BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAFUTA YA PETROL SIYO ANASA, KWANINI MWANANCHI ANABEBESHWA MZIGO MZITO ?.

 

Katika hotuba ya bajeti ya mwaka 2015/16 Serikali ilipendekeza kurekebisha Sheria ya Mafuta ya Petroli, sura ya 392 kwa kuongeza tozo za mafuta ya dizeli, petroli na mafuta ya taa.

Serikali ilipendekeza kuongeza tozo ya mafuta ya dizeli kutoka Sh50 hadi Sh100 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh50 kwa lita. Iliongeza pia, tozo kwa mafuta ya petroli kutoka Sh50 hadi Sh100 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh50 kwa lita wakati mafuta ya taa kutoka Sh50 kwa lita hadi Sh150 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh100 kwa lita. 

Lengo kuu la kuongeza tozo kubwa kwenye mafuta ya taa, Serikali ilieleza ni kuondoa uwezekano wa wafanyabiashara kuchakachua, yaani kuchanganya na dizeli au petroli.


Fedha itakayopatikna itapelekwa kwenye mfuko wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA).


Isitoshe Serikali ikapendekeza Waziri wa Fedha apewe mamlaka ya kusamehe tozo ya mafuta ya petroli kwenye miradi inayotekelezwa kwa misaada ya wafadhili na yenye mikataba isiyohusisha utozaji wa tozo hizo.


Kama hiyo haitoshi, Serikali ikapendekeza kuongeza Ushuru wa mafuta na dizeli itaongezeka kutoka Sh263 hadi Sh313 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh50 kwa lita.


Petroli kutoka Sh263 hadi Sh313 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh50 kwa lita. Hatua ya kuongeza ushuru wa barabara ikaonekana itaongeza mapato ya Serikali ambayo yatapelekwa kwenye Mfuko wa Rea.


Uamuzi huo wa Serikali unatarajia kuleta matokeo ya aina mbalimbali kwa jamii. Kwanza kwa mtazamo wa haraka, ongezeko la bei za mafuta, dizeli na mafuta ya taa kwenye bajeti ya mwaka 2015/16 litasababisha kuongezeka kwa gharama kwa wateja wa bidhaa hizi. Hizi ni bidhaa zenye unyeti wa kipekee na ambazo ni muhimu kwa kila mwanadamu, kwani zinaathiri kila sekta na maisha kwa namna moja au nyingine.


Ongezeko la gharama za bidhaa hizi litasababisha ongezeko la gharama za bidhaa nyingine kama chakula na huduma kutokana na kuongezeka gharama za usafirishaji.


Kwa namna yoyote ile zinapoongezeka gharama za usafiri, gharama za maisha kupanda na kusababisha watu wengi kupata maisha magumu.


Ni haya maisha magumu pia yatasababisha nchi ishindwe kufikia malengo yake ya kupambana na umaskini kama yalivyoainishwa kwenye malengo ya milenia na kugusa nyanja zote, ikiwamo elimu, afya, mazingira na jinsia. Hali hii itawaathiri pia wazalishaji kama vile wakulima, ambao takwimu zinaonyesha ni asilimia 80 ya Watanzania na wengi wao wanaishi vijijini, ambako huduma nyingi bado hazijafika.


Mfano mzuri ni wakulima wadogowadogo vijijini watalazimika kuuza bidhaa zao kwa bei ndogo zaidi ili kufidia gharama za wachukuzi na wafanyabiashara wanaosafirisha mazao hayo kuja mijini na sehemu mbalimbali. Nchi karibu zote Afrika kwenye ukanda wetu wana malengo ya kupambana na umaskini kwa raia wake.


Sasa hapa tutajiuliza, bajeti hii ni kwa ajili ya kumuondoa Mtanzania kwenye umaskini au ni kuendelea kumwongezea mzigo aendelee kuathirika zaidi?


Kwa hali hii sioni kama mipango ya kuondoa umaskini nchini itatimia. Kuondoa umaskini itakuwa ni ngumu kutimia kwa sababu ni sawa na mtu anasafisha eneo na kisha kuja kulichafua tena na tena.


Naishauri Serikali iwe na mpango wa kuweka ruzuku kwa bidhaa hizi kwani siyo bidhaa za anasa bali ni za muhimu kwa maisha na ustawi wa jamii na ni za lazima.

Deogratius Kilawe ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Excel na mshauri wa mambo ya biashara. (0717109362)
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: