CCM YACHIMBIWA MKWARA MZITO, WAITAKA KUMCHAGUA MTU MWENYE FIKRA NA AKILI YA KUIONGOZA TANZANIA NA SIYO KUCHAGUA MTU KWA KIGEZO CHA FEDHA, NO.
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameshauriwa kumchangua mtu mwenye fikra na akili za kuliongoza taifa na siyo kuangalia ukubwa wa mwili wa mtu na fedha alizo nazo.
Ushauri huo ulitolewa jana mjini hapa na Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Wilaya ya Singida Mjini, Swalehe Msuli, wakati akihutubia mkutano wa wananchama wa CCM, waliojitokeza kumdhamini kada wa chama hicho, January Makamba, anayeomba kuteuliwa kugombea urais.
Msuli alisema uongozi siyo mwili mkubwa wa mtu wala fedha, bali mgombea anatakiwa kuwa na fikra sahihi na mipango sahihi ya kuwavusha Watanzania walipo na kuwasogeza mbele kimaendeleo.
"Makamba amezungumza mambo mengi mazuri ambayo yanaonyesha amekomaa kisiasa na anaweza kuliongoza taifa hili kwa kuwa anaonyesha anafahamu matatizo ya watu na anajua kuyachambua," alisema.
Alisema mgombea anayetumia fedha nyingi kununua watu ili wamchague ni hatari kwa kuwa akiingia Ikulu hatajua watu wabaya na wazuri waliomzunguka na hivyo hatua hiyo itamfanya ashindwe kutoa maamuzi sahihi.
"Ukichaguliwa kwa fedha zako, lazima utakuwa umezungukwa na watu wa aina hiyo hivyo itakuwa vigumu kwako kufikiria matatizo ya Watanzania na kuyapatia majibu sahihi," alisema.
Kwa upande wake, Makamba akizungumza na wanachama waliojitokeza kumdhamini, alisema taifa linahitaji kiongozi wa kisasa na siyo kiongozi wa kisiasa.
Alisema kwa muda wa miaka 50 ya uhuru, bado kumekuwa na malalamiko mbali mbali kwa Watanzania kuhusu maisha yao na kwamba yeye anayo majawabu.
Alisema Watanzania wanahitaji kiongozi ambaye akipanda jukwaani hahitaji kutetea kwanza kabla ya kuanza kuhutubia bali wanahitaji mtu asiye na dosari yoyote ili iwe rahisi kwa CCM kushinda.
Makamba alisema anajua changamoto za mkoa wa Singida kwa kuwa amezaliwa huko na kwamba muda wa kuliongoza taifa ni sasa na siyo baadaye.
Kada huyo alipata wadhamini zaidi ya 8000 kutoka wilaya za mkoa wa Singida. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment