
Wachezaji wa timu ya Barcelona wakishangilia baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya jana kwa kuifunga Juventus katika mchezo wa fainali uliofanyika jana kwenye uwanja wa Olympic mjini Berlin,Ujerumani,FC Barcelona walishinda 3-1. Picha na AFP.
Berlin, Ujerumani. Barcelona wametwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya tano baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, katika mchezo wa fainali uliofanyika jana mjini Berlin, Ujerumani.
Mchezo huo ulikuwa na maana kubwa kwa timu zote mbili kwani lilikuwa taji la tatu kwa timu yoyote ambayo ingetwaa taji hilo.
Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Olympic, Barca walikuwa na mchezo mzuri zaidi kutokana na kuanza kwa kasi katika kusaka ushindi.
Miamba hiyo ya Catalan ilianza kuandika bao la kuongoza dakika ya nne wakati Ivan Rakitic akimalizia vizuri pasi safi ya Andres Iniesta.
Bao la Rakitic lilifanikiwa kudumu hadi kumalizika kwa kipindi cha kwanza huku Juve ikionekana kusaka mbinu za kusawazisha kwa kutumia mashambulizi ya kushitukiza.
Kipindi cha pili kilikuwa na faida kwa Juventus, ambao walikuwa wakionekana kusaka bao la kusawazisha na kulazimisha mchezo huo kwenda katika hatua ya dakika 30 za ziada.
Alvaro Morata alifunga bao la kusawazisha kwa kumalizia shuti lililopigwa na Carlos Tevez na kupanguliwa na kipa wa Barca kabla ya mshambuliaji huyo wa Hispania kuumalizia wavuni.
Ilikuwa ni nafuu kubwa kwa vijana wa kocha Massimiliano Allegri, ambao waliamini wamerudi mchezoni baada ya kusawazisha bao hilo.
Lakini hali ilikuwa mbaya baada ya shambulizi la kushitukiza lililofanywa na Barca. Luis Suarez alimalizia kirahisi wavuni shuti lililopanguliwa na kipa wa Juve, Gianluigi Buffon lililopigwa na Lionel Messi na kuzaa bao la pili.
Bao hilo liliwaaamsha Juve, ambao waliona inawezekana kwa kusawazisha na kuamua kupanda wengi kwa ajili ya kushambulia.
Lilikuwa kosa kubwa kwao kwaniBarca walitumia vizuri shambulizi jingine la kusawazisha lililomaliza mpira baada ya Neymar kufunga bao la tatu dakika ya mwisho ya nyongeza na kuumaliza mchezo huo.
Kwa matokeo hayo, Barca sasa wamemaliza msimu wakiwa na mataji matatu, ya Ligi Kuu Hispania, Kombe la Mfalme na la Ligi ya Mabingwa Ulaya.MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment