SERIKALI ya wilaya Ulanga imeobwa kuharakisha utengenezaji wa mashine ya X-ray katika hospitali ya wilaya hiyo ili wananchi waweze kupata huduma kwa wakati na kupunguza kwenda wilaya jirani ya Kilombero kupata huduma hiyo.
Endapo mashine hiyo itafanyiwa matengenezo itaborehsa huduma ya afya kwa wananchi na kupunguza kero ya mufa mrefu iliyopo ya kufuatilia vipimo katika hospitali ya Mtakatifu Francis Ifakara wilayani Kilombero.
Wananchi wilayani Ulanga wameibua kero hiyo wakati wakizungumza na timu ya ufuatiliaji wa rasilimali za umma katika sekta ya afya iliyoandaliwa na Asasi isiyo ya kiserikali ya Kijogoo Group for community Development kwa kushirikiana na The Foundation for Civil Society iliyokuwepo wilayani humo.
Cesilia Zamtanga Mkazi wa kitongoji cha Msufini Kijiji cha Nawenge alidai kuwa tatizo kubwa linalowakabili katika hospitali ya wilaya ni kifaa cha x ray ambayo kwa kipindi cha miezi sita imeharibika jambo ambalo wanalazimika kwenda katika hospitali ya Mt. Francis.
Zamtanga alisema ni muda muafaka kwa serikali kuharakisha kutengeneza kifaa hicho kwa kuwa ni muhimu katika kuwasaidia wagonjwa wanapofika katika hospitali hiyo ya wilaya ya Ulanga.
Naye Andason Mfanga alisema kuwa wananchi wengi wamekuwa katika hali ya chini hivyo kukosekana kwa kipimo hicho wakati mwingine husababisha wagonjwa kubaki majumbani kutokana na kukosa fedha ya usafiri kwenda hospitali ya mtakatifu Francis Kilombero kwa ajili ya kupatan huduma.
Kwa upande wake Katibu wa asasi ya Kijogoo, Ramadhan Said alisema kuwa asasi yake awali ilifanya utafiti na kubaini kuna changamoto nyingi ikiwemo baadhi ya watendaji wa halmashauri kufanya kazi kwa mazoea hali inayopelekea utoaji wa huduma kufanywa chini ya kiwango.
Ramadhan alisema kuwa ili kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi wadau wa maendeleo wanapaswa kuunganisha nguvu za pamoja katika kufuatilia rasilimali zinazotolewa na serikali kuu zinawanufaisha wananchi katika kiwango kinachoridhisha.
Asasi ya Kijogoo inatekeleza wa mradi wa ufuatiliaji wa rasilimali za umma katika sekta ya afya katika vijiji vya Kisewe,Epanko na Nawenge ambapo wamelenga kuwajengea uwezo wananchi waweze kufuatilia wao wenyewe rasilimali zote za umma zinapofika katika maeneo yao.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment