SAKATA LA KUMPINDUA RAIS NKURUNZIZA, HALI YA MJI MKUU WA BURUDNI, BUJUMBURA YAZIDI KUWA TETE
Hali ilivyokuwa katika sehemu ya mji mkuu wa Bujumbura nchini Burundi jana. (Picha na AFP).
HALI ya Burundi imezidi kuwa tete huku makundi mawili hasimu ya wanajeshi, yamekuwa yakipigana, kila moja likitaka kutawala jiji la Bujumbura.
Mapigano hayo ni kati ya wanajeshi wanaomtii Rais Pierre Nkurunziza, ambao wanapambana na wanajeshi wanaompinga, ambao wanamuunga mkono mwanajeshi aliyetangaza mapinduzi, Meja Jenerali Godefroid Niyombare.
Ofisa Mwandamizi wa Jeshi nchini humo, alisema wanajeshi wanaomtii Rais Nkurunziza wamefanikiwa kudhibiti na kurejesha maeneo muhimu ya jiji hilo chini ya utawala wa Serikali, ukiwamo uwanja wa ndege.
Hata hivyo, viongozi wa wanajeshi wanaompinga Rais huyo, wameendelea kudai kuwa wameipindua Serikali ya nchi hiyo.
Hali ya machafuko nchini humo, ilianza baada ya kiongozi huyo kutangaza kuwa ana nia ya kuwania tena kipindi cha tatu cha urais, jambo ambalo wapinzani nchini humo wamedai ni kinyume cha Katiba.
Kwa mujibu wa mashuhuda nchini humo, milio ya risasi na mabomu imekuwa ikisikika usiku kucha kuanzia juzi katika mapigano baina ya vikosi vinavyomtii Rais na vile vinavyotaka mapinduzi, lakini hadi sasa haijafahamika nani aliyefanikiwa kulidhibiti jiji hilo.
“Hatujaweza kulala kutokana na hofu tuliyonayo, milio ya milipuko na risasi imekuwa ikisikika kila sehemu, watu anaogopa kwa kweli,” mmoja wa mashuhuda aliwaambia waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari ndani ya kikosi kinachomtii Rais Nkurunziza, jeshi hilo limeweza kurejesha maeneo muhimu chini ya Serikali kama vile Ikulu, Redio na Televisheni ya Taifa na uwanja wa ndege.
Mitaa ya jiji hilo imejaa askari na polisi wanaomtii Rais na hadi majira ya jioni uwanja wa ndege, ulifunguliwa tayari kwa kutoa huduma za usafiri.
Hata hivyo, bado mapigano yanaendelea eneo ambapo televisheni na redio za taifa zipo, huku vikosi vinavyotaka mapinduzi vikijaribu kuingia ndani ya vituo hivyo vya habari.
Kila kikundi kinataka kudhibiti vituo hivyo vya utangazaji wa taifa, kwa kuwa ndio vyombo vya habari pekee vyenye uwezo wa kusikika hadi nje ya jiji hilo la Bujumbura.
Tayari Mkuu wa Majeshi na Rais Nkurunziza wametangaza na kudai kuwa jaribio la kupindua nchi hiyo, limeshindikana.
Hata hivyo, kauli hizo zimekuwa zikipingwa na viongozi wanaotaka mapinduzi nchini humo, na mmoja wao alisema kuwa wamefanikiwa kudhibiti takribani mji wote wa Bujumbura.
Msemaji wa kundi hilo la waasi, Venon Ndabaneze, alisema askari wanaotawanywa katika jiji hilo, wote wako upande unaotaka mapinduzi na si wanaomtii Rais Nkurunziza.
Juzi, Meja Jenerali Godefroid Niyombare, aliyekuwa Mkuu wa Usalama, alitangaza kumpindua Rais Nkurunziza akiwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, hali iliyozua shangwe kwenye mitaa mbalimbali jijini humo.
Niyombare alifukuzwa kazi na Rais Nkurunzinza Februari mwaka huu. Majengo ya kituo cha binafsi cha Televisheni Renaisance ya Burundi, iliyotumiwa na Meja Jenerali Niyombare, yameripotiwa kuharibiwa vibaya usiku wa kuamkia jana.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kituo hicho, Innocent Muhozi, moja ya ofisi zake ilichomwa moto usiku huo na kusababisha kila kilichokuwepo ndani kuteketea.
Jenerali Niyombare, alitoa tangazo hilo, saa chache tu baada ya Rais huyo kupanda ndege kwenda Dar es Salaam Tanzania kuhudhuria mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliojadili suala hilo la Burundi.
Hata hivyo, iliripotiwa kuwa baada ya tangazo la kupinduliwa kwake, Nkurunziza, alirejea Burundi bila kuhudhuria mkutano huo, lakini alipofika Bujumbura alilazimika kurejea Dar es Salaam baada ya Uwanja wa Ndege wa Bujumbura kufungwa.
Habari zilizopatikana kutoka BBC baadaye jana jioni zilidai wanajeshi watano walikuwa wameuawa, silaha nzito zilikuwa zikitumika, mirindimo ya risasi ilisikika kila kona na waandamanaji walilazimika kujifungia ndani.
Ofisa Mwandamizi wa Usalama wa Taifa kutoka Ikulu ya Dar es Salaam, alipozungumza na AFP, alikiri kuwa Rais Nkurunziza bado yupo Tanzania, jijini Dar es Salaam, lakini haifahamiki ni sehemu gani alipo.
Nkurunzinza yuko wapi?
Suala sehemu alipo Rais Nkurunziza baada ya kufanyika jaribio la kumpindua nchini kwake, limeendelea kuwa tete baada ya Tanzania kusema haijui alipo.
Hatua hiyo imetokana na tetesi kuwa Rais huyo yupo nchini baada ya kuhudhuria mazungumzo ya kutafuta amani kwa marais wa nchi za Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam na baadaye kutangazwa nchi hiyo kupinduliwa na kueleza kushindwa kurejea nchini mwake.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo.
Awali , alipoulizwa alipo Rais huyo, alisema hawezi kujibu swali hilo lakini baadaye alisema hajui huku akiondoka na kucheka.
Membe alisema baada ya tamko la viongozi wa nchi za Afrika Mashariki, kulaani jaribio la kufanya mapinduzi katika nchi hiyo zaidi ya hayo Baraza la Mawaziri lililokutana kwa siku mbili Jumanne na Jumatano, litakutana tena Jumatatu wiki ijayo na kufanya tathmini ya hali halisi ya Burundi kwa siku tatu hizi mpaka Jumatatu.
“Kwa sasa sitaweza kuzungumza jambo jingine lolote kuanzia sasa mpaka Jumatatu jioni baada ya kikao cha baraza la mawaziri wenzangu, ambapo tutajua mambo ya kuzungumza.”
“Naomba kuwatahadharisha Watanzania kuwa hali ni tete Burundi lolote unalosema wewe na kudhani dogo linaweza kugharimu maisha ya mtu naomba mnielewe na mkae mkielewa haya mengine tutazungumza siku hiyo ya Jumatatu,” alisisitiza.
Alisema wananchi wa Burundi wako katika matatizo na vizuri kuvuta subira, badala ya kuendelea kuzungumza, kwani uhai wa mtu unaweza kuwa matatani.
Membe alipoulizwa alipo Rais wa Burundi, kwani inasemekana alirudi nchini Tanzania baada ya ndege yake kushindwa kutua nchini kwake , alisema yeye hajui.
Alisema hali ya Burundi ni tete na sababu hiyo, walikutana kutafuta ufumbuzi wa kudumu na wananchi waache kufanya ghasia na badala yake watulie na kuchagua viongozi wao kwa amani.
Alisema imeelezwa kuwa jaribio la jana la baadhi ya askari kutaka kuipindua Burundi, lililaaniwa na viongozi wote wa Afrika. Alisema Afrika haitaki nchi yoyote, kwa sababu zozote, kuhalalisha kuchukua madaraka kwa njia ya mtutu wa bunduki.
Wakimbizi wafa kwa kipindupinduKigoma
Wakati hali ya utawala nchini Burundi ikiwa tete , wakimbizi wa nchi hiyo waliopo mkoani Kigoma, wameanza kupatwa na majanga mengine baada ya kuripotiwa watu wanne kufa kwa ugonjwa wa kipindupindu.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Leonald Subi alisema mjini Kigoma kwamba watu wawili walikufa wakiwa tayari wanaumwa ugonjwa huo na kufariki hapa nchini.
Alisema watu wawili wengine, walipatwa na ugonjwa huo wakisubiri msaada wa kibinadamu katika kijiji cha Kagunga wilaya Kigoma, mwambao wa Kaskazini wa Ziwa Tanganyika.
Subi alisema kuwa kwa sasa hali ya upatikaji wa huduma za kibinadamu, ikiwemo chakula, maji, mahala pa kujihifadhi na huduma ya choo ni mbaya sana kutoka na idadi kubwa ya wakimbizi hao kuwepo kijijini hapo kwa kipindi kifupi na hivyo kijiji hicho kuzidiwa katika kuwapatia huduma watu hao.
0 comments:
Post a Comment