MBIO za kusaka urais kwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimezidi kushika kasi baada ya mtoto wa tano wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Charles Makongoro Nyerere kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Wakati Makongoro akichukua uamuzi huo kwa mara ya kwanza katika historia ya familia ya Mwalimu Nyerere, mkoani Mbeya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya naye ameingia kwenye mbio hizo.
MAKONGORO
Akitangaza nia yake katika eneo la Mwitongo kijijini Butiama Juni 02/ 2015, Makongoro aliwashambulia makada wenzake ndani ya CCM ambao wanaongoza makundi ya kuwania urais kwa kuwaita ni ‘vibaka’ wanaokivuruga chama hicho kwa maslahi yao binafsi.
Akitoa mfano kwa baadhi ya makada wanaoongoza makundi ndani ya chama hicho, Makongoro aliwataja kwa majina kuwa ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Naibu Waziri wa Fedha,Mwigulu Nchemba na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira.
Alisema makada hao kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia fedha nyingi kuendesha makundi ya urais na akahoji sababu za kutafuta cheo hicho cha juu kwa fedha.
CCM irudishwe kwa wazalendo kwa sababu vibaka wamekuwa na mlengo mbaya wa kukiendeleza chama hicho, alisema.
Alisema ndani ya chama hicho kumekuwa maradhi ya rushwa ambayo yameiambukiza nchi nzima.
Makongoro alisema yeye ni mzalendo wa kweli na anataka kuirudisha nchi katika misingi ya uadilifu endapo CCM itampa ridhaa ya kupeperusha bendera katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Alisema ndani ya chama hicho kumekuibuka genge la watu wachache ambao utajiri wao ni wa shaka na umejijenga kwa fedha chafu.
“Ndani ya chama tawala wamekuwapo ‘vibaka’ wachache… unajua kibaka ni kibaka tu hata kama kapewa gari la Serikali lina bendera ya taifa mbele atabaki kuwa kibaka tu.
“Wananijua vizuri huwa siwaonei haya kuwaambia ukweli, hawa ndiyo wanaotuvurugia chama na hawamheshimu Mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya Kikwete,” alisema Makongoro.
Katika hotuba yake ambayo alitumia saa mbili, Makongoro alijikita kuzungumzia madhara yanayotokana na rushwa ndani ya CCM.
Alisema baadhi ya makada wanaotumia rushwa wamezalisha makundi na mipasuko isiyo ya lazima huku akisisitiza kuwa anachukia kuwapo makundi ndani ya chama hicho.
Kwa mujibu wa Makongoro, hali hiyo imechochea badhi ya viongozi wa CCM katika ngazi mbalimbali wakiwamo wenyeviti wa mikoa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho kuishi kama mifugo.
Alisema hali hiyo imesababisha baadhi ya viongozi hao kuishi maisha ya kusukumwa kwa upepo wa makundi yanayomilikiwa na watoa fedha.
“Vibaka waturudishie CCM yetu, watambue wao ni wachache na sisi wazalendo ni wengi, hawatushindi na fedha zao na kitaeleweka tu.
“Leo hii viongozi wetu wa CCM wamekuwa ni watu wa kuendeshwa na vibaka hawa wanahongwa fedha ovyo…wao wana mifugo yao ndani ya NEC basi mimi sijafuga hata kuku, nasema kitaweleweka,” alisema Makongoro.
Alisema yeye hawezi kufanya hivyo kwa sababu rasimu ya ilani ya chama hicho bado haijapitishwa na chama, hofu yake ni kwamba anaweza kutoa ahadi na zikawa kinyuume na ilani ya chama chake.
“Nimewasikia wanajinadi,nawashangaa sana, najiuliza kwani wao ni akina nani watoe ahadi kabla ya ilani ya chama? Ikitokea ahadi yako ikaenda kinyume na ilani si ndiyo mwanzo wa kuwa na rais muongo…sitaki kuwa rais muongo nitaheshimu chama changu kwa kila mchakato na maelekezo,” alisema Makongoro.
Aliwaasa Watanzania wawaogope watu wanaoonekana kuwa na haraka ya kukimbilia kutawala nchi.
“Ukiona watu kazi inatangazwa ifanywe kwa utaratibu wake na mtu aliyeiomba kazi hiyo anakiuka taratibu, muogopeni sana huyo hafai kukukuongoza maana hata akikuongoza ataendelea kukiuka taratibu ili ajinufaishe,” alisema Makongoro.
Wanawake wananipenda
Makongoro alisema anakerwa na siasa chafu dhidi yake zinazoenezwa na baadhi ya wanasiasa wenzake ndani ya CCM.
Alizitaja siasa hizo kuwa ni tuhuma za kulaaniwa na baba yake, ulevi na mtu anayependa wanawake.
Akijibu tuhuma hizo, Makongoro alihoji umati uliomiminika kumsikiliza kwamba, “jamani naonekana nimelaaniwa? Naelekea kuokota makopo? Jamani mnanionaje, naonekana mlevi? na umati ulikataa kwa kusema, “hapana”.
“Eti wanasema Makongoro anapenda wanawake sasa wanataka nipende wanaume? Wanawake wananipenda na mimi nawapenda, hizi siasa chafu wanazonituhumu hazinisumbuilangu ni moja tu vibaka rudisheni nchi yetu,” alisema.
MSIKILIZE MAKONGORO NYERERE NA RADHA YA SAUTI YA MWL JULIUS NYERERE VIZURI KATIKA HII VIDEO.
0 comments:
Post a Comment