PROF LIPUMBA AWALIPUA WAGOMBEA URAIS NDANI YA CCM, ASHANGAA KUONA WANAOSTAHILI KUKAA MAHABUSU NDIYO KWANZA WANAPEWA NAFASI YA KUGOMBEA URAIS.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amechukua fomu ya kugombea urais kupitia chama hicho na kuahidi kupambana na rushwa huku akishangaa kuwapo watuhumiwa wa ufisadi waliotakiwa kuwa mahabusu lakini wakichukua fomu za kuwania nafasi hiyo kupitia CCM.
Profesa Lipumba alisema iwapo atapatiwa ridhaa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kupeperusha bendera ya umoja huo atahakikisha anaunda Katiba yenye maoni ya wananchi na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuwaunganisha Watanzania dhidi ya ufisadi.
Mwanasiasa huyo mkongwe katika upinzani aliwaambia wafuasi wa CUF waliomsindikiza kuchukua fomu hiyo jijini hapa jana kuwa ameamua kuwania kiti hicho kwa mara ya tano kwa kuwa kati ya viongozi wa juu wa Ukawa anaamini ana sifa, uwezo, uadilifu, uwazi, uwajibikaji wa kuwaunganisha Watanzania ili waondokane na rushwa na ufisadi uliokithiri nchini.
Profesa Lipumba aliyekabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa CUF Wilaya ya Kinondoni, Mohamed Mkandu saa 6.55 mchana, alitaja vipaumbele vyake kuwa ni kujenga misingi ya kuhakikisha watoto wanapata fursa sawa ya maendeleo, ajira, afya, kulinda rasilimali za umma na kupambana na ufisadi.
Profesa Lipumba aliyeanza hotuba yake ya takriban dakika 45 kwa kutoa wasifu wa usomi na kazi mbalimbali za kiuchumi alizozifanya kwa takriban miaka 40, alisema anafahamu bayana matatizo mengi ya Watanzania kwa kuwa amezaliwa na kukulia kijijini.
Alisema matatizo hayo yamesababishwa na “siasa mbovu za chama cha mapinduzi” ukiwamo ufisadi, hivyo iwapo atapatiwa ridhaa ya kuwania kiti hicho cha juu, atakuwa na kazi kubwa ya kuleta uongozi makini utakaohakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa maendeleo ya watu wote.
Alisema iwapo atachaguliwa kuwa rais, hatakuwa na msalie mtume na mafisadi na wote wanaohusika watawajibika kwa mujibu wa sheria na taratibu.
“Inatisha sana kuona mafisadi wakubwa, wala rushwa wakubwa badala ya kuwa ndani ya jela, wanachukua fomu za urais. Tunahitaji kwa kufuata taratibu na haki, mafisadi hao watumikie vifungo na mali zilirudishwe kwa umma walikofisadi,” alisema Profesa Lipumba huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Iwapo atapatiwa nafasi ya urais, alisema katika utawala wake atahakikisha watoto nchini wanapatiwa fursa sawa ya maendeleo kwa kutoa huduma bora afya, lishe na elimu.
Alisema suala la ukuaji imara kwa watoto halijapatiwa kipaumbele na kusababisha udumavu unaowanyima uwezo mkubwa wa kufikiri pindi wanapokuwa wakubwa.
Kufumua Katiba inayopendezwa
Mwanasiasa huyo alisema anachukua fomu nchi ikiwa njia panda baada ya Katiba Inayopendekezwa kuacha masuala ya msingi ya uadilifu na uwajibikaji na kusababisha wachache kujinufaisha kwa rushwa.
Akielezea kwa kina juu ya Katiba Mpya, Profesa Lipumba alisema Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba iliweka misingi ya maadili ya nchi na kubainisha kuwa chanzo kikubwa cha ufisadi ni zawadi ndogondogo lakini viliondolewa na wanasiasa wasiopenda maadili.
“Mafisadi walihakikisha wanaving’oa vifungu vya maadili na zawadi ili wakipatiwa zawadi waende kununua mboga. Tunahitaji kazi kubwa kuyarudisha maoni yalitolewa na wananchi tuweze kuyalinda kwa pamoja na kuyaheshimu ili uwazi, uwajibikaji na uadilifu ziwe ni Tunu za Taifa.
“Uzuri wa katiba inayotokana na wananchi unaweza kuitumia kuizaa Tanzania mpya kwa kuwaambia hii ni katiba yenu muilinde na kuhakikisha viongozi wanawajibika,” alisema.
Serikali ya mseto
Alisema Ukawa ilianza bungeni kupigania maoni ya wananchi kwa kujumuisha vikundi vingine vya kijamii hivyo akiwa rais ataunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili iwaunganishe Watanzania kupambana na ufisadi.
Profesa Lipumba pia alisema atapambana na tatizo la ajira kwa kuhakikisha bandari zote nchini zinafanya kazi kwa ufanisi ili kuzalisha kazi nyingi iwezekanavyo kukidhi mahitaji ya vijana.
Katika kuimarisha sekta ya afya, alisema atahakikisha anapambana na magonjwa yanayoweza kuzuilika kirahisi kama malaria na kifua kikuu na kuwawezesha Watanzania kuwa na bima za afya.
Pia, alisema kutakuwa na mpango maalumu wa kuwaenzi wazee ili waweze kuishi vizuri tofauti na sasa huku akibainisha mipango yote hiyo inatekelezeka lakini sasa imeshindikana kutokana na ufisadi wa kupindukia.
Profesa Lipumba alieleza dhamira yake ya kupitia mikataba yote ya rasilimali nchini hasa iliyopo katika sekta ya madini ili ziweze kuwanufaisha wananchi wote.
“Ili tufanikishe hayo ni lazima tuweke motisha kwa wananchi kulinda rasilimali zao na ni lazima tuweke uwazi kwa viongozi wa Serikali,” alisema.
Alisema iwapo Ukawa watakubaliana asimame mgombea mwingine tofauti na yeye yupo radhi kumwachia na atahakikisha anampigia kampeni kwa nguvu zote ili ashinde katika Uchaguzi Mkuu hapo Oktoba.
Familia yake
Mtaalamu huyo wa uchumi pia alizungumzia maisha yake ya ndoa kwa kueleza kuwa mke wake huwa hajihusishi na siasa kwa kuwa ni mfanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa na taratibu zao haziwaruhusu kufanya hivyo.
“Watu huwa wananiuliza nimeoa? Leo nawaambia nimeoa na naruhusiwa kuwa nao hadi wanne, ila ninaye mmoja tu. Watu wanapaswa kufahamu mimi ni mgombea wa urais siyo familia inagombea urais…
kuna watu wakipata uenyekiti wa chama, basi mke wake kapata tiketi ya viti maalumu, sisi kwetu hayapo hayo, mtu apatiwe nafasi kulingana na uwezo wake,” alisema Profesa Lipumba huku akikoleza kwa salamu ya chama, “CCM kwishaa, kwishaa, kwisha kabisa, nyang’anyang’a, ndembendembe, mlalo wa chali, kifo cha mende na akiitikiwa na wafuasi wa chama hicho huku wakimshangilia.
Alisema akiingia madarakani anataka kuwa rais wa kwanza wa Tanzania kupata Tuzo ya Mo Ibrahim kwa kutenda haki, uwajibikaji na usawa kwa wananchi.
Maalim Seif
Awali, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliwauliza wafuasi wa chama hicho kuwa ni nani kati ya waliotangaza nia kuwania urais kupitia CCM ambaye ni msafi.
Wafuasi wa chama hicho walimjibu kwa sauti ya pamoja, hakunaaa!
Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, aliyetambulishwa juzi Pemba kuwania urais wa visiwa hivyo, alisema muda wa mabadiliko ni sasa na Watanzania wamechoshwa na utawala kandamizi wa CCM.
“Imebaki miezi mitatu, hakuna kulala tumechoshwa na utawala wa mafisadi unaokandamiza na kuonea watu,” alisema.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment