nimesema mara moja na ni mara moja tu basi,’’ alisisitiza.
Askofu Pengo aliwataka waamini na wasio waamini waliomsikia na kukubaliana na aliyosema, kuwa ni wakati wao kuendeleza taarifa hiyo kwa kusambaza katika sehemu mbalimbali.
Akirejea habari za kufufuka kwa Yesu, alisema kusambaza msimamo wake kutaenea kwa watu wengi zaidi kwani ndivyo injili ya ufufuko wa Bwana Yesu ilivyoenea kwa Petro ambaye awali wakati wa mateso ya Yesu, alimkana lakini mara baada ya kufufuka alisambaza taarifa hizo.
Askofu Pengo alisema mashemasi kama Filipo,Stephano na wengine hawakumwachia Petro kusambaza ufufuko wa Bwana Yesu ila kila walipokwenda walitamka kuhusu ufufuko na hakukuwa na haja ya kumuita Petro kuelezea ufufuko huo.
Alisema wasingefanya hivyo injili isingefika duniani kote .
“Hivyo hivyo wale walioamini niliyosema kuhusu msimamo wangu wa Katiba Inayopendekezwa, waendelee kusambaza kila wanapokwenda kwa manufaa ya nchi,” alisisitiza.
Alisema ndivyo inayofundishwa na fumbo la ufufuko wake Yesu kwa jambo jema halitegemei mtu mmoja kurudia rudia kwani atakera watu kutokana na kuwapo wanaosikia jambo moja mara kwa mara.
Askofu Pengo alisema anapoongelea tamko lake kuhusu Katiba si kwamba anataka kugeuza nafasi ya ibada kuwa mahali pa kutangaza siasa au shughuli za kijamii, bali neno lolote analofanya ni ukweli wake na hatobadili.
Alitaka waumini kusimama na kusema potelea mbali katika kusimamia ukweli wa kile wanachoamini kwa kuwa jasiri bila kuogopa chochote na kuwa sawa na mtu anayesema liwalo liwe.
Pengo alisema katika ulimwengu wa sasa, umuhimu wa kutamka ukweli na liwalo liwe, unazidi kudhihirika kutokana na madai ya nyakati kwani ni muhimu kwa maaskofu, mapadre na hata viongozi wa serikali kila mmoja ana nafasi ya kutamka ukweli.
Ugaidi
Aidha, Pengo alizungumzia tukio la ugaidi nchini Kenya lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 147 na kusema hakuna aliyefikiria kuwa Kenya inaweza siku moja kuzingirwa na watu na kufanyika mauaji yenye msimamo wa imani za dini.
Alisema ingawa nchi hiyo ilikuwa na malumbano kadhaa, lakini si dini. Alisema tukio hilo halipendezi si kwa Waislamu wala Wakristo.
“Tumuombe Kristo atuponye na kutuepusha na balaa hilo, na yasiendelee kutokea kwa jirani zetu huku kila mmoja akihakikisha kuwa na ujasiri wa kubaki na msimamo wetu,’’ alisema.
Waraka wa maaskofu Mwezi uliopita Askofu Pengo wakati akifungua Mafungo ya WAWATA, yaliyofanyika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam alikosoa waraka wa maaskofu kupitia Jukwaa la Kikristo, uliotaka waumini kupiga kura ya hapana kwa Katiba Inayopendekezwa.
Alisema kuwaamulia ni kuwadharau kuwa hawana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi wao wenyewe na kuingilia uamuzi wao.
Awali, Jukwaa la Wakristo Tanzania liliwataka waumini wake kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, kuisoma Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya “hapana”.
Taarifa hiyo ilisainiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet.
Waliompinga Pengo
Baada ya Askofu Pengo kutoa msimamo wake, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima alimkashifu na kumtuhumu kusaliti viongozi wenzake wa Kikristo, kitendo kilichosababisha kukamatwa na kuhojiwa na polisi.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment