MAJI YA SHINGO ?: MGOMBEA URAIS WA UKAWA EDWARD LOWAASSA HUENDA AKASHTAKIWA KWA KESI YA MAGENDO IKIHUSISHA KAMPUNI YA RICHMOND.
“Kwa sasa ninasubiri nione iwapo (kesho) leo wakati wa uzinduzi wa kampeni za Ukawa litagusiwa, nitaweka bayana mambo yote ambayo hayakuongewa bungeni kipindi kile,” Dk Mwakyembe.
Mbeya. Mgombea ubunge jimbo la Kyela, Dk Harrison Mwakyembe amesema moto wa kashfa ya mkataba wa kufua umeme wa dharura na kampuni ya Richmond haujazimika, hivyo mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa anaweza kufunguliwa “kesi ya magendo”.
Dk Mwakyembe, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyochunguza sakata la kuipa kampuni hiyo ya Marekani zabuni ya kufua umeme wa dharura mwaka 2008, aliliambia Bunge wakati wa majumuisho ya mjadala kuwa kamati yake haikusoma taarifa kamili ya suala hilo kwa hofu kuwa Serikali nzima ingeondolewa na kuomba uchunguzi mpya ufanyike ili yaibuliwe mengi zaidi.
Lakini miaka saba baada ya kashfa hiyo kuisha kwa Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu, Dk Mwakyembe ambaye ni mwanasheria kitaaluma, ameliibua tena wakati wa kampeni za mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli mjini Kyela.
Akizungumza katika mkutano huo jana, Dk Mwakyembe alisema suala la Richmond lilikuwa limekwisha, lakini anaona kuna watu wanalifungua.
“Kwa sasa ninasubiri nione iwapo (kesho) leo wakati wa uzinduzi wa kampeni za Ukawa litagusiwa, nitaweka bayana mambo yote ambayo hayakuongewa bungeni kipindi kile,” alisema Dk Mwakyembe.
“Nimesikia mtu mmoja akisema ‘jamani kama mgombea wa urais wa Ukawa alikuwa na makosa mbona hamkupeleka mahakamani?’ Unajua wanasema elimu ndogo ni janga, naomba wote wanisikie mimi ni mwalimu wa sheria, kesi zote za jinai hazina ukomo, acha kuchezea moto kwenye petroli. Tunaweza kufungulia kesi ya magendo, “ alisema Dk Mwakyembe kwa ukali na akishangiliwa na wakazi wa Mbeya mjini.
“Chondechonde, atakayekuja kuwa rais (Magufuli) anachukia sana ufisadi na alishatangaza ataunda mahakama maalumu ya mafisadi. Chondechonde, tusiichezee Tanzania, naomba wana-Mbeya kura zote kwa Magufuli.”
Wanasheria walonga
Kauli hiyo ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeibua hisia tofauti kutoka kwa wanasheria, huku wakili wa kujitegemea, Semgalawe Charles akikubaliana na kutokuwapo kwa kikomo cha kesi za masuala hayo, lakini akasema Lowassa hakupatikana na hatia wakati ripoti ya Kamati ya Mwakyembe iliposomwa bungeni.
Alisema mahakama na vyombo vingine ndivyo vyenye mamlaka ya kutoa hukumu na endapo kungekuwa na hukumu Lowassa asingepata nafasi ya kugombea urais.
Maoni kama hayo yalitolewa na mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba ambaye alisema wakati ripoti ile ikisomwa, hakukuwa na hukumu badala yake Waziri Mkuu wa kipindi kile aliambiwa ajipime na kujitathmini.
Akizungumza jana, mwanasheria mwingine, Fulgence Masawe alisema tatizo watu wanashindwa kutofauti tuhuma za kisiasa na jinai za mahakama, Lowassa alikuwa na tuhuma za kisiasa na ndiyo maana alijiuzuru.
“Kama ingekuwa ni jinai angechukuliwa hatua mapema hata urais asingeweza kugombea,” alisema Masawe.
“Tatizo la nchi hii ni kutochukua maamuzi kwa wakati matatizo yake ndiyo haya. Wanakumbuka shuka kumeshakucha. Lowassa aliwajibika kisiasa siyo jinai. Kama jinai sidhani kama angepata fursa hii anayogombania hivi sasa,” alisema Masawe.
Amnadi
Akimnadi Dk Magufuli, Dk Mwakyembe alimuelezea kuwa ni mchapakazi ambaye kamfundisha kazi ya uwaziri na siku zote hataki “zege lilale”.
Akihutubia maelfu ya wakazi wa Kyela kwenye Uwanja wa John Mwakangale, Dk Mwakyembe alisema anawafahamu wagombea wote wakuu wa urais mwaka huu na kueleza hana wasiwasi kuwa Dk Magufuli ataingia Ikulu.
“Lakini yule mwingine naye tunafahamiana sana hata ukweli wa suala lililomtoa uwaziri mkuu nilisimamia mimi,” alisema Dk Mwakyembe.
“Jamani mtoto wenu nasema ukweli tulipitisha uamuzi wa kweli bungeni kwamba baba tumekukuta jikoni ukichomoa mboga ya wazee... mzee tumekukuta jikoni unachomoa mboga za watoto halafu leo unaomba kura aaah, “ alisema Dk Mwakyembe na kushangiliwa na umati wa watu.
Mbunge huyo wa Kyela alisema walichokifanya bungeni kilikuwa sahihi na kinaishi na anaomba Mungu awapatie adhabu iwapo walisema uwongo.
Bila kutaja jina la mgombea huyo, Dk Mwakyembe baadaye akiwa Tukuyu wilayani Rungwe alimtaja kuwa ni “mgombea wa urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)”.
Kauli hiyo ya Dk Mwakyembe ilionekana kuwa kete kuu jana na aliirudia tena hadi Mbeya Mjini na kueleza hukumu iliyotolewa kipindi hicho bado inaishi.
“Sisi watu wa Kyela siyo waongo. Mimi nilikuwa bungeni tulitoa hukumu kuwa jamani fulani tulimwona anadokoa mboga. Sasa Ukawa wanamleta tena eti agombee urais, ngoja wamlete, tutamchapa, “ alisema Dk Mwakyembe.
Dk Mwakyembe aliwakosoa wagombea wengine wanaosema Tanzania inahitaji viongozi wenye uamuzi mgumu, akisema watu wa aina hiyo wanaweza kuwa vibaka na mafisadi ambao wanaamua huku wakijua kwamba wakikamatwa watashtakiwa na hata kuawa.
“Tanzania haihitaji kiongozi mwenye maamuzi magumu, bali inahitaji kiongozi mwenye kufanya uamuzi wa haki na busara kwani watu wenye uamuzi mgumu ni kama Idd Amini ambaye alijua Tanzania ni imara, lakini aliamua kuivamia,” alisema.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Magufuli aliwasihi Watanzania kutotumia jaziba kama watu wa Libya ambao walimwondoa Rais Muammar Gaddaf na mpaka sasa wanajuta.
Magufuli alisema CCM haina makosa, lakini makosa ni kwa mafisadi ambao wameiharibu nchi na kwamba yeye amepania kuondoa kasoro zote hizo.
Akihutubia mjini Tukuyu, Rungwe, Dk Magufuli aliahidi kujenga kwa lami barabara ya Kyela-Kikusi-Matema Beach yenye urefu wa kilomita 39. 5 kwa Sh56 bilioni, akisema mkandarasi tayari yupo eneo la kazi.
Huku akiongea kwa tabu na kwa muda mfupi kuliko mikutano ya awali kutokana na kukauka sauti, Dk Magufuli alisema ataboresha huduma za maji, afya, elimu, umeme, utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kwa wajasiriamali kwa kila kata na kijiji.
Sauti yakwama
Awali, Magufuli aliwaomba radhi wakazi wa Jiji la Mbeya akisema sauti yake imekwama na kwamba pepo lililochukua sauti yake “lishindwe”.
Alikuwa akizungumza kwa shida huku sauti yake ikishindwa kutoka. Maofisa wa karibu na mgombea huyo walisema tatizo hilo lilianza jana akiwa wilayani Chunya na kwamba sababu kubwa ni kuzungumza kwa nguvu katika mikutano 12 kwa saa tisa, wakati kawaida alitakiwa kuzungumza mikutano minne.
‘Unajua Chunya watu walikuwa wakimzuia mara kwa mara na yeye alikuwa akikubali kuwahutubia licha ya kuelezwa mara kadhaa, lakini alisisitiza anawapenda wananchi hivyo lazima aongee nao,’’ alisema ofisa ambaye alitaka jina lake lisiandikwe.
Akiwa mkoani Manyara, mgombea Mwenza, Samia Suluhu Hassan alisema Serikali ya awamu ya tano itakapoingia madarakani, itakamilisha haraka mradi wa maji wa Sh13 bilioni uliokwishauanza mkoani Manyara.
Moja kati ya miradi inayojengwa kuanzia Siha mkoani Kilimanjaro hadi miji ya Longido na Namanga, mkoani Arusha, ina lengo la kuondoa kero ya maji wanayopata wananchi wa maeneo hayo ambao wanalazimika kupangiwa kiwango cha kuchota maji ambacho ni ndoo 10 kwa wiki kwa kila familia.
Samia Suluhu alitoa ahadi hizo katika mikutano ya hadhara ya kampeni za urais, ubunge na udiwani zilizofanyika juzi, tarafa ya Longido mkoani Arusha.
Msafara wa Suluhu jana ulilazimika kusimama mara kwa mara akiwa njiani kutoka Karatu mkoani Arusha- kwenda Babati, Manyara kutokana na akina mama ambao walijipanga na kufunga barabara ili azungumze nao na kusababisha msafara wake kukwama kwa muda hadi alipozungumza nao
Msafara huo ulisimama Karatu, Magala wilayani Babati Vijijini na Magugu Vijijini.
Jana mgombea huyo alitarajiwa kufanya mkutano wake wa mwisho mkoani Manyara, na kuanza kampeni zake mkoani Singida.
Basi lapata ajali
Katika hali isiyo ya kawaida, basi dogo aina ya Toyota Coaster lilipata ajali kwa kuingia msituni baada ya kutaka kuugonga msafara wa mgombea huyo wa urais uliokuwa umesimama kwa dharura katika kijiji cha Kandete, Kyela.
Basi hilo lilidaiwa kukaidi amri ya polisi na kupita kwa kasi na dereva wake alipouona msafara umesimama, alilikwepeshea porini likiwa na abiria ambao walipata mshtuko baada ya kusimama ghafla kwenye magogo yaliyokuwepo eneo hilo.
Hakuna abiria aliyejeruhiwa huku mmoja wa wasafiri hao aliyejitambulisha kwa jina la Hamidu akisema dereva alikuwa akiendesha kwa kasi na alipoona magari yamesimama alipiga breki bila mafanikio na kulazimika kuingia porini.CHANZO:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment