AHADI YA NYINGINE YA EDWARD LOWASA ENDAPO CCM WATAMPISHA KUGOMBEA URAIS NA AKISHINDA WAMACHINGA KUPATA NEEMA.
Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa amesema akichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakomesha tabia ya halmashauri kuwafukuza wafanyabiashara ndogondogo maarufu kwa jina la wamachinga mitaani na badala yake atawawekea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao ili waweze kujikwamua na umasikini.
Lowasa aliyasema hayo jana jijini hapa wakati akitafuta wadhamini kwa ajili ya kumuwezesha kuteuliwa na CCM kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Akiwa mkoani hapa Lowassa alidhaminiwa na wanachama 53,116 kutoka katika wilaya zote za mkoa wa Mbeya, ambao walimkabidhi fomu za udhamini kwenye ofisi za CCM mkoa wa Mbeya.
Akiwashukuru wanachama hao, Lowassa alisema kuwa anauchukia umasikini na hivyo dhamira yake ya kugombea urais inalenga kuwakwamua Watanzania na umasikini unaowakabili.
“Nauchukia sana umasikini, nagombea urais kuondoa umasikini wa taifa letu kwa sababu ninaweza, ninatosha kukabiliana na umasikini wa nchi hii,” alisema Lowassa.
Alisema kuwa akifanikiwa kuingia madarakani ataendesha nchi mchakamchaka katika kutafuta maendeleo ya wananchi na kutokomeza kabisa umasikini kwa kuanza kuwatetea wafanyabiashara wadogo ambao wamekuwa wakifukuzwa na halmashauri nyingi nchini kila wanapoonekana wakiendesha biashara zao.
“Nitaendesha nchi hii kwa speed ili kuondoa umasikini, wanyonge wanaofukuzwa na halmashauri nitawatetea wote, msiwafukuze bali wapeni kazi za kufanya kwani kama ninyi mnakula mikate, waacheni wao wale mihogo,” alisema Lowassa.
Aidha, Lowassa aliahidi kuboresha biashara za mpakani ili kuitoa fursa ya wananchi wa maeneo ya mpakani kama ilivyo kwa mkoa wa Mbeya kunufaika na mazingira hayo kwa kufanya biashara wakiwa huru na wenzao wa nchi jirani.
Aliwahakikishia wakazi wa Mbeya kuwa akifanikiwa kuingia madarakani ataendesha nchi kwa speed (kasi) kali na kwamba asiyeweza kuendana na kasi hiyo ataondolewa kwa maamuzi magumu.
Aliwashukuru wana-CCM wa Mkoa wa Mbeya kwa kujitokeza kwa wingi kumdhamini, ambapo alisema kuwa wapo watu wameanza kumwonea wivu kwa jinsi anavyopata idadi kubwa ya wadhamini kila anakokwenda.
Alisema kuwa kwa wingi wa watu wanaojitokeza kumdhamini anaamini kuwa tayari amefunga goli lisilokuwa na shaka kama wanavyofunga wachezaji mahili wa soka nchini Hispania, Reonel Messi WA Bacelona na Christiano Ronaldo wa Real Madrid.
Aidha, aliwataka wananchi kujiandikisha na kutunza shahada zao za kupigia kura ili wazitumie kumchagua pale atakapokuwa ameteuliwa na CCM ili azma yao ya kumchagua kuwa rais iweze kitimia.
Akimkaribisha kuzungumza na wana-CCM wa Mkoa wa Mbeya, Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya, Mwangi Kundya alisema kuwa Lowassa ni kiongozi mwenye rekodi nzuri ya utendaji kazi hivyo anastahili kuungwa mkono katika mbio hizo za urais.
“Tmani ya kiongozi haitokani na uzoefu wake wa miaka mingi kazini, bali unatokana na kazi nzuri aliyowahi kuwafanyia wale anaowaongoza, Lowassa ni kiongozi mwenye sifa hiyo na anastahili,” alisema Kundya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mstaafu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita alisema kuwa wananchi wa Tanzania wamechoka na siasa za kulalamika, hivyo wanahitaji kiongozi anayeweza kutoa maamuzi badala ya kulalamika.
Alisema kuwa miongoni mwa wana-CCM wote waliojitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuwania urais mwaka huu, kiongozi mwenye sifa hiyo ni Lowassa pekee. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment