BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HALI TETE BUNGENI, WABUNGE SABA WA UPINZANI WAADHIBIWA AKIWEMO JOHN MNYIKA, TUNDU LISSU KWA KUPIGWA STOP KUHUDHURIA VIKAO VYA BUNGE DODOMA.

 
Dodoma. Hali tete ndani ya ukumbi wa Bunge jana iliendelea kutanda wakati Spika Anne Makinda alipolazimika kuahirisha kikao asubuhi kutokana na kelele na baadaye chombo hicho kuwaadhibu wabunge saba wa upinzani, wakiwamo watano waliozuiwa kuhudhuria hadi kumalizika kwa Bunge la 10.

Hali hiyo ndani ya Bunge iliendelea kwa siku ya pili mfululizo na mara zote kusababisha Spika kuahirisha vikao baada ya shughuli za Bunge kushindwa kuendelea kutokana na kelele za wapinzani wanaopinga kitendo cha uongozi kuwasilisha miswada mitatu kwa hati ya dharura wakidai hakuna haja ya haraka hiyo.


Jana Spika Makinda, ambaye aliwahi kukumbana na hali kama hiyo wakati wa mjadala wa sakata la Akaunti ya Escrow kwenye Bunge la 18, aliibuka na dawa mpya na kuitumia Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwaadhibu wabunge hao saba.


John Mnyika, Moses Machali, Tundu Lissu, Felix Mkosamali na Paulin Gekul, ambao wamekuwa wakipinga hoja mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na miswada mitatu iliyotakiwa kuwasilishwa kwa dharura kuanzia jana, wamefungiwa kushiriki vikao kuanzia leo hadi Bunge litakapovunjwa Julai 9.


Wabunge wengine wawili, Mchungaji Peter Msigwa na Rajab Mbarouk wamefungiwa kushiriki vikao viwili kuanzia leo baada ya Kamati hiyo kuwatia hatiani wawakilishi hao wote saba kwa kudharau mamlaka ya Spika.


Wengine watatu, Joseph Selasini, Khalifa Suleiman Khalifa na Rajabu Abdalah wanatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo leo saa 4:00 baada ya wito wa kuwataka wahudhurie jana kuchelewa.


Kikao cha jioni cha Bunge hilo, ambacho kilipokea taarifa ya kamati hiyo ya maadili na mapendekezo ya adhabu hizo, kilichelewa kuanza kwa saa moja na dakika ishirini kusubiri kumalizika kwa kazi ya kuwahoji watuhumiwa.


“Mashtaka yetu yaliendeshwa kwa haraka, hatukupatiwa muda wa kutosha kujieleza wala kumtumia wakili,” alisema Machali baada ya Bunge kuahirishwa.


“Pamoja na kuadhibiwa, hatutaogopa kusema kuwa miswada hiyo ina matatizo ili Watanzania wafahamu na iwapo miswada hiyo itapitishwa malalamiko ya vizazi vijavyo juu yatakayotokea kwenye sekta ya gesi yatakuwa juu ya Serikali na CCM.”


Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alisema ni bora kufukuzwa kuliko kuendelea kushuhudia gesi ya Watanzania ikiuzwa kwa nguvu bila ya huruma.


“Hii ni bora kuondolewa. Hukumu haikuwa ya haki na tungeweza kukata kukata rufaa kwenye Kamati ya Kanuni, lakini mwenyekiti wake ni Spika hivyo basi tena, acheni wafanye wanachotaka kukifanya,” alisema Lissu.


Mchungaji Msigwa, ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini, alisema hata angefungiwa kushiriki vikao vyote, asingeathirika.


“Adhabu tuliyopewa leo inayonyesha kuwa hatuna Spika... Spika yupo kiserikali zaidi hatendi mambo kwa haki. Akiamrishwa na Serikali anafanya kama alivyoambiwa,” alisema Mchungaji Msigwa.


“Binafsi hainiathiri hata wangenizuia vikao vyote ningekuwa na furaha kwa sababu hatukuhojiwa,” alisema Msigwa.


Adhabu ya kutohudhuria vikao
Kwa kawaida vikao vya jioni vya Bunge huanza saa 10:00 jioni, lakini jana lilianza saa 11:20 jioni na wabunge walikuwa wamejaa ukumbini tofauti na asubuhi.


Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya maadili, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi alitoa hukumu hiyo baada ya kueleza kuwa wabunge hao walikuwa wamevunja kanuni ya 74 (1) a,b ambayo inatoa zuio kwa mbunge yeyote kusimama na kupiga kelele wakati Spika akiendesha kikao.


Ngwilizi alisema kitendo cha wabunge hao kusimama na kupiga kelele kiliathiri shughuli za Bunge, kitu ambacho ni kinyume cha kanuni iwapo kitamlazimisha Spika kusitisha shughuli za chombo hicho cha kutunga sheria.


Ngwilizi alisema kamati yake iliwahoji wabunge saba walioitikia wito huo na baada ya majadiliano iliridhika kuwa walifanya kosa hilo ambalo alisema halina tija.


Ngwili alipendekeza wabunge hao watano wazuiwe kushiriki vikao vyote kuanzia leo na wengine wawili vikao viwili na kupendekeza watatu waliosalia wafike mbele ya kamati leo kwa ajili ya kuhojiwa, mapendekezo yaliyokubaliwa na Bunge na baadaye kujadiliwa kwa kifupi kabla ya Spika kuahirisha kikao.


Hata hivyo, mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo, Mchungaji Israel Natse alisema kuwa aliwaeleza wajumbe wenzake bayana kuwa watuhumiwa walitakiwa kuruhusiwa kwenda mbele ya kamati wakiwa na wanasheria wao au watu wengine wowote ambao wangewapendekeza, lakini kikao kiligoma.


Alisema baada ya wenzake kugoma, aliweka bayana kuwa hawezi kushiriki kwenye uamuzi ambao unakiuka haki ya msingi ya mtuhumiwa.


Wakizungumza nje ya bunge mara baada ya kutoka nje, Felix Mkosamali alisema kuwa hukumu hiyo ilitolewa kwa ubabe mkubwa na hawakupewa nafasi ya kujitetea kwani ulitumika ubabe zaidi.


Rajabu Mbarouk ambaye alihukumiwa kutoshiriki siku mbili, alilia na Spika akisema ndiyo chanzo cha vurugu hizo kwani alikuwa wa kwanza kuvunja kanuni kwa kupeleka miswada kibabe.


Kwa upande wake Machali, alisema hukumu hiyo ilikuwa ni ya kifisadi kwa kuwa mashtaka yao yaliendeshwa kwa haraka bila ya kupatiwa muda wa kutosha kujieleza wala kumtumia wakili.


Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu alisema bora ya kufukuzwa kuliko kuendelea kushuhudia gesi ya Watanzania ikiuzwa kwa nguvu bila ya huruma.


“Hii ni bora kuondolewa, hukumu haikuwa ya haki na tungeweza kukata kukata rufaa kwenye kamati ya Kanuni lakini Mwenyekiti wake ni Spika hivyo basi tena, achene wafanye wanachotaka kukifanya,” alisema Lissu.


Hukumu hiyo iliyotolewa jana haikujuisha jina la mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde ambaye alitajwa asubuhi na Spika kuwa mmoja wa watu waliotakiwa kufika mbele ya kamati.


Sakata la asubuhi
Mapema jana hali ilionekana kuwa ya kila upande kuchukua tahadhari baada ya kikao cha juzi kulazimika kuahirishwa kutokana na vurugu hizo. Baadaye wabunge walibaini kuwa miswada miswada hiyo mitatu- Muswada wa Sheria ya Petroli, Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na gesi na Muswada wa Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Uchimbaji yote ya mwaka 2015- ilikuwa imeingizwa tena kwenye shughuli za kazi. Kama ilivyokuwa juzi, jana mara baada ya kipindi cha maswali na majibu kupita, wabunge walisimama wakitaka kuomba mwongozo, lakini Spika alizuia kwani kulikuwa na kazi ya kupitisha Muswada wa Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi wa mwaka 2015 ambao ulikuwa katika hatua ya kamati.


Hali ilibadilika ghafla baada ya kumalizika kwa kazi ya kuupitisha muswada huo. Spika alimruhusu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene kusoma Muswada wa Sheria ya Mafuta na Petroli.


Waziri Simbachawene alipoanza kusoma, kelele za kuomba mwongozo zilianza.


Wakati huo, Lissu (CCM) na Khalifa Suleiman Khalifa (Gando–Cuf) walikuwa wamesimama wakitaka mwongozo wa Spika lakini hawakupewa nafasi ya kuzungumza.


Wakati Simbachawene akiendelea kusoma muswada huo yalianza kusikika maneno kutoka kwa wabunge wa CCM wakisema “wamezoea hao, usiwasikilize, achana nao”.


Kauli hizo ziliamsha hasira kwa wabunge wa upinzani ambao walihamasishwa na kusimama wakitanguliwa na Felix Mkosamali na Ezekiel Wenje ambao walianza kupiga kelele wakitaka wenzao wasimame.


Hali ilizidi kuwa mbaya zaidi baada ya wabunge zaidi ya 40 kutoka upinzani kusimama wote na kuanza kupiga kelele na kufanya maneno ya Waziri Simbachawene yasiweze kusikika kwa wabunge na watu waliokuwa ndani ya ukumbi.


Hali hiyo ilimfanya Spika asimame na kumtaka Waziri asiendelee kusoma Muswada na baadaye kutaja majina ya wabunge kumi na moja ambao aliona walikuwa wanavunja sheria.


“Sasa wapiga kelele nawataja kwa majina, Tundu Lisu (Singida Mashariki), Peter Msigwa (Iringa Mjini), John Mnyika (Ubungo), Paul Gekul (Viti Maalumu), na mbunge wa Rombo Joseph Selasini wote kutoka Chadema.


Wengine ni Wabunge wa NCCR – Mageuzi Moses (Kasulu Mjini) na Felix Mkosamali (Muhambwe) pamoja na wabunge wa Cuf Khalifa Suleiman Khali (Gando), Rajab Ali Abdarah na Rajab Mbarouk (Ole),” alisema Makinda.


Alisema wabunge hao wanatakiwa wafike mbele ya Kamati ya Maadili na baadaye kutamka kuahirisha shughuli za Bunge huku akiita kamati ya uongozi kukutana. Hiyo ilikuwa ni saa 5: 34 asubuhi.


Kilichotokea
Wakati Spika na makatibu wakitoka nje, wabunge wa upinzani walipeana ishara za kutoka nje huku upinzani wakitaka waendelee kuwa ndani ndipo zikaanza kelele kwa wabunge wa CCM kuanza kugonga meza kwa kuimba “CCM, CCM,CCM”, huku wapinzani wakiimba “wezi M, wezi M, wezi M”.


Wakiongozwa na Khalifa Suleiman Khalifa na Tundu Lisu, wapinzani walikubaliana kwenda nje na kuanza kikao cha wazi ndani ya ukumbi huku wabunge wa CCM na baadhi ya mawaziri wakiendelea kusikiliza kila kilichokuwa kikifanyika.


Waziri wa Nchi, Sera Uratibu na Bunge, Jenister Mhagama, aliwaita haraka wabunge wa CCM na kupaza sauti yake akisema: “Msiwe wepesi wa kutoka, hii miswada ni lazima na lazima itapita hakuna kuzubaa.”


Hata alipomaliza kuzungumza nao, wengi wa wabunge waliendelea kubaki ndani wakitaka kujua kinachofanywa na wenzao.


Katika kikao cha upinzani ambacho kilikuwa cha wazi, walikubaliana kutorudi nyuma hata kama watafukuzwa wote ndani ya Bunge, wakisema wanataka kurejesha heshima ya nchi.


“Hata kama itatokea sisi tulioitwa tukafukuzwa, bado ninyi mtakaobaki ndani endeleeni kukomaa hadi mwisho. Msiogope kufukuzwa na ikibidi hadi waweke mpira kwapani hawa,” alisema Lissu.


“Tukubaliane kuwa tutasimama pamoja na kukaa pamoja, tutacheka pamoja na kulia pamoja. Naombeni msicheze mbali zaidi ya kuwapa wenzetu nafasi ya kwenda kuswali,” alisema.


Lissu alisema kuwa uamuzi wa kuwafukuza ulishafanywa tangu juzi na kwamba jana waliingia kwenye Bunge wakijua nini kilikuwa kinaendelea na kuapa kuwa hawatashiriki dhambi kama iliyofanywa mwaka 1997.


Nje ya ukumbi
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini John Mnyika aliwaambia waandishi wa habari akisema: “Kinachofanywa na Serikali ni kiini macho kwani hakuna makubaliano kwenye muswada huo.”


Mnyika alisema kuwa upinzani wanayo taarifa kuwa kuna shinikizo kutoka mataifa ya nje wakitaka miswada hiyo isainiwe kuwa sheria kabla Rais Jakaya Kikwete hajaondoka madarakani na akasema hali ikizidi wataanika kila kitu hadharani.


Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Richard Ndasa alisema kuwa suala la muda wanalolilalamikia wapinzani halina ukweli wowote. Ndasa alitolea mfano kuwa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) walishachambua na kutoa mapendekezo yao vizuri hivyo wapinzani walikuwa na kazi ya kupinga kwa kuwa ziko dalili za mashinikizo kutoka nje ya bunge.


Ulinzi wamarishwa
Tangu juzi ulinzi umekuwa ni mkali kwenye viwanja vya Bunge na polisi wa kawaida wameongezwa kwa kiasi kikubwa.aarifa zilizopatikana jana na kuthibitishwa na mmoja wa wabunge wa CCM zinasema kuwa miswada huyo inawapa wakati mgumu kwani wanalazimishwa kuipitisha.


Mmoja wa mawaziri ambaye alisema sio msemaji aliliambia gazeti hili kuwa wameweka utaratibu maalumu wa kuhakikisha wanashinda na tayari wameshawaita wabunge wao kote waliko ili waende kuongeza nguvu.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: