Dar es Salaam. Mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa, ambaye leo atazindua kampeni zake kwenye viwanja vya Jangwani, jana aliamua kufunguka dhidi ya vitendo vya Jeshi la Polisi kupiga wananchi, akisema havikubaliki kwa kuwa vifaa vinavyotumika vinanunuliwa na kodi wanazokatwa.
Lowassa, ambaye anagombea urais chini ya mwavuli wa vyama vinne-Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi, anazindua kampeni hizo baada ya kukabiliana na vizingiti kadhaa vilivyowekwa na taasisi za Serikali kuanzia wakati anatafuta wadhamini hadi sakata la kibali cha kutumia eneo hilo leo.
Akizungumza jana wakati wa majumuisho ya ziara zake fupi za jijini Dar es Salaam ambazo pia zilikatishwa na mazuio kutoka Jeshi la Polisi na Wizara ya Afya, Lowassa alisema vitendo hivyo vinaweza kuifanya Serikali ishtakiwe iwapo kutatokea vurugu. “Haiwezekani hela za walipakodi zitumike na polisi kupiga mabomu ya machozi. Tutawapeleka The Hague (Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Kihalifu),” alisema Lowassa wakati akiongea na makundi mbalimbali kwenye Hoteli ya Lamada jana.
Lowassa pia alisema kuna watu wanazusha kuwa akiingia madarakani atawafukuza Watanzania wenye asili ya Asia, jambo ambalo alisema si la kweli na hawezi kufanya hivyo kwa kuwa yeye si rais wa zamani wa Uganda, Idi Amini.
Katika makundi hayo, kulikuwa na wasanii zaidi ya 60 wa muziki wa kizazi kipya na waigizaji filamu, wengi wao wakiwa ni wale ambao hawajaonekana kwenye mikutano ya kisiasa tangu kuanza kwa harakati za uchaguzi.
Mkutano wa leo unafanyika baada ya Chadema kukataliwa na Serikali kutumia Uwanja wa Taifa, wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000, na baadaye Ofisi ya Manispaa ya Wilaya ya Ilala kukatalia viwanja vya Jangwani kwa madai kuwa vilishakodiwa na CCM kwa siku tatu mfululizo kwa ajili ya matamasha ya wasanii.
Hata hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliingilia kati na chama hicho kikuu cha upinzani kuruhusiwa kutumia viwanja hivyo maarufu kwa michezo na mikutano mikubwa ya kidini na kisiasa.
Vyama vilivyo katika Ukawa vimepania kufanya mkutano mkubwa jijini Dar es Salaam kabla ya Lowassa kwenda Iringa kuanza rasmi kampeni za mikoani, na mgombea mwenza, Juma Haji Duni kuelekea Lindi na Mtwara.
“Tumekamilisha maandalizi kwa asilimia 90,” alisema Tumaini Makene, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Chadema, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo wa leo wa uzinduzi.
“Tutakuwa live (kusikika na kuonekana moja kwa moja kutoka Jangwani) katika redio nne na televisheni nne. Hatuwezi kutaja ni redio gani, lakini wananchi wawe makini na kuzingatia uwezekano wa wao kupata matangazo hayo kuanzia saa 9:00 alasiri mpaka saa 12:00 jioni,” alisema Makene.
Alisema baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa uzinduzi, Lowassa ataanza kampeni katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa kuanzia Mkoa wa Iringa ambako alikusanya wanachama wengi waliomdhamini wakati alipokuwa akiwania urais kwa tiketi ya CCM kabla ya kuhamia Chadema.
Lowassa anatarajiwa kutumia mkusanyiko wa leo kuanza kumwaga sera za chama hicho na Ukawa baada ya kushindwa kufanya hivyo kwenye mikutano ya awali kuepuka kukiuka sheria inayokataza kuanza kampeni mapema.
Katika taarifa yake ya jana, Jeshi la Polisi lilisema limejiandaa vizuri kuhakikisha kunakuwa na usalama kwenye viwanja hivyo na askari wake watalizunguka eneo hilo.
“Watu wanaruhusiwa kuja katika makundi madogo madogo kwa kutumia vyombo vya usafiri kama vile mabasi, magari madogo, pikipiki, watembea kwa miguu au baiskeli na si kusubiriana katika makundi makubwa yanayoashiria taswira ya maandamano,” inasema taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Mkutano wa leo utahudhuriwa pia na Duni, ambaye amepitishwa kuwa mgombea mwenza wa Lowassa baada ya Chadema kufikia makubaliano maalumu ya yeye kuhamia chama hicho akitokea CUF chini ya mpango wa ushirikiano wa Ukawa wa kujiandaa kushika dola.
Wengine wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano wa leo ni Seif Sharif Hamad, anayegombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Twaha Taslima (Kaimu Mwenyekiti wa CUF), Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema), James Mbatia (Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi), na Emmanuel Makaidi (Mwenyekiti wa NLD).
Mkutano wa leo umetanguliwa na matukio mengi ya kusigana baina ya Chadema na vyombo vya Serikali. Awali Chadema iliomba kufanyia mkutano huo kwenye Uwanja wa Taifa kutokana na idadi kubwa inayomfuata Lowassa kila aendako, lakini Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ilimkatalia kwa madai kuwa imeona kwa sasa uwanja huo ubakie kwa shughuli za kimichezo tu.
Baadaye Lowassa alifanya ziara fupi jijini Dar es Salaam, akianza kwa kupanda basi la daladala kutoka Gongo la Mboto hadi Chanika na siku iliyofuata alitembelea maeneo ya Tandale kabla ya Jeshi la Polisi kupiga marufuku safari zake likisema zinasababisha foleni zisizo na umuhimu kutokana na kuibuka kwa misafara kila anakokwenda.
Mbunge huyo wa Monduli pia alipanga kutembelea hospitali tatu za wilaya za Dar es Salaam, lakini Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikatangaza kuzuia ziara hizo, ikidai zingesumbua wagonjwa, kitu ambacho Chadema imekipinga ikitoa mfano wa mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu kutembelea hospitali mjini Moshi bila ya kubughudhiwa na vyombo vya dola.
Wakati Chadema na Ukawa wakijiandaa kwa mkutano wa leo, Ofisa Utamaduni wa Wilaya ya Ilala aliwaambia waandishi wa habari kuwa chama hicho kisingeweza kutumia viwanja vya Jangwani kwa kuwa vimeshachukuliwa na CCM. Hata hivyo suala hilo lilimalizwa juzi. Kutokana na msigano huo, NEC imewaagiza wakurugenzi wote wa wilaya, ambao pia ni wakurugenzi wasaidizi wa uchaguzi kuhakikisha shughuli za kampeni zinapewa kipaumbele wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Juzi Chadema ilikwepa vikwazo hivyo vya Serikali baada ya kuandaa mkutano wa ndani na wanawake wa makundi mbalimbali jijini Dar es Salaam uliofanyika katika jengo la Millennium Towers ambao ulihudhuriwa na wanawake kutoka katika kila kada. Katika mkutano huo, Mbowe aliwaomba wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi leo kwenye viwanja vya Jangwani kumsikiliza mgombea wa urais wa Chadema (Ukawa).
“Tunaomba Watanzania waje kwa mamilioni sio kwa maelfu,” alisema Mbowe kwenye mkutano huo na kuwaahidi wanawake wote watakaofika Jangwani kuwa wataandaliwa eneo maalumu ambalo litakuwa na ulinzi ili kuwawezesha kufuatilia matukio bila usumbufu.
Mkutano huo unafanyika katika eneo hilo ikiwa ni siku sita tangu mgombea wa CCM, Dk John Magufuli kuzindua kampeni zake kwenye viwanja hivyo akiwa ameambatana na Rais Jakaya Kikwete, marais wa zamani, Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi na makada wengine wa CCM.
19 wapata dhamana
Wakati kampeni za Chadema zikianza leo, wafuasi 19 wa chama hicho waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kufanya mkusanyiko na maandamano wameachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.
Wafuasi hao, ambao ni pamoja na wanafunzi na wafanyabiashara, walikaa Segerea kwa siku tatu kutokana na kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana. “Tutakuwa live (kusikika na kuonekana moja kwa moja kutoka Jangwani) katika redio nne na televisheni nne.
Hatuwezi kutaja ni redio gani, lakini wananchi wawe makini na kuzingatia uwezekano wa wao kupata matangazo hayo kuanzia saa 9:00 alasiri mpaka saa 12:00 jioni,” Tumaini Makene.chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment