Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimezidi kupata mtikiso baada ya vigogo kadhaa akiwemo Mwenyekiti wa Mkoa kujitoa na kujiunga na Chama cha Demokrasi ana Maendeleo(Chadema) Waliojitoa na kujiunga na Chadema ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Dar es Salaa, John Guninita.
Kujitioa kwa viongozi hao kumefanya idadi ya vigogo waliojitoa CCM kufika 12.
Vigogo wengine waliotangulia awali kujitoa na kujiunga na Chadema ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa singida, Mgana Msidai, mwenyekiti wa CCM Arusha, Onesmo Ole Nangole na Katibu Itikadi na Uenezi Mkoa wa Arusha Issac Joseph, maarufu kadogoo na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Sumbawanga mjini, Emmanuel Kilindu.
Wabunge waliomaliza muda wao waliojitoa ni Mbunge wa Kahama Mjini, James Lembeli; Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye; Segerea, Dk. Makongoro Mahanga; Sikonge, Said Nkumba na Viti Maalum, Ester Bulaya.
Mgeja (pichani) alisema ameitumikia CCM kwa muda mrefu na kuwa ilikuwa na malengo na shabaha, kasoro zilizokuwapo zilikuwa zikirekebishwa, lakini kwa sasa chama hicho kimekosa mwelekeo.
“Chama ni cha wanachama, lakini CCM ya sasa hata taswira imetoka, chama kimeondoka kwenye taswira ya wanachama na sasa imekuwa kama kampuni au mali ya familia, tulipofikia ndani ya chama hiki, ni lazima malengo na matumaini yanapotea kabisa,” alisema.
Mgeja alisema wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais, yeye na wenyeviti wenzake wa CCM wa mikoa 23, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, baadhi ya wabunge na wana CCM waliona mabadiliko yanakuja kwa kumpata mtu atakayekata kiu ya Watanzania.
“Tuliona mabadiliko yanaweza kufanywa ndani ya chama kwa maslahi ya chama na Taifa na tukaona mtu huyu ndiye anaweza, tulishawishika anayeweza kutuletea mabadiliko ni Lowassa,” alisema.
Alisema katika mchakato huo walitegemea demokrasia pana ndani ya chama ingetumika, kwani gari lilipofika halihitaji dereva ambaye ni lena anayejifunza, lakini bahati mbaya mawazo ya wanachama yalipuuzwa.
Aliongeza kuwa yaliyofanyika Dodoma wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais hayakubariki na wala hayavumiliki.
Aliongeza kuwa wakati wa vikao vya CCM, kulikuwa na polisi wengi, polisi wa farasi, mabomu ya machozi na magari ya kuwasha hali iliyowatisha wajumbe na wale waliotoka vijijini walifyata mkia.
“Nimeamua leo kwa maslahi mapana ya nchi namuenzi Nyerere kwa vitendo aliyesema kama mabadiliko hayawezi kupatikana ndani ya CCM yatatafutwa nje ya CCM, kung’ang’ania ndani ya chama ambacho hakitaki mabadiliko ni tatizo, nimeamua kujiunga Chadema ili tukashirikiane na Ukawa alisema. Kwa upande wake, Guninita alisema amefanya kazi ndani ya CCM kwa miaka 35, lakini kwa hali ilivyo sasa chama hicho kimefika mwisho ni wakati mwafaka wa kufa.
“Chama cha siasa huishi kama binadamu, binadamu akiwa duniani hufikia malengo yake, CCM kilipofika kimekosa malengo yake na sasa kinaugua lazima kife,” alisema.
Wakati huo huo, viongozi wa CCM wa Kata ya Monduli Mjini, mkoani Arusha wametangaza kujiuzulu nyadhifa zao na kujiunga na Chadema kwa kile walichoeleza wamechoshwa na manyanyaso na matusi ya chama hicho dhidi ya Lowassa.
Waliojiondoa ni mwenyekiti, katibu, wajumbe wa kamati ya siasa, na mabalozi wote.
Wakizungumza katika mkutano na wanachama wa mtaa wa Sabasaba jana, viongozi hao walilalamikia kitendo cha kukatwa jina la Lowassa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia CCM uamuzi uliofanyika Julai 12 mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Monduli Mjini, Swalehe Ramadhan Kilavo, alisema amechukua uamuzi wa kuachia ngazi nafasi yake na kujiunga na Chadema kwa vile hajapenda jinsi Lowassa alivyoonewa katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Dodoma. CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment