Katibu wa Mipango na Mikakatiwa chama cha ACT-Wazalendo, Habibu Mchange akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu kufanyika kwa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho leo na kesho kwa ajili ya kumpendekeza mgombea urais kupitia chama hicho. Kushoto ni Katibu wa Fedha na Rasilimali wa chama hicho, Peter Mwambuja. (Picha na Fadhili Akida).
KITENDAWILI cha nani atapeperusha bendera ya Chama cha ACT-Wazalendo katika nafasi ya urais katika uchaguzi wa Oktoba hakijateguliwa baada ya kushindwa kuweka bayana atakayepewa jukumu hilo.
Juzi ACT-Wazalendo ilikuwa ni miongoni mwa vyama kadhaa vya siasa hapa nchini ambavyo vimechukua fomu ya urais katika ofisi za Tume ya Uchaguzi huku wakibainisha kuwa mashauri wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo ndiye aliyepewa jukumu hilo sambamba na mgombea mwenza Hawra Shamte, ambao wote kwa nyakati tofauti walikana kuhusika na kazi ya kupeperusha bendera ya ACT katika uchaguzi ujao.
Mkumbo aliweka bayana kuwa hatagombea nafasi hiyo, akisema: “Nimekuwa nikilitafakari jambo hili tangu Alhamisi nilipoombwa rasmi kutafakari uwezekano wa mimi kugombea baada ya juhudi zetu za kutafuta mgombea kushindikana.
Nimefanya mawasiliano mapana katika familia, ndani ya chama, chuoni ninapofanyia kazi, kanisani kwangu na kwa watu na taasisi mbalimbali ninazohusiana nazo. “Baada ya tafakari na mawasiliano mapana nasikitika kusema kwamba sina utayari na maandalizi ya maana ya kisaikolojia, kifamilia, na kisiasa kuniwezesha kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi huu.
Wakati Mkumbo akiyasema hayo, Shamte alipotafutwa kuthibitisha alijibu kwa kifupi, akisema: “Sina taarifa, sijui chochote na wala si mwanachama na sina kadi ya ACT na hata zilipo ofisi zao sizijui. Kimsingi, hakuna makubaliano yoyote kati yangu na ACT, hivi ninavyozungumza nawe niko ofisini kwangu.”
Akizungumza jana Katibu Mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba alisema awali Kamati Kuu ilimpendekeza Mkumbo, lakini baadaye ilikubaliana kuwa wasimsimamishe yeye kutokana na sababu mbalimbali.
“Tulifanya majadiliano na kukubaliana na uamuzi wa Kitila ili asigombee nafasi hiyo kutokana na sababu ambazo siwezi kuzisema maana haya ni mambo ya ndani ya chama,” alisema.
Aliongeza: “Mpaka sasa chama bado kinaendelea na vikao vya Kamati ya Uongozi kujadili suala hilo na kama litakamilika basi kesho (leo) tutamtangaza mgombea huyo.” Mwigamba alisema mbali na suala la mgombea urais, kamati hiyo pia ilijadili suala la kama ACT-Wazalendo endapo haitasimamisha mgombea wauunge mkono Ukawa au CCM.
“Ukitaka kutoa kitu dhaifu ni lazima kuweka kitu imara na katika vyama vyote ACT-Wazalendo tumejitathimini na kuona kuwa ni imara na tunapaswa kusimamisha mgombea urais,” alisema.HABARILEO

0 comments:
Post a Comment