BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAKONGORO NYERERE AANZA NA NUKSI MBIO ZA URAIS, MSAFARA WAKE WAPATA AJALI WAKATI WA KUKUSANYA SAINI KIGOMA.

 
Gari ilikuwa imebeba wasaidizi wa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Makongoro Nyerere likiwa limeanguka wilayani Kasulu, Kigoma jana wakati likiwa kwenye msafara kwa ajili ya kusaka wadhamini. Picha na Blog ya Michuzi

Kigoma. Msafara wa kada wa CCM, Makongoro Nyerere jana ulipata ajali baada ya gari moja kupinduka na kusababisha watu watano kujeruhiwa katika eneo la Mwilamvya, nje kidogo ya mji wa Kasulu mkoani Kigoma.


Hata hivyo, pamoja na ajali hiyo, mfasara huo uliendelea na kufika Kigoma Mjini, kwa ajili ya kukusanya saini za wanachama wa CCM waliojitokeza kumdhamini.


Akitoa taarifa za ajali hiyo, kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui alisema ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Land Cruiser lililokuwa linaendeshwa na Julius Kambarage Nyerere ambalo lilipinduka saa 4:30 lilipofika eneo la Mwilamvya na kujeruhi watu watano.


Mtui aliwataja majeruhi kuwa ni dereva wa gari hilo, Julius Nyerere, Evance Magige, Fikiri Malumba, Ally Tesha na mtu mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Musiba na kwamba hali zao zinaendelea vizuri, baada ya kutibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kasulu.


“Chanzo cha ajali hiyo ni vumbi iliyotapakaa barabarani ikasababisha dereva ashindwe kuona mbele na matokeo yake gari likapinduka. Msafara huo ulikuwa na magari matatu baada ya gari la mbele kupita likifuatiwa na lililombeba Makongoro Nyerere, ndipo hilo lililokuwa nyuma likaanguka kwa vile lilikuwa karibu sana na gari la mbele yake,” alisema Kamanda Mtui.


Dereva wa gari hilo ni mtoto wa Makongoro hivyo ajali hiyo ilisababisha ratiba ya kujaza fomu za wadhamini Kigoma Mjini, kuchelewa kwa zaidi ya saa tano.


Akiwa Mjini Kigoma, Makongoro aliwaambia wanachama wa CCM waliomdhamini kuwa mara tu ajali ilipotokea baadhi ya watu walitaka kupora mkoba uliokuwa na fomu za wadhamini wakidhani ni fedha zilizojazwa humo, lakini polisi waliokuwa wamefika muda huo walifanikiwa kuzuia uhalifu huo.


“Inawezekana hili zoezi tunalofanya hapa lisingekuwepo leo kwa sababu gari lilipoanguka lilianza kutoa moshi mkubwa, ikabidi kijana wangu mmoja arudi ndani ya gari kuchukua mkoba wenye fomu za wadhamini kwa vile ulisahaulika ndani, ndipo baadhi ya watu wakadhani umejaa fedha. Lakini nawashukuru polisi waliofika hapo walidhibiti jaribio hilo la wizi. Vinginevyo kila kitu kingekwama,” alisema Nyerere.


Makongoro aliwataka wana-CCM kumchagua yeye kwa vile ni mwadilifu na atakomesha tatizo la rushwa ambalo limekuwa likistawi kila siku nchini na kusababisha watu kukosa haki zao za msingi.


“Kuna wanachama wa CCM wasiozidi 20 wamejikita katika ulaji rushwa uliotopea na matokeo yeke kila mwana-CCM leo hii anachukuliwa kuwa ni mwizi na fisadi, lakini hii yote inasababishwa na mwenyekiti wetu wa CCM (Jakaya Kikwete) kuwa mpole kupindukia, jambo linalochukuliwa na mafisadi kama kuwaogopa na baadhi yao ndiyo hawa tunaowaona wapo mbele kutafuta nafasi ya kuteuliwa na CCM kugombea urais, wakataeni wala rushwa na mafisadi,” alisema Nyerere.


Baadhi ya mikoa ambayo anapita kukusanya wadhamini ni Dodoma, Singida, Shinyanga, Tabora, Geita na Kigoma na leo hii atakusanya wadhamini katika mikoa ya Katavi na Rukwa.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: