KATIBU Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mzee Yusuph Makamba, amesema watu wanaoendelea kulalamikia mchakato wa kumpata mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Magufuli, wana maslahi binafsi si kwa ajili ya kukiimarisha chama hicho.
Alisema wapo baadhi ya wana CCM na viongozi wanaoendelea kununa kutokana na kile kilichotokea Mjini Dodoma akisema si jambo sahihi hasa kwa chama kilichokomaa kama CCM kwa sababu ya ubinafsi wao.
Mzee Makamba aliyasema hayo Mjini Korogwe, mkoani Tanga juzi, katika mahojiano maalumu na gazeti hili juu ya mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM na kusisitiza kuwa, huwezi kutenganisha siasa na makundi kama ilivyo kwenye mpira wa miguu au ngoma.
Aliongeza kuwa, wanapojitokeza wagombea wengi kama ilivyojitokeza kwa wagombea waliochukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM kuwa mgombea urais wa chama hicho, lazima makundi yatokee.
"Kila kundi litamuunga mkono mgombea anayeona anafaa...makundi ya ushabiki wa mpira hayana mwisho hata kama timu yako ikishuka daraja utaendelea kuiunga mkono lakini ya kisiasa yana mwisho.
"Mwisho wake ni pale anapopatikana mgombea, mimi na baadhi ya marafiki zangu kama Alhaji Mwenda wa Dar es Salaam, Mzee Muya na Mbaruku wote wa Kiteto, tulimuunga mkono January si kwa sababu ni mtoto wangu, alikuwa na hoja nzito," alisema.
Alisema baada ya chama kumteua Dkt. Magufuli, yeye na marafiki zake pamoja na January, wako pamoja na mgombea huyo hadi kieleweke na watamsaidia kwenye kampeni zake hadi apate ushindi.
"Viongozi wanaoukubali ushindi wa Dkt. Magufuli hawako makini, wao kitu muhimu kwao ni mtu kwanza si chama, hili ni kosa pia ni ubinafsi, nampongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete kwa uvumilivu na msimamo alioonesha katika vikao vya uteuzi, pia naipongeza Sekretarieti ya CCM, Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu," alisema.
Mzee Makamba alisema vikao hivyo vimeteua mgombea mzuri ambaye anajiuza na kusisitiza kuwa, wana CCM wanapaswa kuwa kitu kimoja na kuvunja makundi yote ili chama kiendelee kuongoza dola.
"Namjua vizuri Dkt. Magufuli...ni mcha Mungu, hodari wa kazi na daima anaongozwa na falsafa ya Hayati Rais Abeid Amani Karume inayosema, usiogope kugombana na mwenzi wako katika jambo ambalo mtakuja kupatana...Kwa Dkt. Magufuli jambo lenye manufaa mtagombana lakini mwisho wa mafanikio, mtakuwa naye pamoja," alisema.
Aliongeza kuwa, utendaji pekee si kigezo cha mtu kuchaguliwa kushika uongozi bali kuna vigezo vingine kama uadilifu, namna unavyoonekana mbele ya jamii ambapo vigezo 13 vya kiongozi vilivyowekwa na CCM vinazidiana.
Alisema ndani ya CCM kuna wazee wenye busara ambao waliangalia vitu vingi hadi kuteua mgombea kwani unaweza kuwa mtendaji mzuri lakini ukawa na kasoro nyingi hivyo kuonekana unaweza ushindwe kukivusha chama kwenye ushindi.
Mzee Makamba alisema, wakati mwingine unakuta watu wote wana vigezo vinavyotakiwa na chama lakini ukivichunguza vigezo hivyo pia vinatofautiana.
"Wakati mwingine kwa kuwa nafasi inayotakiwa ni moja, inabidi muwakate wengine abaki mmoja maana hakuna njia nyingine...hata mimi kwenye utawala wangu nimeshawahi kuwakata wagombea wazuri," alisema Mzee Makamba.
Kauli ya Kingunge yapingwa
Katika hatua nyingine, Katibu wa CCM mkoani Mwanza, Miraji Mtaturu, amesema madai ya mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale- Mwiru kuwa mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM ulikiuka kanuni si kweli bali kauli hiyo imelenga kukivuruga chama.
Alisema kauli hiyo inaonesha Mzee Kingunge amenunuliwa na hayo anayoyasema ametumwa kwa sababu kila mtu alikuwa na mgombea wake na kudai ameshangazwa na kauli zake za kuwashambulia wazee wastaafu ambao ni viongozi wa chama akiwatuhumu kuendesha vikao vya kumpata mgombea urais kimizengwe.
Mtaturu aliyasema hayo jijini Mwanza jana na kuongeza kuwa, Mzee Kingunge aliaminika na kusifika akiwa mwalimu mzuri wa siasa wakati akifundisha somo hilo Chuo cha CCM Kivukoni na alikuwa akisisitiza 'Chama kwanza mtu baadaye' sasa inakuwaje leo anageuka.
Aliongeza kuwa, kitendo cha kada huyo kuwashambulia kwa maneno makali wajumbe wa Baraza la Ushauri la Wazee wastaafu kwa madai ya kubeba jukumu la Kamati Kuu (CC), anasahau mwaka 1995 wakati Hayati Mwalimu Julius Nyerere alipowakata baadhi ya wagombea.
Aliwataka waliokuwa wagombea wa nafasi hiyo, kuvunja makundi yao na kumuunga mkono mgombea aliyepita kwenye mchakato badala ya kuendelea kusema maneno ya kukivuruga chama.MAJIRA

0 comments:
Post a Comment