
Akizungumza na gazeti hili eneo la tukio mjini hapa, Mwenyekiti wa mtaa wa Kikundi kata ya Sabasaba Manispaa ya Morogoro, Ramadhan Chamchuwa (72) alisema kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme iliyotokea katika moja ya chumba cha mpangaji wa nyumba hiyo.
Chamchuwa alisema kuwa chumba hicho kinatumiwa na vijana, Ismail Madaraka mwanafunzi wa darasa la nne shule ya msingi Mwere B na George Peta na wakati tukio hilo linatokea hawakuwepo katika chumba hicho.
Hakuna madhara kwa binadamu yaliyotokea baada ya kutokea kwa tukio zaidi ya kuungua mali ikiwemo nguo na vifaa vingine vya ndani ya nyumba.alisema Chamchuwa.
“Kwanza nawashukuru wafanyakazi wa tenesco na kikosi cha zimamoto kwa kufika kwa wakati eneo la tukio na kila mmoja wao kuwajibika kutokana na majukumu yao ya kazi lakini kama wangechelewa pengine madhara yangekuwa makubwa.”alisema Chamchuwa.
Mmoja wa wapangaji aliyenusurika kifo yeye na mtoto wake Lailat Japhet (miezi tisa) alisema kuwa alikuwa amelala chumbani, kitandani akimbembeleza mtoto alale ili afanye shughuli nyingine lakini alivuta harafu ya moshi mzito na kumlazimu kutoka chumbani humo.
Japhet alisema kuwa baada ya kutoka chumbani, alikutana na mpangaji mwenzake ukumbi, Halima Mumba (54) na kugundua uwepo wa moshi katika chumba kimoja wapo na baada ya kufungua mlango walikutana na moshi mzito na moto ukianza kuwaka kabla ya kuwaita wanaume waliochukuaa jukumu la kuwaita watu wa tenesco na zimamoto.
Moto huo ulifanikiwa kuzimwa ndani ya dakika 15 huku chumba hicho kikiwa tayari mali zilizokuwemo zikiwa zimeteketeza na moto.
“Baada ya kuona ile hali ya kuwaka kwa moto katika chumba kile, akili ilienda mbali kwani niliingia chumbani na kumbeba mtoto na kutoka nje nikapoteza fahamu nimeambiwa kuwa nilipoteza dakika kama tano hivi.”alisema Japhet.
Walionusurika na kuungua na moto huo ni pamoja na watoto Shaaban Seleman (3), Lailat Shomari (Miezi tisa), Jesca Jophet (25) na Halima Mumba (54).
Kaimu mkuu wa kituo cha Fire, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Manispaa ya Morogoro, Awadh Hamza aliwapongeza wananchi kuwajulisha tukio hilo mapema na wao kuweza kufika eneo la tukio kwa wakati na kufanikisha kuzima moto huo.
Hamza alisema kuwa majanga ya moto au mengine yanayohitaji msaada kutoka katika taasisi za jeshi la polisi, jeshi la Zimamoto na Ukokoaji na Tenesco wananchi wanapaswa kutoa taarifa mapema ili wafanyakazi wa taasisi hizo waweze kunusuru maisha ya binadamu, mali na n:k.
Akizungumzia juu ya tukio hilo, Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo alisema kuwa amepokea taarifa za moto kuunguza chumba kimoja katika nyumba iliyopo mtaa wa Kikundi majira ya saa 5:25 asuhubi Manispaa ya Morogoro baada ya kutokea hitilafu ya umeme.
Paulo alisema kuwa katika tukio hilo hakuna madhara kwa binadamu ambapo hitilafu hiyo imesababisha uhalibifu wa mali mbalimbali katika chumba hicho.

0 comments:
Post a Comment