BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAANDISHI WA HABARI WAMPIGIA MAGOTI RAIS KIKWETE ILI ASISAINI MISWADA YA TAKWIMU NA MTANDAO.


Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (Misa-Tan), Simon Berege.

Wadau wa habari, wamiliki wa vyombo vya habari, wahariri na waandishi wa habari nchini, wamepinga vikali miswada ya Takwimu na Makosa ya Mtandaoni ambayo ina kandamiza uhuru wa habari na kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutoisani, badala yake irudi bungeni kujadiliwa na wadau kutoa maoni.


Ombi hilo walilitoa jana wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, yaliyofanyika hapa nchini mjini Morogoro, chini ya kauli mbiu ya ‘Usalama wa vyombo vya habari katika zama za kidigitali, uandishi makini, usawa wa kijinsia na faragha’.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (Misa-Tan), Simon Berege, alisema pamoja na serikali kuonyesha nia ya kuruhusu uhuru wa kujieleza na wa kupata taarifa kupitia Katiba inayopendekezwa, serikali hiyo hiyo imeanza kufanya mambo yenye kila dalili za kuminya uhuru wa wananchi na vyombo vya habari wa haki ya kupata taarifa.

“Miswada hii ina vipengele vingi vinavyoleta ukiritimba katika upatikanaji wa taarifa na kuminya uhuru wa vyombo vya habari kufanya kazi zake,” alisema na kuongeza:

https://hivisasa.co.tz/wp-content/uploads/2014/07/rais-kikwete1.jpg  

Dkt Kikwete.

“Pamoja na kwamba Rais kupitia Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu ameshatoa msimamo wa kusaini miswada hiyo, sisi bado tunatoa rai kwa kumsihi (Rais) kutosaini bali irudishwe bungeni na kuwasilishwa upya kwa utaratibu wa kawaida ili wadau waweze kuijadili na kutoa maoni yao yatakayoboresha.”

Alisema hakuna asiyetambua kipindi cha uongozi wa Rais Kikwete amekuwa mliberali, anayependa kusikiliza maoni na kuyafanyia kazi, hivyo kusainiwa kwa sheria hizo kutatia dosari sifa nzuri aliyojiwekea kwa wapenda demokrasia, ndani na nje ya nchi.

“Jambo moja la msingi ambalo watendaji na viongozi wetu wa serikali na hata wa taasisi na mashirika binafsi wanapaswa kukumbuka ni kwamba, ulimwengu kwa sasa uko kwenye zama za taarifa. Kuminya taarifa ni kuwafanya wananchi wapitwe na zama hizi ambazo zinampa nguvu na ushindi zaidi mtu mwenye taarifa sahihi kuliko asiye nazo, tujihadhari kutokufanya mambo yatakayosababisha zama hizi zitupite kama zilivyotupita zama za mapinduzi ya viwanda,” alisema.

Berege alisema harakati za serikali kutaka kufifisha uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata taarifa zinafanyika huku tafiti zikionyesha kwamba nchi za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania zinaendelea kuporomoka kwenye viwango vya kidunia vya kupima hali ya uhuru wa vyombo vya habari.

Berege alitolea mfano wa waandishi kutishwa, kupigwa na kunyanyaswa wakiwa kazini ikiwamo gazeti hili Julai, 2014 Mhariri Mtendaji, Jesse Kwayu (NIPASHE) na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa The Guardian Limited, Kiondo Mshana, kuitwa polisi kuhojiwa kuhusiana na habari kuhusu madai ya rushwa miongoni mwa askari wanaodhibiti ujambazi kwa kutumia pikipiki, lakini hawakuhojiwa.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, alisema mwaka huu ni wa kipekee kwa kuwa unahitimisha kipindi cha utawala wa miaka 10 ya serikali ya awamu ya nne ikiwa na misukosuko ya vyombo vya habari na waandishi wa habari.

“Wanahabari na wahariri wameingia kwenye misukosuko mikubwa, kupoteza maisha, kujeruhiwa na kukamatwa na polisi, polisi kuvamia vyombo vya habari kuwapiga na kuwajeruhi waandishi na kumwagiwa tindikali na kufikishwa mahakamani,” alieleza na kuongeza:

“Tunahitimisha jinamizi la mateso kwa wanahabari na waandishi, viongozi wanasema wasichomaanisha na kutishia waandishi wa habari…sheria kandamizi zimepitishwa na Bunge, hili ni jinamizi hatari na tishio kwa uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kupata habari.”

Kibanda alikumbushia hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu dhidi ya kesi ya uchochezi iliyokuwa inamkabili yeye na wenzake kuwa kwa mara ya kwanza mahakama ilithibitisha kuwa serikali ilifungua kesi hiyo kwa misingi ya uonevu.

Aidha, aliutaka Umoja wa Ulaya (EU) kuingilia kati na kutoa tamko kwani wakati wa kuumizwa, kuteswa na kujeruhiwa kwake (Kibanda), Waziri mmoja alitoa taarifa potofu kwa mataifa ya nje kuwa alipatwa na janga hilo kutokana na sababu za maisha yake binafsi na si masuala ya kazi.

“Ninaitaka EU ije na kauli thabiti, kukaa kimya ni kuruhusu serikali ijayo kuendeleza matukio haya zaidi ya ilivyosasa,” alisema.

Mkurugenzi wa Mfuko wa Waandishi wa Habari Tanzania (TMF), Ernest Sungura, alisema wamekumbana na mkono wa vyombo vya dola mara kadhaa na kwamba ameshahojiwa mara tatu, watumishi wake mara mbili, polisi kufika kwenye ofisi hizo na kutaka ushahidi na waliponyimwa waliahidi kutumia nguvu za kisheria kuupata.

Alisema misukosuko hiyo imetokana na TMF kufadhili vyombo vya habari na waandishi wa habari za uchunguzi ambazo zinagusa maslahi yao moja kwa moja.

Mwakilishi wa Shirika la Ujerumani (Kas), Stefan Reith, alisema Tanzania inahitaji sheria zinazotetea uhuru wa habari na vyombo vya habari kwa utetezi wa demokrasia.

“Serikali imesema Sheria ya Takwimu na Mitandao ni kwa ajili ya usalama wa nchi, lakini cha kujiuliza ni kwa usalama wa nchi au usalama wa watawala?” alihoji.

Makamu wa Rais wa Muungano wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Jane Mihanji, alisema asilimia 80 ya waandishi hawana mikataba na wanapewa malipo duni na hawana vitendea kazi.

Alisema wanaangalia uwezekano wa kuanzisha vyama vya wafanyakazi ili kupata stahiki zao na kwamba wataendelea kudai uhuru wa waandishi wote na mmoja mmoja.

Katibu Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Henry Muhanika, alisema chama chake kitaunga mkono tamko ambalo lilitarajiwa kutolewa baada ya mkutano huo jana jioni.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Kiongozi wa mabalozi wa EU nchini, Balozi Filiberto Bregondi, alisema EU itaendelea kuishawishi serikali kuheshimu haki za binadamu, haki ya kupata taarifa na huduma kwa vyombo vya habari, kwa maendeleo endelevu ya taifa lenye misingi ya demokrasia na utawala bora.


Naye Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini (UN), Balozi Alvero Rodriguez, alisema mwaka huu ni muhimu kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari kuangalia mazingira ya uandishi wa habari katika chaguzi zijazo na sheria mpya na wajibu wa kuimarisha ulinzi na usalama. CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: