KAMATI YA BARAZA LA WAWAKILUSHI YA KATIBA NA UTAWALA BORA LAMMWAGIA SIFA DKT KIKWETE KWA KUTATUA MGOGORO WA KISIASA ZANZIBAR.
KAMATI ya Baraza la Wawakilishi ya Katiba na Utawala Bora, imempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kumaliza mgogoro wa kisiasa na kuimarika kwa amani na utulivu chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Kamati ya Ofisi ya Kusimamia Viongozi Wakuu wa Serikali, Shadya Mohamed Suleiman wakati akisoma maoni ya kamati hiyo katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Ikulu na Utawala bora.
Suleiman alisema wakati Rais Kikwete alipoingia madarakani alisema anasononeshwa na mgogoro wa kisiasa uliopo Zanzibar na kusema ataufanyia kazi kwa kuupatia ufumbuzi wa kudumu.
Alisema kazi iliyofanywa na Rais Kikwete ni kubwa, ambapo mazungumzo ya kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar, yalianza na hatimaye Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliundwa na kufanya kazi zake vizuri hadi leo.
“Tunampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kazi kubwa ya kufanikisha kuleta amani ya kudumu ya kumaliza mgogoro wa kisiasa na hatimaye kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema.
Alisema Rais Kikwete atakumbukwa kwa kazi hiyo wakati akimaliza muda wake wa kipindi cha miaka 10 cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, Hijja Hassan Hijja (CUF) alisema akiulizwa jambo gani lililofanywa na Rais Kikwete, ambalo hatalisahau katika maisha yake ni uwezo wake wa ushawishi wa kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar.
Hijja alisema Kikwete anastahiki kupongezwa kwa sababu ya kufanya kazi kubwa ya kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar, ambao ulikuwa ukichafua jina la Tanzania kama kisiwa cha amani na utulivu mkubwa.
Alisema, leo hii tunashuhudia wananchi wanaishi kwa pamoja na kushirikiana pamoja na kufanya kazi za kuleta maendeleo, kama ilivyokuwa zamani, kutokana na kuunganishwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Mheshimiwa Naibu Spika… mimi nikiulizwa jambo kubwa lililofanywa na Rais Kikwete ambalo sitalisahau ni suala la kumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar na wananchi kuishi kwa amani na utulivu,” alisema.
Aliitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kulinda matunda hayo kwa vitendo na kamwe watu wenye nia ya kutaka kuharibu mafanikio hayo, wasipewe nafasi hata kidogo kufanya wanavyotaka.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment