BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MNAOMPENDA EDWARD LOWASSA JE MMEYAFIKIRIA MAMBO HAYA YANAYOWAFANYA MUUNGE MKONO ?.

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa UKAWA kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Edward Lowassa na Mgombea Mwenza wake, Dkt. Juma Haji Duni wakiwapingua maelfu ya wafuasi wa vyama vya Siasa vinavyounda UKAWA, jijini Dar es salaam, Augusti 10, 2015, Picha ya maktaba.

 NAOMBA nikiri kwamba pamoja na kuwa mfuatiliaji sana wa mambo ya siasa, nchini na duniani kwa ujumla, si kawaida yangu kuandika hasa kuhusu siasa kwenye magazeti. 

Nimeaamua kuvunja kawaida yangu baada ya kuona mushkeli mkubwa kuhusu namna ambavyo siasa zetu zinakwenda katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba.

Liko vuguvugu kubwa limezaliwa sasa nchini, wananchi wengi wanasikika wakitaka mabadiliko, hii ni haki kabisa kwa sababu chini ya jua hakuna kitu cha kudumu isipokuwa mabadiliko. 


Hiyo kiu ya mabadiliko ni haja ya kawaida kabisa kwa binadamu yeyote.

Lakini kitu kinachonitisha kuhusu mabadiliko ya wanayoyatamani baadhi ya Watanzania, ni aina ya mabadiliko wanayoyataka, na mtu wanayeamini ataleta mabadiliko hayo.


Aliyekuwa mtia nia wa kuwania urais kwa tiketi ya CCM, ambaye sasa ni mgombea wa Urais kupitia Chadema, akiungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, ndiye anayeonekana kuwa mbeba bendera ya mabadiliko hayo. 

Sina tatizo binafsi na Lowassa, lakini kinachonitatizo ni vitendo vyake kuelekea katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Najiuliza ni kwa kiasi gani wafuasi wa Lowassa, walioko Chadema na Ukawa na wale wanaomfuata alikohamia kutoka CCM, wanachukua hata dakika moja kutafakari aina ya mtu wanayemuunga mkono kwa nguvu zote namna hiyo. 


Hayo mabadiliko wanayoyaimba kila siku yataletwa naye wanajua ni mbadiliko ya aina gani?

Sitaki kuwahukumu, lakini sina uhakika kama wanatafakari kwa makini aina ya mabadiliko wanayotaka na mtu wanayemtumaini kuongoza mabadiliko hayo.


Dalili zinaonyesha uko uwezekano mkubwa wanafanya hivyo kwa sababu wameamua kuwa mashabiki tu ili kuridhisha nafsi zao.


Duniani kote viongozi wanaoongoza mabadiliko au mapinduzi yaliyoleta manufaa kwa jamii zao, kwanza ni lazima wawe na falsafa wanayoisimamia, wawe tayari kuifikia falsafa hiyo, na zaidi sana wawe na msimamo unaoaminiki, kiasi kwamba yeyote anayemfuata anakuwa na uhakika na kauli na vitendo vya kiongozi huyo.


Kuwa na kigeugeu haijawahi kuwa sifa ya kiongozi wa dhati anayesimamia mabadiliko ya kweli kwenye jamii.


Nikimtazama Lowassa, kwa dhati ya moyo wangu, sioni kama ni kiongozi wa kuaminika, sioni ndani yake uongozi wenye uwezo wa kusimamia kauli zake kwa dhati, bila kujali zinaweza kumgharimu kiasi gani ili mradi anaamini katika msingi ya aina fulani. Siyasemi haya kwa sababu nina chuki binafsi naye, lakini nayasema kwa sababu ni mambo yaliyo dhahiri kwa kila mtu.


Mei 30, mwaka huu 2015, wakati anatangaza nia kuomba kuwania urais kupitia CCM, jijini Arusha haya ndiyo aliyotuambia Watanzania.


“Kiuchumi, tumeshuhudia ukuaji mzuri na kuongezeka kwa mapato ya ndani ya Serikali na uimarishaji wa mfumo wa uwajibikaji na ulipaji kodi. Kwa upande mwingine, Serikali ya Rais Benjamini Mkapa na Rais Jakaya Kikwete zimefanya kazi kubwa katika uendelezaji wa sekta ya mafuta na gesi asilia ambapo kiwango kikubwa cha gesi asilia kimegunduliwa.


“Tanzania sasa imekuwa ni miongoni mwa nchi zinazovutia uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo ambayo inatajwa kwamba inaweza kuja kubadilisha kabisa maisha ya Watanzania.


“Rais Jakaya Kikwete amefanya kazi kubwa katika kipindi chake na kama ambavyo amekuwa akisisitiza mara kwa mara katika hotuba zake za karibuni ni kwamba yeye ametekeleza wajibu wake.
“Pia amesema anamwachia atakayemkabidhi uongozi wa nchi yetu baada ya yeye kumaliza muda wake kuendeleza pale atakapoachia”.


“Serikali za awamu zilizotangulia zimeyajadili na kujaribu kuyatafutia ufumbuzi. Mimi pia nimekuwa sehemu ya jitihada hizi wakati wa utumishi wangu katika chama na serikali huko nyuma”.
Ilipofika Agosti 10, mwaka huu 2015, baada ya kuchukua fomu ya uteuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, alituambia Watanzania kwamba;


“Rafiki yangu Rais Jakaya Kikwete kauharibu uchumi wa nchi, lakini sitaki kutoa mashtaka nataka kuzungumza kwa data, mwaka 2005 wakati Rais Benjamin Mkapa alipomaliza muda wake kilo moja ya sukari ilikuwa shilingi 650 lakini sasa hivi kilo moja ni Sh. 2,300, mchele umepanda hadi Sh. 2,220, sembe ni Sh. 1,200 na kibiriti ilikuwa Sh. 50 lakini sasa hivi ni Sh 200,”


“Katika hali hiyo CCM haina haki ya kuendelea kutuongoza, nawaalika wenzangu waliobaki CCM waje bila haya, waelewe matumaini yapo ndani ya chama chetu, (Chadema)”.
Lakini akitangaza nia Arusha huu ndiyo ulikuwa msimamo wake kuhusu CCM;


“Najua kwamba Ilani ya CCM ya mwaka 2015 imo katika hatua za mwisho za kukamilishwa na itakapopata baraka za vikao vya chama itakuwa ndiyo msingi wa utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano itakayochaguliwa Oktoba mwaka huu.” Hapo alikuwa akimaanisha serikali itakayoongozwa na CCM, lakini akaongeza


“Lakini kama alivyotuusia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1995, wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi hapa nchini, Watanzania wasipoyapata mabadiliko hayo ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM!


“Sina shaka, CCM tunao uwezo wa kuwapa Watanzania mabadiliko wanayoyataka”.


Wiki chache baadaye msimamo wake ukawa huu; “Kwa mantiki hii nitakuwa mnafiki kama nitaendelea kujidanganya mimi mwenyewe na umma wa Watanzania kwa kusema kuwa bado nina imani na CCM au kuwa CCM ni chama kitakachowaletea ukombozi wa kweli wa kiuchumi, kisiasa na kijamii. 


CCM niliyoiona Dodoma siyo tena kile chama nilichokulia na kilichonipa malezi na maadili ya siasa yaliyojengwa kwenye misingi ya haki, usawa na uadilifu.”

“Ni dhahiri kwamba CCM imepotoka na kupoteza mwelekeo na sifa ya kuendelea kuiongoza Tanzania yetu. Mimi kama Mtanzania aliye na uchungu na nchi yake nasema imetosha na sasa basi!


“Hivyo basi, baada ya kutafakari kwa kina nimeamua kuwa kuanzia leo ninaondoka CCM na kuitikia wito wa Ukawa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuungana nao katika kuleta mabadiliko ya kweli ya nchi yetu”.


Ukiyasoma kwa umakini maneno haya, unaona wazi kwamba ndani ya kipindi cha majuma nane, amekuwa na misimamo miwili mizito inayokinzana kuhusu CCM.


Ninachokiamini mimi ni ukweli kwamba CCM inaweza kuwa na matatizo yake makubwa, lakini haiwezekani yakawa yalitokea ndani ya muda mfupi kiasi hicho, yaani kuanzia alipokatwa, na alipohamia Chadema. Kama kupoteza mwelekeo wa kuongoza hakuwezi kuwa kumekuja CCM ndani ya muda wa siku 30 tu, kama huo ubovu upo aliuujua tangu kabala ya kuchukua fomu kugombea Urais.


Sasa kama alitambua hilo, kwanini aliamua kuimwagia sifa CCM na uwezo wa ilani yake kuingoza serikali ya awamu ya tano, lakini alipokatwa ghafla zile sifa ‘nzuri’ za CCM zikafutika. Mara ghafla ikawa hakiwezi tena kuingoza nchi, msimamo ambao unakinzana na kauli yake aliyoitoa siku chache zilizotangulia.


Katika hili ni ama akiwa CCM alitudanganya ili apate anachokitafuta, au alisema ukweli na sasa akiwa Chadema, anatudanganya ili apate anachokitafuta, au anasema ukweli lakini awali alidanganya. Vyovyote vile inavyoweza kuwa, ndani ya muda huo wa kuhama kwake, kuna mahali amewahadaa na kuwadanganya Watanzania.


Hapa ndipo ninapopata shida, kwa sababu mtu ambaye kwa muda mfupi namna ile amekuwa na misimamo miwili tofauti inayokinzana kisiasa, unawezaje kumuamini kwamba hiki anachokisema sasa ni kweli na siyo uongo kama ambavyo alituambia Mei na anayotuambia sasa.


Sina uwezo wala mamlaka ya kumchagulia mtu aina ya mtu au chama cha kuunga mkono kwenye siasa, hilo litakuwa ni kuingilia uhuru wa mtu, lakini ninao wajibu kama raia mwema wa taifa hili, kuwakumbusha wananchi kuona kile ambacho inawezekana wengine hawakioni au hawataki kukiona.


Tunapotaka mabadiliko lazima pia tuukubali ukweli mchungu kwamba mabadiliko lazima yawe ni kwa manufaa mapana ya jamii yote, na siyo ya kikundi cha watu wachache, kuwatumia wananchi wengi kujipatia maslahi yao binafsi.


Mabadiliko yoyote yale lazima yasimamiwe na watu makini, wanaoweza kuaminika, kutumainiwa kutokana na uthabiti wa maneno ya vitendo vyao, umuazi wa kuwa na misimamo miwili inayotofautina mithili ya mbingu na ardhi ndani ya muda mfupi hivyo kwenye mambo makubwa ya nchi, haiwezi kuwa sifa ya kutumainiwa kuongoza mabadiliko tena.


Mwandishi wa Makala haya, amejitambulisa kuwa ni Juma Khalfani mtumishi mstaafu wa serikali na msomaji wa gazeti hili anayeishi Shinyanga.CHANZO http://www.raiamwema.co.tz
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: