Edward Lowassa ni miongoni mwa wagombea 40 wa urais ndani ya CCM katika uchaguzi mkuu Oktoba 2015 nchini.
Kamati Kuu Maalum (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), imekutana kwa dharura mjini Dodoma kupokea, kuchambua na kutoa baraka kwa vipaumbele na ahadi za Rais ajaye vilivyoainishwa katika ilani mpya ya uchaguzi ya mwaka 2015.
Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete; iliwaita Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wassira, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam ya Kuandaa Rasimu ya Ilani ya Uchaguzi, pamoja na wajumbe wake kwa ajili ya kuikabidhi na kutoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo.
Kamati hiyo ilikuwa na kibarua kizito cha kutoa ufafanuzi kuhusu Rasimu za awali ambazo zilikuwa zimefanyiwa maboresho na kisha kupatikana kwa ilani mpya itakayotumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kabla ya Rais Kikwete kuwasili mjini hapa saa, 8:37 mchana na kuendesha kikao hicho kwa zaidi ya saa nne; wapambe wa makundi ya baadhi ya wagombea wa kiti cha urais, walionekana wakirandaranda Makao Makuu ya CCM kwa lengo la kutaka kujua kinachoendelea baada ya kuitishwa ghafla kwa kikao hicho.
Wajumbe wa Kamati ya Wassira ni Anamringi Macha (Katibu), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy Mwalimu na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali-Zanzibar, Ali Juma Shamhuna.
Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Anthony Mavunde, Mbunge wa Manyoni Mashariki, Kapt. John Chiligati, na Mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz Aboud; ndio walioitwa ili kukabidhi ilani hiyo.
Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya CC hiyo, vilieleza kuwa ajenda nyingine ilikuwa ni kuwajadili wenyeviti 18 wa mikoa wa CCM ambao wanadaiwa kujilipua kwa kumuunga mkono mmoja wa wagombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015, kupitia chama hicho.
Ajenda ya tatu ilikuwa ni kupata mrejesho wa hali halisi ya mwenendo wa bunge; kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo inaundwa na vyama vinne vya Ukawa kuchafua hali ya hewa kwa siku mbili na kulazimika kuahirishwa ili kupata utulivu.
Awali, akifungua kikao hicho, Rais Jakaya Kikwete alisema, kikao hicho ni maalum kwa ajili ya kujadili Rasimu ya Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015.
CC YA ZANZIBAR LEO (JULAI 5)
Aidha, Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi kwa upande wa Zanzibar, nayo inakutana leo Makao Makuu ya CCM-Kisiwandui, Zanzibar kwa ajili ya kupendekeza jina la mgombea wa urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ); kwa tikiti ya chama hicho.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai ally Vuai, alisema kikao hicho kitafanyika saa 4 asubuhi, chini ya Makamu Mwenyekiti, atakayeteuliwa na kikao hicho, kwa kuwa Rais Dk. Ali Mohamed Shein ni mgombea urais, kwa hiyo hawezi kujijadili.
Alisema kamati hiyo inakusanya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kutoka Zanzibar na kukutana kwaajili ya kikao hicho cha kupendekeza jina la mgombea huyo. CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

0 comments:
Post a Comment