Na Juma Mtanda.
Mashindano ya umoja wa michezo kwa shule za sekondari Tanzania (UMISETA) ngazi ya mkoa imeanza kutimua vumbi katika uwanja wa jamhuri kwa kushirikisha wilaya saba zinazounda mkoa huo mkoani hapa.
Katika michezo ya ufunguzi timu ya soka ya wavulana Manispaa ya Morogoro iliisambatarisha wenzao wa wilaya ya Kilosa kwa kuwabamiza bao 5-0 huku wasichana wao nao wakikiona cha mtema kunde kwa kufungwa vikapu 34-9 katika mchezo wa netiboli.
Mshambuliaji wa timu ya soka ya Manispaa, Yahaya Machupa alifunga bao tatu pekee yake huku Fidoline Emmanuel akifunga bao mbili katika ushindi huo wa bao 5-0.
Kwa upande wa soka la wasichana Mvomero ilishindwa kutamba mbele ya Ulanga kwa kulazimisha sare ya 0-0 huku katika michezo mingine wilaya ya Kilombero ilikubali kichapo cha kufungwa vikapu 53-5 na Morogoro Vijijini katika mchezo wa netiboli.
Wakati Kilombero ikibugia vikapu hivyo, Morogoro Vijijini hiyo hiyo ilionyesha tena uhondari wake katika mchezo huo kwa kuiadhibu wasichana wenzao wa wilaya ya Gairo kwa vikapu 37-3 kabla ya Mvomero nayo kupata ushindi wa vikapu 18 dhidi ya 15 vya Ulanga.
Mtaribu wa mashindano ya Umiseta ngazi ya mkoa huo, Maximillian Lipingu alieleza kuwa mashindano hayo yanashirikisha michezo mbalimbali ikiwemo mchezo wa soka ikijumuisha wavulana na wasichana.
Lipingu alitaja michezo mingine kuwa ni netibali, basketiboli wasichana na wavulaana, mpira wa mikono wavulana na wasichana, mpira wa wavu wasichana na wavulana, riadha kuanzia mita 100 hadi mita 3000.
“Michezo imeanza leo (jana) na lengo letu ni kusaka wachezaji wenye vipaji ambao watachaguliwa katika kila mchezo ili kuunda timu ya mkoa yenye uwezo wa kufanya vizuri katika michezo ya Umiseta ngazi ya taifa ili mkoa wa Morogoro iweze kuibuka washindi wa kwanza na kurudi na vikombe, medali na zawadi mbalimbali na uwezo huo upo kutokana na kusheheni kwa vipaji.”alisema Lipingu.
0 comments:
Post a Comment