DK SLAA KUIBUA MAPYA BAADA YA KUTOJISHUHUSISHA NA CHADEMA KWA MUDA MREFU KATIKA NAFASI YA UKATIBU MKUU.
Dar es Salaam. Baada ya kimya cha zaidi ya mwezi mmoja na kutoonekana hadharani, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa anatarajia kuzungumza na vyombo vya habari leo saa nane mchana jijini hapa.
Dk Slaa aliyekuwa anatajwa kuwa angepeperusha bendera ya vyama vinavyounda Ukawa kwenye kinyang’anyiro cha urais alikuwa adimu kwenye shughuli za chama hicho tangu aliyekuwa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa alipojiunga na Chadema Julai 28 akitokea CCM.
Kwa mujibu wa Azam TV, Dk Slaa anatarajia kuzungumza kuanzia saa 7.00 mchana na mkutano wake huo utarushwa moja kwa moja vituo vya runinga na redio.
Mara ya mwisho Dk Slaa alizungumza na Mwananchi Agosti 11 na kuikana akaunti ya Twitter yenye jina lake ambayo imekuwa ikitoa matamko mbalimbali kumhusu.
Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Dk Slaa kuzungumza na gazeti hili tangu alipojitenga na shughuli za Chadema, ikielezwa kuwa anapumzika na angejiunga nao mbele ya safari.
Matukio makubwa ambayo ameyakosa ni pamoja na kutambulishwa kwa Lowassa na kukabidhiwa kadi, kuchukua fomu za chama na kuzirudisha, kuchukua fomu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuzirudisha na uzinduzi wa kampeni.
Mbali na kukanusha kumiliki na kuendesha akaunti hiyo, Dk Slaa alirudia kauli yake aliyokuwa ameitoa kwa gazeti hili wiki moja kabla, kuwa angejitokeza kutoa msimamo wake muda muafaka utakapofika.
“Subira yavuta heri, sasa ili uipate hiyo heri unatakiwa kuvumilia. Kwa hiyo wakati ukifika nitazungumza tu na Watanzania,” alisema.
Alipoulizwa ni wapi alipokuwa wakati huo, alisema yupo Dar es Salaam anapumzika, lakini akasema yeye na mke wake, Josephine Mushumbusi walikuwa wanatarajia kusafiri kwenda nje ya nchi kwa wiki moja.
, ingawa hakuweka wazi nchi wanayotarajia kuitembelea.
Mara ya mwisho Dk Slaa kuonekana kwenye shughuli za Chadema ilikuwa ni katika kikao cha Kamati Kuu.Chanzo:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment