WAGOMBEA WANAOJINADI URAIS NDANI YA CCM KUMBE WANATWANGA MAJI KATIKA KINU NA KUPOTEZA MUDA WAO TU.
Dodoma/Dar. Wakati makada wanaotangaza nia na kuchukua fomu kugombea urais kupitia CCM wakiendelea kujinadi kwa kutaja sifa mbalimbali za rais ajaye, chama hicho kimesema hayo yote ni kazi bure kwa kuwa chenyewe kina vigezo vyake 13 ambavyo kitavitumia kumpata mgombea wake wa nafasi hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana huku wasomi na wachambuzi wa siasa wakisema sifa hizo na ahadi wanazotoa wagombea hao si rahisi kutekelezeka ndani ya mfumo uliopo wa chama hicho.
Mangula, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ndogo wa maadili, alisema: “Kila mtu anatoa sifa zake anazozipenda. Ohh nataka mgombea ajaye awe hivi… lakini chama chetu kimetaja sifa 13 za mgombea urais. Mtu anayetaka kuwa mgombea kupitia CCM lazima awe na vigezo hivyo.
Mangula alisema kifungu cha tano cha kanuni za uteuzi wa wagombea wa CCM, kinaipa jukumu Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC) kuzingatia mambo kadhaa muhimu wakati wa uteuzi wa mgombea katika nafasi ya urais.
Aliyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni uzito wa nafasi hiyo, haja ya kulinda na kuendeleza mshikamano miongoni mwa wanaCCM, haja ya kupanua demokrasia ya ndani katika kuwapata wagombea na hali halisi ya nyendo za ushindani wa kisiasa nchini.
Vigezo 13 vya urais
Mangula alitaja vigezo vya mgombea urais CCM kuwa ni uwezo mkubwa wa kuongoza nchi kwa kutumia uzoefu katika uongozi wa Serikali, umma au taasisi, awe mwadilifu, mwenye hekima na busara.
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi.
“Unapimaje hekima?” aliuliza Mangula na kujibu mwenyewe: “Unapima kwa kuangalia yale mliyokubaliana kama ameyatekeleza kama mlivyokubaliana.”
Alivitaja vigezo vingine kuwa ni elimu ya chuo kikuu au inayolingana na hiyo, upeo mkubwa wa kudumisha na kuendeleza Muungano, umoja, utulivu na mshikamano wa kitaifa, wepesi wa kuona mbali, asiyeyumbishwa na mwenye uwezo wa kuona mbali kuhusu masuala nyeti na muhimu kwa Taifa kwa wakati unaofaa.
Vigezo vingine ni upeo mkubwa na usiotiliwa shaka kuhusu masuala ya kimataifa ili aweze kuwa kiungo imara kati ya nchi na dunia yote, asiwe mwenye hulka ya udikteta au ufashisti, bali awe mtu mwenye kulinda Katiba, utawala bora, kanuni na taratibu za nchi.
Mangula alisema mgombea urais wa CCM anapaswa kuwa mtetezi wa wanyonge wa haki za binadamu na mzingatiaji wa maendeleo ya watu wote. Pia asiwe na tamaa ya kujitafutia umaarufu wa mtu binafsi. Pia mgombea lazima awe mstari wa mbele katika kuzifahamu, kuzieleza, kuzitetea na kuzitekeleza sera na ilani ya uchaguzi ya CCM, awe mpenda haki na jasiri wa kupambana na dhuluma na uonevu.
Alisema anatakiwa asiwe mtu anayetumia nafasi yake ya uongozi kujilimbikizia mali, awe ni mtu anayekubalika na wananchi, makini katika kuzingatia masuala ya uwajibikaji wa viongozi na asiyevumilia uzembe wa majukumu au wajibu aliokabidhiwa ili kuinua nidhamu ya kazi tija na ufanisi.
Kutafuta wadhamini
Mangula alisema katika kipindi ambacho wagombea hao wanatafuta udhamini, chama kinafuatilia kila wanachofanya na kuweka kumbukumbu zitakazosaidia kupata wasifu wa mgombea husika.
“Wakati huu wa kutafuta wadhamini, kila kilichofanywa na mwanaCCM anayetafuta wadhamini 450 kitaingia katika kumbukumbu za tathmini ya mgombea mtarajiwa,” alisema.
Mangula aliziagiza kamati za maadili za wilaya kukutana mara moja baada ya wagombea kujaza majina ya wadhamini wilayani na kuwajadili.
“Mihtasari iletwe mara moja makao makuu ya chama ili kamati ya maadili ya taifa itumie taarifa hizo za tathmini ya wilaya katika jumla ya kumbukumbu za kila mgombea mtarajiwa,” alisema.
Kampeni marufuku
Katika hatua nyingine; Mangula alipiga marufuku watia nia hao au mawakala wao kufanya vitendo vyovyote vinavyoonekana dhahiri kuwa ni sehemu ya kampeni za kuwania nafasi wanayoitafuta kabla muda wa kampeni.
Alitaja vitendo vinavyoashiria kampeni kabla ya wakati kuwa ni pamoja na utoaji wa misaada ambayo dhahiri ina lengo la kuvutia kura.
“Kanuni hii haitamhusu rais, mbunge, mwakilishi na diwani ambaye yupo madarakani,” alisema Mangula.
Mangula alieleza kuwa katika kipindi cha mchakato huo, CCM itatumia kanuni za uteuzi wa wagombea wake katika vyombo vya dola zilizotolewa na NEC ya CCM toleo la 2010. Pia alisema miiko ya shughuli za uchujaji na uteuzi inawataka wagombea hao kutofanya kampeni za kupakana matope dhidi ya wenzao.
Kauli za wachambuzi
Wakati mchakato wa kumtafuta mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala ukiwa umepamba moto, baadhi ya wanasiasa, wanataaluma na wananchi wa kawaida, wamesema kati ya wanaCCM takriban 24 waliokwishajitokeza, hakuna mwenye uwezo wa kuvunja mfumo mbovu wa utawala uliopo, hivyo wanayoahidi si rahisi kuyakamilisha.
Makada waliojitokeza ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere na Balozi Amina Salum Ally.
Pia, wamo Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangala, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Balozi Ally Karume.
Wengine ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Ofisi wa Rais (Kazi Maalumu) Profesa Mark Mwandosya na Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Sospter Muhongo.
Katika foleni hiyo pia wapo Mkurugenzi wa Kampuni ya Forecast Enterpreneurship, Boniphace Ndengo, Leonce Mulenda, Peter Nyalali, Wakili Mwandamizi wa Mahakama Kuu, Godwin Mwapongo, na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na leo wakitarajiwa, Dk Mwele Malecela na Balozi Augustine Maiga.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema Watanzania wanapaswa kutambua kuwa katika kutafuta kiongozi wa juu wanatakiwa kuangalia mfumo mzima wa uongozi ambao CCM imeshauharibu.
“Hata wakipata kiongozi mzuri kiasi gani, mfumo wao hauwawezeshi kutekeleza mabadiliko. Wananchi wajue mapema kati ya waliotangaza nia ni nani atathubutu kuuvunja mfumo uliopo?...hakuna. Tunapozungumzia mabadiliko ya kimfumo ni kuanzia ngazi ya taifa hadi katika vijiji,” alisema Nyambabe.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim aliyesema kati ya wote waliojitokeza hakuna anayemuona anafaa kutokana na kushindwa kuainisha namna atakavyovunja mfumo mbovu wa uongozi uliopo.
“Hakuna mgombea aliyezungumza atafanyaje kuuvunja mfumo huo hii ni kwa sababu utawaharibia hata wale watakaohusika kuwavusha katika kile wanachokitafuta.
“Binafsi sijapata kiongozi ambaye ataivusha Tanzania miaka 10 ijayo. Sijamwona mwenye ujasiri wa kuvunja mfumo mbovu uliopo na angekuwapo tayari angekuwa ameshazungumzia namna kuuvunja,” alisema Salim.
Mhadhiri Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Dar es Salaam, Daniel Kitwana alisema watangaza nia wote hawawezi kutekeleza mambo wanayosema kwa kuwa watalazimika kufuata mfumo wa chama, ambao umeshindwa.
Aliongeza kuwa hata waliotangaza kuwa watawaletea maendeleo wananchi kwa kuwa wanachukia rushwa hawawezi kufanya hivyo kwa kuwa watakapoingia madarakani watamezwa na mfumo wa chama hicho.
Ukanda
Kuhusu kitendo cha wagombea wengi kutangazia nia katika maeneo walikotokea, Salim alisema kutatengeneza tatizo la ukanda na ukabila ambao utaleta matatizo siku zijazo kwa kuwa kiongozi atakayepita ataanza kulipa shukrani kwanza eneo alikotokea.
Mkazi wa Tabata, Dar es Salaam, Hijja Omary (28) alisema kitendo cha makada wengi kujitokeza kuwania urais kunatokana na kukosa kiongozi msimamizi na ni sawa na kukosekana baba kwenye nyumba, hivyo kufanya kila mtoto kujiona anaweza kuongoza.
“Sioni kama kulikuwa kuna haja ya msururu wote huu wa watu kutangaza nia ya kuwania urais. Naweza kusema kinachotokea sasa ni vurugu. Maana licha ya kuwapo kwa sera za CCM, kila kada anayetangaza nia anatangaza sera yake. Kwa hali hii sioni kama kuna kiongozi wa kweli hapa,” alisema.
Katibu wa Kanda ya Dar es Salaam, Umoja wa Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco), Moses Kyando alisema kinachosikika ni matumizi ya lugha za kuwavutia wananchi, ili viongozi hao waingie madarakani, lakini wakishapata nafasi hawatafanya walichoahidi.
“Sidhani kama kuna jambo jipya, wengi hawana jipya. Kwa mfano kwenye elimu tumeshuhudia mfumo wa kutoa matokeo ya mitihani ukibadilishwa, mara wanasema Matokeo Makubwa Sasa (BRN), lakini hakuna kinachofanyika,” alisema Kyando.
Kada mkongwe wa CCM, Ibrahim Kaduma alisema kujitokeza wagombea wengi ni jambo zuri kwa kuwa kunatoa fursa kwa wananchi kumchagua wanayemwona anafaa.
Hata hivyo, alisema Watanzania hawana haja ya kuwa na wasiwasi wa rais ajaye kwa kuwa Mungu amekwisha waandalia kiongozi atakayeisaidia nchi kutimiza mipango yake ya maendeleo... “Mungu atafanya hivyo atatuonyesha mambo makubwa na magumu tusiyoyajua, atatupa mtu atakayeweza kutumia vizuri rasilimali tulizonazo.”
Mwenyekiti Mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Ameir Manento alisema ameona mabadiliko ndani ya CCM katika mchakato huo, hasa kwa kutoa uhuru wa kutosha kwa watangaza nia, wakiwamo wanaotaka kujitangaza tu.
“Kuna wengine wanataka kufahamika majimboni tu, ukimuuliza ‘una nia kweli’? Anakwambia ana nia, lakini wanataka kufahamika tu,” alisema Jaji Manento.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment