Hivi karibuni serikali ilipitisha sheria ya kudhibiti matumizi ya mawasiliano na wakati huo huo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), pia imesema haitasita kufunga au kuchukua hatua za kinidhamu kwa kituo cha radio au runinga ambacho kitageuzwa kuwa genge au kijiwe kwa watangazaji kuacha kufuata kanuni na sheria za utangazaji.
Kutokana na ukiukwaji wa kanuni na taratibu za mawasiliano, ambazo husababisha migogoro na usumbufu mkubwa ikiwemo uvunjifu wa maadili katika jamii, Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa TCRA, Elizabeth Nzagi mwishoni mwa wiki hii alisema tayari mwaka huu idara yake imefungia vituo viwili vya redio ambavyo vipo mikoa ya Mbeya na Singida kwa kwenda kinyime cha sheria za utangazaji.
Mkurugenzi huyo alisema vipo vituo vingine ambavyo vimetimiza vigezo vya msingi na kupata vibali vya kuendesha matangazo pamoja na mawasiliano ya ujumla, alivitaja vituo vilivyopewa leseni kuwa ni Radio One Sterio, Capital FM Radio, East Africa Radio, Times FM, Upendo Radio, Tumaini Radio na Wapo Radio.
Alisema zipo radio na runinga ambazo zimeamua kujifanyia mambo zitakavyo ikiwamo kugeuza maeneo hayo kama vijiwe au magenge kwa watangazaji kuongea mambo ambayo hayastahili na kwamba licha ya kuwa hiki ni kipindi cha kampeni za kisiasa, idara yake haitaogopa kuchukua hatua yoyote.
Ikumbukwe kuwa mawasiliano ya redio huwafikia wasikilizaji wengi kwa muda mfupi, suala lolote linaloongelewa kwenye redio wasikilizaji huweza kuchukua hatua mara moja wakiamini kuwa walichoambiwa ni sera sahihi inayoweza kulinda maslahi ya msikilizaji.
Madhara yanayoweza kutokea kwa taarifa zinazorushwa na redio pamoja na njia nyingine za mawasiliano ambazo hazizingatii kanuni na maadili yakinifu, ni upotoshwaji wa jamii na uharibifu wa dhana nzima ya mawasiliano.
Wananchi wanahitaji kupata taarifa zinazohusu maendeleo yao, pia wanategemea redio kama chombo cha mawasiliano wapate elimu ya kuboresha uchumi wa maisha yao, ingawa pia wanahitaji redio ziwape burudani zinazozingatia maadili ya Kitanzania.
Mkurugenzi Nzahi alisisitiza kuwa ni wajibu kuwakumbusha watangazaji wetu na kanuni zibandikwe kila mahali wazisome kabla ya kuingia kwenye chumba kutangazia, alisema vituo vingine vinajiita kioo cha jamii, sasa alisema ni vyema yanayozungumzwa katika radio kuakisi sura inayoonekana kwenye kioo.
Alisema kinyume chake, wapo wanaozungumza lolote watakalo kwenye redio, hali ambayo inasababisha mmomonyoko wa maadili, akasema maamuzi ya bodi ni kuvifungia vituo hivyo kabisa, kwamba wao hawataogopa mtu hata wakati huu wa kampeni za kisiasa.
Wakati huo huo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya utangazaji wa TCRA, Frederick Ntobi, alisema kuelekea uchaguzi mkuu vituo vya radio na runinga vina dhamana ya kulinda na kutunza amani ya nchi, hivyo alisisitiza kuwa wamiliki wanapaswa kuhubiri amani muda wote.
Tunaunga mkono jitihada zote zinazochukuliwa na TCRA kudhibiti vyombo vya habari ili vifanye kazi kwa weledi mkubwa utakaozingatia maadili na kanuni zilizopo kisheria.
Tunaamini kuwa redio na vyombo vingine vya habari vinaweza kuijenga jamii yenye mwenendo na maadili mema kama vikifuata kanuni na maadili yao ya kitaaluma, kinyume chake vinaweza kusaabisha balaa.CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

0 comments:
Post a Comment