BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MESSI WA TANZANIA AWAZIDI ELIMU VIONGOZI WA SIMBA SC KATIKA SUALA LA MKATABA.


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiQNFYP2DPsxPwqKP-Z2VPFu31Kn4iPwrl2iMJWt_YWVeI-xNdD-bdzzfPvAI2TYHUdY6JWwme8wDSqbplm6TpCbRn7T58QfnXdZv-lP3FhUM3A8VeFyBI6rVdV6_lR0Sggqx3GH8zKiwJ1/s1600/MESSII.jpg 

Ramadhani Singano 'Messi' 

Dar es Salaam. Hatimaye Ramadhan Singano ‘Messi’ sasa yuko huru. Ni baada ya sakata lililodumu kwa miezi kadhaa baina ya mshambuliaji huyo na klabu yake, Simba ambayo ameibwaga.

Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilieleza jana kuwa mchezaji huyo yuko huru, hana mkataba na klabu hiyo.


Kutokana na uamuzi huo, Singano ana njia nyeupe kutua Azam, klabu inayoonekana kuhitaji huduma yake msimu ujao na inaelezwa kuwa tayari amemalizana na klabu hiyo tajiri nchini na muda wowote itamtangaza kama mchezaji wao.


Akizungumza na gazeti hili jana, Messi alisema, “Sijui kama niko huru, nilikwenda kwenye kikao na baadaye nikatoka, sijajua uamuzi uliotolewa, wewe ndiyo unanipa taarifa.


“Kama ni kweli, Mwenyezi Mungu amesikia kilio changu, sina budi kumshukuru,” alisema nyota huyo bila kuweka wazi mikakati ya baadaye kisoka zaidi ya kusema anatulia kwanza.


Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alibainisha jana kuwa Messi yu huru na kueleza kuwa kamati imefanya hivyo kutokana na maombi ya Messi.


“Kamati imeamua Messi awe huru kama alivyoomba,” alisema Mwesigwa kwa kifupi.


Naye mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe alieleza kuwa uamuzi huo ni wa upendeleo na kusisitiza wao (Simba) hawana namna zaidi ya kuyakubali kwani walioamua ndiyo wenye mpira wao.


“TFF ndiyo imeamua iwe hivyo, sisi hatua namna zaidi ya kukubaliana nayo, wafanye wanavyotaka,” alisema Hanspope.


Mapema jana, gazeti hili ilimshuhudia, Hanspoppe, Messi, mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji Soka Tanzania ( Sputanza), Mussa Kissoky, katibu mkuu wa TFF, Mwesigwa na wajumbe wengine watatu wakiwa katika kikao kizito cha kutatua mgogoro uliokuwa ukiendelea kwa muda sasa.


Habari za uhakika ambazo gazeti hili lilizipata kutoka ndani ya kikao cha Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji kilichofanyika jana makao makuu ya TFF zilieleza kuwa Singano amewagagaragaza Simba baada ya uongozi wa klabu hiyo kushindwa kupeleka vielelezo kuonyesha kuwa walimlipia kodi ya nyumba kama mkataba wake unavyotaka.


Chanzo huru kutoka ndani ya kikao hicho kilisema katika vielelezo vilivyowasilishwa na Simba, ilionekana kuwa klabu hiyo haikuwa ikimlipia malazi mchezaji huyo kwa mujibu wa mkataba wake.


“Kamati iliomba Simba itoe uthibitisho wa mshahara, bima na malazi ambako bima na mshahara vilikuwa sawa, lakini katika malazi kuna walakini, Simba walileta uthibitisho ukionyesha amelipiwa Sh600,000, lakini haionyeshi ni ya muda gani, hivyo kamati imegundua Simba ilikiuka katika hili na kuchukua jukumu la kumweka huru Messi.


Awali, kamati hiyo iliwataka Simba kupeleleka vielelezo vya malipo ya kodi ya nyumba kama walivyodai awali kuwa walikuwa wakimlipia nyumba mchezaji huyo.


Pia, ilionekana ni kweli mchezaji huyo amemaliza mkataba na klabu hiyo na siyo kwamba mkataba wake unamalizika mwakani kama ilivyodai klabu hiyo.


Messi aliingia katika mgogoro na Simba baada ya kudai amemaliza mkataba na klabu hiyo huku ongozi ukidai bado ana mkataba wa mwaka mmoja unaomalizika Julai mwakani.


Hata hivyo, Singano alipinga na kushikilia msimamo wake kuwa hana mkataba, uongozi ulighushi mkataba wake.


Kitendo cha Simba kuambiwa kuwa imeghushi mkataba kiliwakasirisha viongozi wa Simba na hivyo kila upande kuanza kutoleana maneno, jambo lililosababisha TFF kuita pande zote mbili na kukaa pamoja kwa lengo la usuluhishi.


Katika kikao hicho kilichosimamiwa na katibu mkuu wa TFF, Mwesigwa kila upande ulitakiwa kupeleka mkataba, lakini hata hivyo jambo la kushangaza TFF ilionekana kama iliibeba Simba baada ya kuzitaka pande hizo mbili kukaa na kuanza makubaliano ya kusaini mkataba mpya.


Kitu kilichowashangaza wadau ni kitendo cha TFF kushindwa kutoa majibu, hasa kuhusu upande gani ulighushi mkataba kati ya Simba na Singano.


Licha ya Simba kutakiwa kukaa na mchezaji huyo, uongozi wa klabu hiyo uliibuka na kudai hauwezi kufanya hivyo kwani wanachotambua bado ni mchezaji wao halali, jambo lililosababisha suala hilo kufikishwa Kamati ya Sheria na Hadhi ya wachezaji, ambayo jana ilikaa na kulitolea uamuzi.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: