Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Kibasila, Gaudensia Albart, anayedaiwa kuishi na kinyesi chumbani kwake, anaendelea na matibabu baada ya kugundulika alikuwa na matatizo ya akili.
Albart ambaye ni mtaalamu wa masomo ya Biolojia na Kemia, anaendelea na matibabu katika hospitali ya Muhimbili.
Habari zinadai kuwa awali baada ya vipimo, mwalimu huyo alionekana na matatizo ya akili ambapo daktari aliwajulisha kuwa ugonjwa huo haujafikia kwenye hatua mbaya kwani anaweza kutibiwa na kurudi katika hali yake ya kawaida.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa, mwalimu huyo anaendelea vizuri na amefanya mitihani yake ya Chuo Kikuu Huria (OUT).
Aidha, alisema mwalimu huyo amekuwa ni mzuri katika masomo ya Sayansi, anawapenda wanafunzi, hivyo tukio hilo liliwashangaza kama anaishi na kinyesi chumbani kwake.
“Kiukweli ni mwalimu mzuri huwa anafundisha kidato cha tatu na hata akitunga mtihani ni lazima atumie vitabu vitano,” alisema.
Februari 22, mwaka huu, mmiliki wa nyumba aliyopanga mwalimu huyo, Ruben Shayo, alidai kuonekana moshi kwenye chumba cha mwalimu huyo, ambapo wapangaji wenzake walitoa taarifa kwa mwenye nyumba wao kwenda kushuhudia moshi huo ili kuweza kujua chanzo chake.
Baada ya kuingia ndani waliona vyombo mbalimbalia ambavyo vilikuwa vimehifadhiwa kinyesi na mkojo, huku kukiwa na funza na mende wamezagaa hadi kitandani.
Tukio hilo liliwastaabisha watu wengi cha mtu kuweza kuishi na uchafu ndani ya nyumba yake. CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment