BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SPIKA WA BUNGE AWAPIGA MKWARA NA KUAGIZA VYAMA VYA SIASA KUWAAMURU WABUNGE WAO, WAGOMBEA URAIS NA MAWAZIRI KUREJEA BUNGENI BAADA YA UTOROKA VIKAO VYA BAJETI DODOMA.

https://hivisasa.co.tz/wp-content/uploads/2014/11/ANNA-MAKINDA.jpg



Spika wa Bunge Anne Makinda.
 
WAKATI wasaka urais wa CCM wakizunguka nchi nzima kutafuta wadhamini ili watimize masharti ya kutimiza ndoto zao, vita ya wasaka majimbo imepamba moto kiasi cha kukimbiza wabunge na mawaziri karibu wote katika vikao vya Bunge vinavyoendelea Dodoma.


Uchunguzi wa gazeti hili wiki hii imebaini kuwa, baadhi ya wasaka urais katika kutafuta watu wa kuwaunga mkono, wameamua kuunga mkono baadhi ya wasaka majimbo, ambao wamekuwa wakijijenga kwa lengo la kuangusha wabunge waliopo kazini.

Hali hiyo imesababisha wabunge walazimike kukimbia vikao muhimu vya Bunge la Bajeti na kurejea kutetea majimbo yao, hatua iliyomlazimu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, kuagiza vyama vyote vya siasa kurejesha wabunge wao bungeni ifikapo kesho.

Akizungumza bungeni juzi, Spika Makinda alitaka wabunge hao warejeshwe na vyama vyao, ili wasikilize majibu ya Serikali kuhusu hoja na maswali waliyouliza wakati wa kuchangia mjadala wa Bajeti ya Serikali unaoendelea.

Nguvu za wagombea Katika uchunguzi huo, gazeti hili lilibaini katika baadhi ya majimbo, wabunge wa sasa wanakabiliwa na ushindani mkali wa watangaza nia za ubunge, ambao wanaungwa mkono na makundi ya wasaka urais wa CCM wenye nguvu.

Katika wiki mbili hizi, waandishi wetu walishuhudia watangaza nia hao wanaoungwa mkono na makundi ya wasaka urais, wakihangaika kuandaa mikutano ya ujio wa wagombea urais, kuwasindikiza na kushiriki kuwatafutia wadhamini.

Mbali na watangaza nia majimboni wanaoungwa mkono na makundi ya wasaka urais, gazeti hili limebaini pia kuwa baadhi ya watangaza nia ni walioshindwa katika kura za maoni za mwaka 2010, wabunge wa zamani wanaotaka kurejea bungeni, wenyeviti wa halmashauri na madiwani.

Pia wapo makamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM wa mikoa na wilaya, wanasheria, wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM Taifa, wafanyabiashara wakubwa, watendaji wa nafasi za juu serikalini, wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa.

Arusha utitiri
Katika baadhi ya majimbo ya Mkoa wa Arusha kwa kuanzia na Jimbo la Arusha Mjini, linalowakilishwa na Godbless Lema (Chadema), tayari wanaowania kupambana na mbunge huyo, wanazidi 17 kutoka ndani ya CCM pekee. Wanaotajwa kuwania nafasi hiyo na kumweka Lema kiti moto ni pamoja na mfanyabiashara mmoja anayemiliki Kampuni ya Nafaka, kigogo wa UVCCM Mkoa wa Arusha na mmiliki mmoja wa kampuni maarufu ya utalii.

Pia wapo wafanyabiashara wawili wa madini, Diwani wa Kata moja ya Jimbo la Simanjiro, Mwanasheria na kigogo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika mikoa ya Kaskazini. Katika jimbo la Arumeru Magharibi, aliko Goodluck ole Medeye (CCM), anakabiliwa na ushindani wa mfanyabiashara mmoja wa madini, ambaye pia anatajwa kuungwa mkono na kundi moja lenye mashabiki wengi la msaka urais.

Mbali na mfanyabiashara huyo, Medeye pia anakabiliwa na ushindani wa ndani ya CCM kutoka kwa Mwenyekiti wa UVCCM wa mkoa mmoja wa Kanda ya Kaskazini na Mkuu wa Wilaya wa miaka mingi, ambaye kwa sasa ni mstaafu. Katika Jimbo la Arumeru Mashariki, aliko Joshua Nassari (Chadema), naye anakabiliwa na ushindani wenye nguvu kutoka kwa watangaza nia kadhaa wa CCM, akiwemo mmoja wa wafanyabiashara wakubwa wa Bima nchini.

Mbali na mfanyabiashara huyo, pia yupo kigogo wa UVCCM katika jimbo hilo na mmoja wa wafanyakazi katika sekta ya benki, ambaye anaungwa mkono na kundi moja la msaka urais. Katika Jimbo la Karatu, aliko Mchungaji Israel Natse, naye anakabiliwa na ushindani kutoka kwa Balozi mmoja anayewakilisha Tanzania katika moja ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Uchunguzi Tabora
Katika Mkoa wa Tabora, kwenye Jimbo la Tabora Mjini, aliko Aden Rage (CCM) anakabiliwa na ushindani kutoka kwa mwanasheria ambaye pia ni mfanyabiashara mkoani humo, kigogo mmoja katika kampuni moja ya ulinzi na kigogo mwingine kutoka kampuni ya usambazaji mafuta nchini.

Rage pia anakabiliwa na ushindani wa mbunge mmoja wa zamani, Meya katika moja ya manispaa za hapa nchini na mfanyabiashara mmoja ambaye pia ni mjumbe katika vikao vya juu vya CCM, ambaye pia anaungwa mkono na makundi kama mawili yenye nguvu ya wasaka urais.

Katika Jimbo la Nzega, Mbunge wa sasa Hamisi Kigwangala (CCM), ambaye amechukua fomu ya kugombea urais na kuweka wazi akikosa nafasi hiyo, atarejea jimboni, naye anakabiliwa na ushindani mkubwa. Mmoja wa washindani wake ni kigogo katika vyombo vya habari na anaungwa mkono na kundi moja la wasaka urais.

Pia kigogo mwingine katika sekta ya madini na mwandishi mmoja wa habari. Kwa upande wa Jimbo la Urambo Magharibi, anakotoka Profesa Juma Kapuya (CCM), gazeti hili limebaini kuwa anakabiliwa na ushindani kutoka kwa mmoja wa wafanyabiashara wa mkoani Dar es Salaam na mhadhiri kutoka katika moja ya vyuo vikuu, ambaye ni Profesa pia.

Katika jimbo la Urambo Mashariki anakotoka Samuel Sitta, ambaye ameshatangaza kung’atuka ubunge na kuchukua fomu ya kugombea urais, ushindani pia ni mkali kati ya wanaowania. Miongoni mwao yupo mbunge mmoja wa viti maalumu, anayetajwa kuwa na nguvu lakini akikabiliwa na ushindani mkubwa wa diwani ambaye pia ni mfanyabiashara na kigogo mmoja kutoka katika kampuni moja kubwa ya simu za viganjani.

Katika Jimbo la Bukene, linalowakilishwa na Selemani Zedi (CCM), yeye anakabiliwa na ushindani kutoka kwa kigogo mmoja katika moja ya asasi za kiraia, ambaye pia ni mfanyabiashara na mbunge wa zamani, ambaye ameonesha nia ya kutaka kurejea Dodoma.

Katika Jimbo la Igunga, linaloongozwa na Dk Peter Kafumu, yeye anakabiliwa na ushindani wa wazi kutoka kwa kigogo mmoja wa UVCCM, ambaye pia anaungwa mkono na kundi moja la urais na Diwani ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri moja katika mkoa huo.

Jimboni Sikonge, alipo Said Nkumba (CCM), anapambana na mbunge wa zamani kutoka moja ya miji ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, mwenyekiti mmoja wa halmashauri ambaye pia anaungwa mkono na kundi moja la msaka urais na mhandisi wa maji kutoka mikoa inayopakana na Ziwa Tanganyika.

Mbeya utitiri

Moja ya majimbo yanayowaniwa na utitiri wa watangaza nia ni Mbeya Mjini, anakotoka Joseph Mbilinyi maarufu Sugu (Chadema). Mbunge huyo anakabiliwa na ushindani wa karibu watangaza nia 30. Gazeti hili katika uchunguzi wa baadhi ya watangaza nia hao, limebaini yupo Mwandishi wa Habari kutoka moja ya magazeti kongwe ya Kiswahili hapa nchini, ambaye inadaiwa anaungwa mkono na makundi karibu matatu yenye nguvu ya wasaka urais.

Pia yupo mbunge mmoja wa Viti Maalumu wa sasa, mfanyabiashara mkubwa mwenye mabasi na wafanyabiashara wengine wawili, ambao mmoja anaungwa mkono na kundi moja la msaka urais. 


Katika moja ya vituko vya wasaka jimbo hao, wapo wengine kama watatu wanaungwa mkono na msaka urais mmoja, akiwemo mfanyabiashara mmoja wa Tunduma, anayejishughulisha na masuala ya fedha, kigogo mmoja kutoka Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Dar es Salaam, Kigogo wa zamani wa Muungano wa Klabu za Waandishi Tanzania (UTPC) na mmoja wa wanasheria maarufu, ambaye alisikika sana alipokuwa Chadema lakini sasa kahamia CCM.

Katika Jimbo la Rungwe Mashariki, anakotoka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, ambaye ametangaza kung’atuka kwa heshima ya kupita bila kupingwa kwa muda mrefu na kuamua kuchukua fomu ya kuwania urais, ushindani umeibuka.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa ushindani mkubwa utakuwa katika Jimbo tarajiwa la Busikelo, ambalo linatarajiwa kupatikana baada ya kugawanywa kwa jimbo la sasa. Katika jimbo hilo tarajiwa, amejitokeza Ofisa Elimu katika moja ya mikoa ya Kanda ya Kati, kigogo wa Benki Kuu (BoT), kutoka moja ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na mfanyabiashara mmoja kutoka Tunduma.

Shinyanga utitiri
Katika Mkoa wa Shinyanga, Jimbo la Kahama Mjini, anakotoka Mbunge machachari, James Lembeli (CCM), linalotarajiwa kugawanywa na kupata Jimbo la Ushetu, nalo lina utitiri wa wasaka jimbo, ambao ushindani utakuwa mbaya kama halitagawanywa.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa katika jimbo hilo, wako wasaka jimbo zaidi ya 30, akiwemo kigogo kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kigogo kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na Mwanasheria wa Kujitegemea kutoka jijini Dar es Salaam.

Iringa hapatoshi
Katika Jimbo la Iringa Mjini, anakotoka Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), anakabiliwa na ushindani kutoka kwa Mwenyekiti mmoja wa CCM Mkoa. Mbali na huyo yupo mwandishi mmoja wa habari kutoka gazeti kongwe la Kiswahili la chama, kigogo wa UVCCM katika mkoa mmoja wa Nyanda za Juu Kusini, Mjumbe mmoja wa vikao vya juu vya CCM ambaye pia ni mfanyabiashara na Daktari Bingwa wa wanawake katika moja ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Pia yupo kigogo mwingine wa UVCCM katika Kanda hiyo ya Nyanda za Juu Kusini, Mhadhiri wa zamani ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), na mwimbaji mmoja wa nyimbo za injili ambaye amewahi kushika nafasi za juu za CCM katika mikoa hiyo ya Nyanda za Juu Kusini.

Hata hivyo, kada mmoja wa CCM ambaye ni kigogo kwenye kampuni maarufu sana katika mikao ya Nyanda za Juu Kusini, anatajwa kuwa na uwezo wa kushinda kama akichukua fomu, ingawa mara zote alipoulizwa, amekuwa akikataa kukubali au kukanusha kuwa katika mbio hizo.

Mwingine anayetajwa kuwania jimbo hilo ni kigogo katika klabu maarufu ya mpira ya Dar es Salaam, Mkuu mmoja wa Wilaya, anayetajwa pia kuwa na nguvu kubwa ya ushindi na mhadhiri mwingine kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Katika Jimbo la Ismani, anakotoka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, ambaye ametajwa bungeni kuwa jembe la CCM, anakabiliwa na ushindani kutoka kwa kigogo moja wa Idara ya Misitu, Mhandisi wa Maji katika moja ya mikoa inayopakana na Ziwa Victoria na Mkuu mmoja wa Wilaya.

Katika Jimbo la Kilolo, anakotoka Profesa Peter Msolla (CCM), anakabiliwa na ushindani kutoka kwa kigogo mmoja wa mtandao wa kutoa fedha katika mabenki, Mkuu wa Wilaya, Katibu wa CCM katika wilaya za Nyanda za Juu Kusini.

Katika Jimbo la Kalenga, anakotoka Godfrey Mgimwa (CCM), anakabiliwa na ushindani kutoka kwa kigogo wa kampuni maarufu ya simu za viganjani na mmoja wa wakuu wa mikoa maarufu nchini.

Kwenye Jimbo la Mufindi Kaskazini, anakotoka Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa, anakabiliwa na ushindani kutoka kwa Ofisa mmoja kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kigogo kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mwanza
Katika Mkoa wa Mwanza, changamoto kubwa iko katika Jimbo la Nyamagana, anakotoka Ezekiah Wenje (Chadema), yeye anakabiliwa na ushindani kutoka mmoja wa mameya wa miji maarufu hapa nchini.

Wengine wanaonyemelea jimbo hilo ni Mbunge na Waziri wa zamani, Mwenyekiti wa wilaya wa CCM katika moja ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na Bosi wa Shirikisho la Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), ambaye ni mchumi na mfanyabiashara.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: