HUYU NDIYE MWENYE SIFA YA KUGOMBEA URAIS KUPITIA CHAMA CHA ACT KATIKA UCHAGUZI MKUU WA OKTOBA 2015.
ZITTO KABWE.
Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema atalazimika kuachia wadhifa huo kwa mtu mwingine atakayeteuliwa na chama hicho kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Kwa mujibu wa katiba ya chama hicho mwanachama anayeruhusiwa kugombea urais ni lazima awe kiongozi wa chama, wadhifa ambao unashikiliwa na Zitto ambaye hajafikisha umri wa kikatiba wa kugombea urais ambao ni kuanzia miaka 40. Kwa sasa ana miaka 39.
Zitto alitoa kauli hiyo alipozungumza na waandishi wa habari wa Mwananchi katika ofisi za gazeti hili Dar es Salaam juzi.
“Ikitokea hivyo (ACT ikapata mgombea urais, kutoka ndani au nje ya chama hicho), mimi natoka namwachia mtu mwingine na tumeshaamua hivyo, kwetu sisi tatizo siyo cheo. Tukipata mgombea urais leo nitampisha, sitakuwa kiongozi wa chama nitabaki kuwa mwanachama wa kawaida na mjumbe wa Kamati Kuu.”
Hata hivyo, alisema ili mtu huyo apate nafasi hiyo ni lazima aelewe malengo ya chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei, mwaka jana.
“Tunataka mtu ambaye hata tukipata mabadiliko asiwe kikwazo cha hayo mabadiliko. Nasema hivi kwa sababu mnaweza kupata mtu mwingine kuwa kiongozi wa chama lakini baadaye anang’ang’ania na hataki kutoka,” alisema.
Alifafanua kuwa yeye bado ni kijana ana muda mrefu katika siasa na anaungwa mkono sehemu nyingi, hivyo hana haja ya kuharakisha katika kila jambo.
Hata hivyo, akizungumzia watu wa vyama vingine watakaojiunga na chama hicho alisema, “Kati ya watu watakaojiunga ACT au walioonyesha nia kutoka CCM au Ukawa hadi sasa hakuna ambaye ni mgombea urais.”
Alifafanua, “Sisi (ACT) tutasimamisha mgombea wetu wenyewe katika nafasi ya urais au tunaweza kumuunga mkono mgombea wa upinzani.”
Alisema watafanya hivyo kwa sababu hawataki kuua matumaini ya nchi kupata Serikali inayotokana na vyama vya upinzani, “Pale ambapo tutaona ni lazima kuunga mkono wenzetu kuing’oa CCM madarakani tutafanya hivyo. Si kama tunajiunga Ukawa, hapana ni kwa sababu bado hatujawa na mazungumzo nao na kujua nini kitakachotuunganisha.”
Sera na Ilani
Zitto aliziponda sera na ilani za vyama vya siasa nchini kwamba hazina tofauti, zote zina mfumo wa kiitikadi na mwelekeo uleule, isipokuwa kwa ACT Wazalendo.
Alisema kwa uzoefu wake wa miaka 10 akiwa mbunge na miaka saba akiwa mwenyekiti wa kamati za Bunge zinazoshughulikia matumizi ya Serikali, amebaini kuwa nchi haiwezi kusonga mbele bila kubomoa mfumo uliopo.
“Ndiyo maana wakati wa uchaguzi vyama vinasema vitahakikisha vinapunguza matumizi ya Serikali kwa kupunguza malipo ya viongozi wa Serikali, lakini wakiingia bungeni hilo halitekelezwi kwa sababu kila mtu anafaidika na fedha hizo, hawezi kuubomoa mfumo,” alisema.
Alilifananisha suala hilo na posho za wabunge, matumizi ya magari ya kifahari ya Serikali lakini akisema kuwa hayo ni matumizi madogo ya Serikali kati ya mengi inayoyafanya.
Alisema ACT wanaanza kupambana na suala la matumizi ya viongozi mapema, ndio sababu ya kuweka kipengele katika katiba yao kinachowabana viongozi wa chama hicho kutangaza mali zao.
Alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipendekeza uwepo wa miiko ya uongozi na kuiweka katika Rasimu ya Katiba, lakini hakuna chama cha siasa kilichoiweka miiko hiyo katika katiba yake.
“ACT tumeiweka miiko ya uongozi katika Katiba yetu. Tunajua kuwa tutapata wanasiasa wapya vijana na tunataka wajikute wakiwa katika mfumo huo kabla hata ya kuingia madarakani,” alisema.
Mwanasiasa huyo aliyelazimika kung’atuka ubunge baada ya kufukuzwa uanachama na Chadema, alisema kuna wabunge wanachanganyikiwa na fedha wanazopata mara baada ya kupata ubunge kutokana na kukua katika siasa bila kupitia katika vyama vinavyoheshimu miiko ya uongozi.
“Mtu anakuwa mbunge mara baada ya kutoka chuoni, mshahara analipwa Sh11 milioni, mkopo wa gari Sh90 milioni na benki zinatoa mikopo ya Sh200 milioni. Wabunge wanachanganyikiwa.”
Akizungumzia kazi zinazofanywa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana za kufanya ziara mikoani na kuisema Serikali inayoongozwa na chama hicho, alisema, “Uamuzi wa wananchi kumchagua mbunge ni tofauti na uamuzi wanaochukua kumchagua rais. Unaweza ukawa na mgombea mzuri wa ubunge mzuri lakini asiwe mgombea urais mzuri.”
Alisema Kinana anajitahidi lakini anakabiliwa na kazi ngumu ya kurejesha imani ya wananchi kwa CCM kwa maelezo kuwa imeshapotea kwa kiasi kikubwa.
Alisema katibu mkuu huyo angeweza kuifanya kazi hiyo vizuri kama angeshika wadhifa huo miaka 10 iliyopita.
“Kinana anapata watu wengi kwenye mikutano yake, anaongeza mambo mazuri lakini amekuwa mlalamikaji tu. Hatuoni malalamiko yake anayoyatoa kama yanafanyiwa kazi na Serikali yake,” alisema.Alisema kuwa katika Kamati Kuu ya CCM, Rais Kikwete ndio mwenyekiti wa kikao, hivyo Kinana anayeandika miniti hawezi kumfanya jambo lolote.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment