BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HILI LA POMBE ROMBO, TBS ISIKAE KIMYA KUTOKANA NA MADAI YA KUPUNGUZA NGUVU ZA KIUME.



Yapo malumbano ambayo kwa sasa yanaendelea miongoni mwa viongozi nchini, malumbano yanayohusu athari za pombe za kienyeji ambazo zinadaiwa kutengenezwa kiholela wilayani Rombo na ambazo yapo madai kuwa zinapunguza nguvu za kiume na kuathiri mahusiano ya ndoa kwa jamii hiyo.


Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini amewajia juu Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Lemise Kipuya na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Anthony Tesha akiwataka wajiuzulu nyadhifa zao kwa madai ya kushindwa kusimamia sheria wilayani humo.

Selasini alitoa kauli hiyo wiki hii huko Bungeni alipokuwa akizungumzia taarifa ya wanawake wa Rombo inayodai kwamba wanakodi wanaume kutoka Kenya ili wafanye nao tendo la ndoa kwa madai kuwa wanaume wa Rombo sasa wameshindwa kufanya tendo hilo kutokana na pombe za kienyeji ikiwemo gongo kuwapotezea nguvu za kiume.

Inadaiwa kuwa eneo lililoathirika zaidi na unywaji wa pombe haramu na ambazo zinatengenezwa kiholela bila viwango ni la Kikelelwa, lililopo mpakani mwa Kenya na Tanzania, na ndio maana kumekuwepo na madai kuwa wanawake Wilayani humo hukodi wanaume kutoka Kenya kwa ajili ya kufanya nao tendo la ndoa baada ya waume zao kupoteza nguvu kutokana na ulevi.

Katika toleo la wiki iliyopita, nilijenga hoja ya sababu kubwa kwa Watanzania kutambua umuhimu wa kuishi kwa kuthamini viwango, hali hiyo inajumuisha masuala mengi yakiwemo yanayolinda heshima na ustawi wa familia na jamii nzima.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewahi kutoa tathmini ya athari ya vinywaji aina ya juisi ambazo zilikuwa zikizalishwa chini ya viwango vilivyowekwa, na baada ya kupimwa kitaalamu, juisi hizo ziligundulika kuwa na vimelea vyenye athari kubwa kiafya hasa kwa watoto wa umri mdogo, juisi hizo zilidhihirika kuathiri viini vya sehemu ya mwili wa binadamu.

Mbunge Selasini alikanusha na kusema "Siungi mkono unywaji holela wa pombe ambazo hazina viwango vya TBS. Kama kuna mtu ana tatizo la tendo la ndoa ajitokeze tumjue, hili jambo limenifanya nipokee simu nyingi sana" aliongeza kuwa inawezekana hakuna mwananchi wake mwenye tatizo hilo kwa vile hakuna utafiti wala majina ya waathirika.

Hata hivyo yapo maelezo kuwa hata Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, kwamba aliwahi kutoa kauli inayofanana na ya Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Lipuyo aliposema wapo baadhi ya wanandoa wilayani humo wanalala "mzungu wa nne".

Hatua za awali zinazotakiwa kufanywa ni kwa TBS kuchukua sampuli za aina mbalimbali za pombe hizo za kienyeji zinazotengenezwa na kupelekwa katika maabara na kuchunguzwa kikamilifu, ili kubaini madhara yake kwa wanaume kama inavyodaiwa na Mkuu wa Wilaya ya Rombo.

Vipimo vya athari za pombe hizo vitakapotolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), au labda kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ndipo suluhu ya mgongano kati ya Mbunge Selasini na Mkuu wa Wilaya ya Rombo itakapopatikana, aidha viongozi husika wasiendelee kulumbana wakati zipo taasisi zinazoweza kusaidia kufikia mwafaka wa tatizo hilo.

Kwanza pombe za aina hiyo kisheria ni haramu, vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya, na hasa idara ya polisi wanatakiwa kusimamia uhalali wa pombe zinazodaiwa kunywewa na wananchi wa eneo hilo na kuchukua hatua za kisheria.

Kujiweka katika viwango vinavyozingatia afya zetu haitegemei upande wa vyakula na vinywaji peke yake, inaunganisha masuala mengi yakiwemo uvaaji wa nguo zinazokubalika, nguo za mitumba za ndani ni moja ya nguo zilizopigwa marufuku hapa nchini.

Kama ambavyo imedaiwa kuwa pombe za Rombo zimeathiri watumiaji wanaume wengi, nazo nguo za ndani za mitumba zinazouzwa katika masoko mengi ya nguo, pia zimethibitika kuwa na maambukizi ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya ngozi, ingawa athari zake siyo kama za pombe za Rombo.

Tatizo kubwa linaloweza kukwamisha juhudi za kupambana na bidhaa hafifu nchini linatokana na wafanya biashara ambao kimsingi wao wanajali zaidi faida itokanayo na mauzo bila kujali ubora wa bidhaa husika, na ndio maana inadaiwa huko Rombo kuna wazalishaji lukuki wa pombe haramu.

Hatua zilizochukuliwa na TBS za kukabiliana na uingizwaj wa nguo za ndani nchini, ni pamoja na kukamata nguo hizo zilizokuwa zikiuzwa katika masoko ya Ilala, Temeke na kwenye godauni la Kampuni ya Dema iliyoko Mwenge ambako walikuta marobota 28 ya nguo za aina hiyo.

Wakati wa uteketezaji wa nguo za ndani, uliofanyika katika Dampo la Pugu Kinyamwezi jijini Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Roida Andusamile alisema zoezi la kuteketeza bidhaa za aina hiyo litaendelea kila watakapozibaini.

Aidha Bi. Roida alisema Shirika lake limekuwa likichukua muda mrefu kuteketeza bidhaa hafifu kutokana na urasimu wa upatikanaji wa vibali kutoka Mamlaka ya Jiji la Dar es Salaam na Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Hata hivyo Roida alisema kuwa ili kuondokana na ucheleweshwaji wa kuteketeza bidhaa zisizostahili kwa matumizi ya binadamu, tayari Shirika lao limeunda kikosi kazi ambacho watashirikiana kuandaa miongozo ya uteketezaji wa bidhaa husika.

Ili sasa kunusuru afya za Watanzania wengi, na hasa kurejesha mahusiano ya kifamilia kwa wakazi wa Rombo wanaodaiwa kuathirika kwa pombe haramu, TBS waingilie kati ili kujua kemikali za pombe hizo na kuchukua hatua stahiki. Tuwasiliane: 0715-047304 na 0788-483422. CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: