Neno ‘shemeji’ lilitawala zaidi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi yaliyofanyika kitaifa mkoani Mwanza baada ya walimu kubeba bango lenye maandishi yanayosomeka “Shemeji unatuachaje?”. Maandishi hayo yalimlenga Rais Jakaya Kikwete.
Tena walimu hao wakiwa wanapita mbele ya Rais, walilielekeza bango hilo upande wake ili aweze kulisoma vizuri. Walimu wamekuwa wakimuita Rais Kikwete shemeji kutokana na mke wake, Mama Salma, kutoka katika kada hiyo.
Mama Salma Kikwete kabla ya mume wake hajawa Rais alikuwa ni mwalimu wa shule ya msingi, akiwa amefundisha shule kadhaa, ikiwemo ya Mbuyuni, jijini Dar es Salaam.
Ujumbe huo wa walimu unatokana na mgogoro wao wa muda mrefu na Serikali juu ya madai na malimbikizo ya madeni yao.
Njia waliyoitumia walimu ililenga kuhoji hatima ya masuala yote wanayoyahitaji. Sababu kubwa ni kubaki kwa miezi michache kabla ya Rais Kikwete kumaliza awamu yake ya pili na kukabidhi kijiti kwa rais mwingine. Walimu hao bado wanaona matatizo yao hayajatatuliwa katika kipindi chote cha miaka 10 ya utawala wa Rais Kikwete.
Kilichofanywa na walimu hawa kinafanana na madai yanayotolewa na watu wa kada mbalimbali nchini, wanaotaka Serikali kuiboresha Katiba ya sasa kutokana na kuwapo kwa uwezekano mdogo kwa Katiba Inayopendekezwa kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Mpaka sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imeahirisha Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa na haijulikani itapigwa lini, huku uandikishaji wa wananchi katika daftari la wapigakura ukiendelea kusuasua.
Mambo hayo manne ambayo yanapigiwa kelele kuboreshwa ni ushindi wa urais kuamuliwa kwa asilimia zaidi ya 50, mgombea binafsi katika nafasi za udiwani, ubunge na urais, tume huru ya uchaguzi na urais kupingwa mahakamani.
Nakumbuka Rais Kikwete aliwahi kukutana na viongozi wa vyama vya siasa chini ya kivuli cha Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kukubaliana juu ya mambo hayo ili kufanikisha uchaguzi huo kabla ya kupitishwa kwa Katiba Mpya, lengo likiwa ni kuondoa uwezekano wa vurugu.
Walikubaliana kuwa iwapo uchaguzi wa mwaka huu utafanyika kwa kutumia Katiba ya 1977, Bunge lingekutana Novemba mwaka jana kufanya marekebisho hayo ya 15 ya Katiba na endapo hilo lingeshindikana, basi lingekutana Februari, jambo ambalo pia halikufanyika. Utekelezaji wa masuala hayo utawezekana iwapo Serikali itawasilisha marekebisho hayo bungeni ili yajadiliwe kwa dharura katika mkutano wa Bajeti wa mwisho wa Bunge la Kumi, kwa kuwa uwezekano wa kupata Katiba Mpya kabla ya uchaguzi ni kama haupo.
Hili ni jambo la msingi ambalo Serikali inatakiwa kutolipuuza kwa sababu kwa kipindi kirefu watu wanadai uwepo wa mgombea binafsi. Kitendo cha kufanyika kwa uchaguzi wa mwaka huu bila kuwepo kwa jambo hilo kunaweza kuwagawa wananchi.
Kinachotakiwa kufanyika sasa ni Serikali kuahirisha upigaji wa Kura ya Maoni hadi mwakani, iongeze nguvu katika uandikishaji wa wananchi katika Daftari la Wapigakura na kuiboresha Katiba ya sasa katika maeneo hayo.
Kwa sasa, kuna baadhi ya makundi na watu wanaoamini kuwa Katiba inayopendekezwa imetupilia mbali baadhi ya mambo yaliyopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba yaliyotokana na maoni ya wananchi, hivyo wanaipinga na baadhi yao wanatishia kutoipitisha.
Hili ni jambo la kusikitisha, lakini siyo jambo la kupuuza. Katiba siyo kitu kinachotegemea kura, bali inatakiwa iwe na muafaka. Katiba ya nchi ndiyo sheria mama na msingi wa kuendesha nchi na uzuri wake, sharti iungwe mkono na wengi. Katiba inayopingwa na kundi kubwa la watu, ni chanzo cha mfarakano kwenye nchi.
Itakuwa ajabu sana hata yale mazuri yasiyo na ubishi yasitumiwe kwenye uchaguzi huo.
Katika kila Uchaguzi Mkuu, tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, maeneo hayo manne niliyoyataja ni kati ya mengi yanayolalamikiwa na wanasiasa na wananchi kuwa kukosekana kwake katika Katiba kunaufanya uchaguzi huo kutokuwa wa kidemokrasia.
Haiwezekani wananchi wakaendelea kuiamini Nec ambayo watendaji wake ni wateule wa rais ambaye ndiye mwenyekiti wa chama kilichopo madarakani.
Haiwezekani wananchi wakaendelea kukosa fursa ya kugombea kama wagombea huru, yaani wasiobanwa na chama chochote cha siasa. Jambo hili ni zito na tayari hukumu imeshatolewa na Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika (AfCHPR) Juni 13, mwaka 2013 ikiitaka Katiba ya Tanzania imtambue mgombea binafsi katika uchaguzi wa udiwani, ubunge na urais.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila. Hivyo kuendelea kusuasua katika utekelezaji wa suala hili na mengine kunaifanya Serikali ionekana kama inabana masuala fulani kwa masilahi ya wachache.
Sijui, ila kama ilivyo kwa walimu. Rais Kikwete utatuachaje juu ya mambo haya manne nasubiri kuona hatima yake. 0754 597315.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment