Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani akiondoka makao makuu ya CCM Dodoma jana, baada ya kuchukua fomu za kuomba kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia chama hicho. Picha na Edwin Mjwahuz
Dodoma. Jaji Mkuu wa zamani wa Tanzania, Augustino Ramadhan, mmoja wa watu waliokuwa wakitajwa kuwa na nia ya kuingia kwenye mbio za urais, jana alichukua fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kugombea nafasi hiyo, akisema “chema chajiuza, kibaya chajitembeza”.
Jaji Ramadhan ni mmoja wa makada wengi wa CCM ambao wamekuwa wakitajwa kwa muda mrefu kuwa wanaweza kuomba ridhaa ya CCM kuwania nafasi hiyo ya kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano baada ya Rais Jakaya Kikwete kuachia ngazi mwishoni mwa mwaka.
Ubashiri huo ulitimia jana wakati brigedia huyo wa zamani alipofika ofisi za makao makuu ya CCM mjini hapa, akisindikizwa na familia yake, kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya wanachama kuwania urais zikiwa zimesalia siku 15.
Jaji Ramadhan, ambaye ni rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, alifika katika ofisi hizo saa 6:30 mchana akiwa ameambatana na mke, watoto wake watatu, mdogo wake na msaidizi wake.
“Hao ndio watu niliokuja nao sikutaka makeke kwa sababu waswahili wanasema chema chajiuza, kibaya kinajitembeza,” alisema baada ya kuwatambulisha watu alioongozana nao.
Jaji Ramadhan, ambaye hakutaka kuzungumzia mikakati yake lakini akakaribisha maswali ya waandishi wa habari, anakuwa kada wa 36 kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo, ambayo kama atapewa atakuwa pia mwenyekiti wa CCM.
Akijibu maswali , Jaji Ramadhan alisema: “Nina uwezo wa kuwatumikia wananchi wenzangu, tuende huko tunakotaka, tujenge Taifa tunalolitaka na kunyanyua hali za binadamu. Nimefanya hivyo katika masuala ya haki nimekuwa Jaji na Jaji Mkuu Zanzibar na Muungano,” alisema Jaji Ramadhan ambaye anajulikana zaidi kutokana na hukumu ya kesi iliyofunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila ya kutaka mahakama itambue mgombea binafsi.
“Hakuna hata mtu mmoja anayeweza kuniambia kwamba nilichukua rushwa au huyu nilimuangamiza au nilimwonea mtu sasa. Nilipata nafasi hiyo na leo nataka nafasi kubwa zaidi ya kiuongozi nchi nzima.”
Katika kesi hiyo, Jaji Ramadhan na jopo lake walisema uamuzi huo unatakiwa ufanywe na Bunge, na kuibua mjadala mkubwa.
Jaji Ramadhan alikuwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu, Agosti 1969 wakati akisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na alipomaliza alijiunga na Jeshi la Wananchi (JWTZ), huku akiwa mwanachama wa Tanu.
Aliendelea kuwa mwanachama wa Tanu hadi mwaka 1992 wakati mabadiliko ya Katiba yalipozuia wanajeshi na majaji kuwa wanachama wa vyama vya siasa baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, lakini alirejea CCM baada ya kustaafu mwaka 2011.
“Upande wa Jeshi nilikaa hadi nilipokuwa brigedia na nilitoka tena kwa sababu ya sheria. Katiba ilipoleta hoja ya mtu kutokuwa mwanajeshi na Jaji nikaamua kuacha,” alisema.
Alipoulizwa kama kuna makada anawahofia katika mbio za urais, Jaji Ramadhan alisema: “ Niliacha jeshi nikiwa na cheo cha Brigedia Jenerali sijui kama Brigedia Jenerali anaogopa, au sivyo hamna jeshi. Kama Brigedia Jenerali anaogopa, hamna jeshi, kwa hiyo siogopi mtu.”
Katiba Pendekezwa
Kuhusu mapendekezo yaliyoondolewa kwenye Rasimu ya Katiba, Jaji Ramadhan, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema hawezi kufanyia marekebisho Katiba Inayopendekezwa kwa kuwa kazi ya Tume yao ilimalizika ilipokabidhi Rasimu ya Pili kwa Rais Jakaya Kikwete.
“Pale kazi yetu ilikwisha na ilifuata kazi ya Bunge Maalumu la Katiba nalo limemaliza kazi yake kilichobaki ni wananchi wapigie kura ya ndio ama siyo,”alisema.
“Kwa hiyo uamuzi wa wananchi ndio tunaousubiri.”
Alisema endapo atateuliwa na chama chake na hatimaye kuchaguliwa na wananchi kuwa Rais, atatekeleza siasa za chama chake.
“Kikubwa ni kuhakikisha ninaitekeleza siasa, kwa sababu chama kitatengeneza manifesto (ilani), yatakayokuwa kwenye manifesto hiyo ndiyo nitakayotekeleza,”alisema.
Rushwa
Kasisi huyo wa Kanisa la Anglikani pia hakusita kuzungumzia suala la rushwa, ambalo limezungumziwa na takriban kila mwana-CCM aliyechukua fomu za kuwania urais.
Alisema alipokuwa mahakamani alifanya kazi hiyo ya kupambana na rushwa. Alisema kwa kuwa Tume ya Uajiri ya Mahakama ndiyo inayoshughulika na nidhamu kwa watumishi wa taasisi hiyo, alizunguka mikoa 15 akiwa na wajumbe saba kwa lengo la kuhakikisha wanaondoa doa hilo kwenye chombo hicho cha kutoa haki.
“Mimi nikawaambia hakimu akifanya mazongezonge yake huko, usiniletee barua. Namuhamisha kutoka Dodoma ili nimpeleke wapi? Ninyi mna wajibu wenu wa kisheria wa kumchukulia hatua, mnamfungulia mashtaka hapa hapa Dodoma,” alisema.
“Nikijaliwa kuwa rais sheria zipo tutazitekeleza kukabiliana na rushwa.”
Agostino Radhaman ni nani?
Jaji Augustino Ramadhani alizaliwa Desemba 28 mwaka 1945 mjini Unguja, Zanzibar akiwa mtoto wa pili kati ya watoto wa familia ya Mathew Douglas Ramadhani.
Pamoja na kuwa na majina mawili ya dini tofauti, Jaji Ramadhan ni Mkristo na kwa sasa ni kasisi wa Kanisa la Anglikani na ni maarufu kwa upigaji kinanda cha kuongozea nyiumbo za liturugia.
Alisoma Shule ya Msingi Mpwapwa mwaka 1952 -1953 hadi darasa la pili na kuhamia Shule ya Msingi Town mjini Tabora mwaka 1954 – 1956 hadi darasa la tano. Alisoma Shule ya Msingi ya Kaze Hill (sasa Itetemia) hadi darasa la saba mwaka 1958 na kurejea Mpwapwa ambako alimalizia darasa la nane mwaka 1959.
Alisoma Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora (1960 hadi 1965) kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita na baadaye kujiunga katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1966- 1970) akisomea sheria na alipomaliza alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kabla ya kuajiriwa na JWTZ.
Kwa mujibu wa Jaji Ramadhan, kwa kuwa nchi haikuwa na wasomi wa kutosha, Rais wa Zanzibar wakati huo, Aboud Jumbe Mwinyi alimwondoa jeshini Jaji Ramadhan na kumteua kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar mwaka 1978 na baadaye kuwa Jaji Mkuu wa visiwa hivyo mwaka 1978. Alirejeshwa jeshini mwaka 1979 na kupewa jukumu la kuendesha kesi za mahakama ya kijeshi akiwa tayari na cheo cha Luteni Kanali.
Mwaka 1980 alirejeshwa uraiani na kuapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na miaka tisa baadaye aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, kazi ambayo aliifanya kwa miaka minne hadi alipoteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) mwaka 1993. Alikaa NEC hadi Oktoba 2002 alipohamishiwa Zanzibar kufanya kazi kama Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) hadi Oktoba 2007.
Kati ya Novemba 2001 hadi Novemba 2007 aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki. Mwaka 2007 alifikia wadhifa wa juu kabisa kwa wanasheria wa Tanzania, alipoteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania hadi alipostaafu mwaka 2010.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment