BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

UCHAGUZI MKUU 2015: CCM YAJIVUNIA DK MAGUFULI KWA REKODI YA UCHAPA KAZI SERIKALINI, HALI HIYO IMEWAFANYA IMPACHIKE JINA LA TINGATINGA. CHOMBO KISICHOCHOKA.


Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, John Pombe Magufuli akihutubia katika mkutano wa ufunguzi wa kampeni za chama hicho uliofanyika katika Vwanja vya Dar es Sala
Dar es Salaam.
John Pombe Joseph Magufuli ndiye mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi(CCM) anayetajwa na CCM kama ‘tingatinga’ kutokana na rekodi yake katika kazi.

Hakika ni kiongozi wa mfano katika Serikali inayomaliza muda wake, hata kufaa kuwania nafasi anayowania kutokana na rekodi nzuri ya utekelezaji na usimamizi wa majukumu yake tangu alipoibuka kwenye siasa za Tanzania mwaka 1995.

Amekuwa waziri kwa miaka 20 sasa, miaka 15 kati ya hiyo amehudumu katika wizara ya ujenzi, hivyo bila shaka anaijua Serikali na shida za wananchi, hasa kutokana na kazi ya uwaziri lakini pia kuhudhuria vikao vya baraza la mawaziri kwa kipindi chote.

Kihistoria Dk Magufuli alizaliwa Oktoba 29, 1959 wilayani Biharamulo mkoani Kagera (hivi sasa Chato ni wilaya ya mkoa mpya wa Geita) na atatimiza miaka 56 Oktoba mwaka huu.

Mgombea huyo wa CCM aliyemteua Amina Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza katika kuipeperusha bendera ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa tano wa vyama vingi nchini utakaofanyika Oktoba 25, alianza mbio za ubunge mwaka 1995 katika Jimbo la Biharamulo Mashariki sasa Chato, alipojitosa kwa tiketi ya CCM na alishinda na kuwa mbunge.

Akiwa na umri wa miaka 36, Dk Magufuli alishinda kiti hicho cha ubunge, kisha aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Miundombinu na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Katika Uchaguzi Mkuu uliofuata, mwaka 2000 Dk Magufuli aligombea tena kiti cha ubunge Jimbo la Chato na kushinda kwa mara ya pili, safari hii Rais Mkapa ambaye pia alishinda kiti cha urais kwa mara ya pili akamteua kuwa Waziri wa Ujenzi, wadhifa aliokuwa nao hadi Serikali ya Awamu ya Tatu ilipomaliza muda wake mwaka 2005.

Watendaji wa Wizara ya Ujenzi wanasema ni vigumu kumyumbisha Magufuli katika jambo analoona ndiyo sahihi, lazima litekelezwe kwanza. Tabia ya namna hiyo alikuwa nayo pia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwamba akishaamua jambo fulani na kama anajua njia yake, humtoi relini.

Wanamsifu kuwa muda wote huwa wa kwanza kuingia ofisini na wa mwisho kutoka na hachoki kufuatilia utendaji katika wizara, hali ambayo imejitokeza hata kwa Rais Kikwete anayemsifu mara kwa mara na ndiye aliyemwita jina la ‘Tingatinga’.

Mawaziri kadhaa akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wamekuwa wakisifu uchapakazi wa Dk Magufuli usitotetereka, asiye na ubaguzi, anayesimamia haki na sheria za nchi bila kusita wala kumwonea yeyote.

Aliwahi kuwatimua kazi wafanyakazi 400 kwenye mizani ya kupima uzito wa magari kutokana na kuhusishwa na rushwa na ubadhirifu, kisha kuajiri wengine hali inayoonyesha kutaka kujenga nidhamu kazini.

Mwaka huo wa 2005, Dk Magufuli aliingia kwenye rekodi ya wagombea ubunge waliopita bila kupingwa na kwa kutambua utendaji wake, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambapo alipambana na matatizo mbalimbali yaliyoikabili sekta ya ardhi na nyumba.

Anatajwa kuwa mkali dhidi ya watendaji wazembe, wavivu, wabadhirifu wa mali ya umma na wala rushwa na hasiti kuwachukulia hatua za kinidhamu ili kunyoosha utendaji kwa maslahi ya taifa.

Alidumu katika nafasi aliyokuwa nayo hadi mwaka 2008, alipomhamishia Wizara ya Mifugo na Uvuvi(maarufu wizara ya vitoweo), aliyodumu nayo hadi mwaka 2010.

Akiwa katika wizara hiyo, Dk Magufuli pia alionyesha umahiri mkubwa katika utendaji hasa kukabili uvuvi haramu huku akiweza pia kujua takwimu za samaki waliomo kwenye bahari, maziwa na mito nchini.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 ambapo pia alitetea kiti chake cha ubunge kwa mara ya nne mfululizo kwa kumshinda aliyekuwa mgombea wa Chadema, Rukumbuza Vedastus Albogast kwa kupata asilimia 66.39 ya kura, dhidi ya asilimia 26.55 za mpinzani wake.

Kufuatia ushindi huo, Rais Kikwete aliendelea kumwamini na kumteua tena kuwa waziri katika Serikali yake, safari hii akimrejesha katika Wizara ya Ujenzi, nafasi anayoishikilia hata sasa baada ya chama chake CCM kumpitisha kuwa mgombea urais.

Aliibuka kidedea akiwabwaga wanaCCM zaidi ya 38 waliowania kuteuliwa ‘kuibeba’ CCM, akiwamo Edward Lowassa ambaye baadaye alijiengua na kuhamia Chadema na sasa anawania kiti cha urais kupitia chama hicho chini ya kofia ya Ukawa.


Alivyochukua fomu na kurejesha
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alimwuliza Dk Magufuli kama atawania kuteuliwa kama walivyofanya wana CCM wengine, naye alimjibu kuwa anachukua fomu za urais, lakini bila mbwembwe, wala kuzungumza na waandishi wa habari tofauti na wengine walivyofanya.

Ndani ya chama chake anatajwa kujitenga na makundi, kutotumia pesa wala kuchangiwa na matajiri kusaka kuteuliwa hali inayomweka kwenye nafasi nzuri kuwatumikia Watanzania kwa uhuru akilinda maslahi ya taifa.

Juni 4, Dk Magufuli alijitokeza ofisi za Makao Makuu ya CCM, Dodoma, saa 11.30 jioni na kuchukua fomu za kuwania urais, akiwa amevalia sare za chama chake, suruali nyeusi na shati la kijani akisindikizwa na mbunge wa Nkenge, Asumpter Mshama na wapambe wengine wawili.

Kama alivyoeleza kwa Rais Kikwete, Dk Magufuli hakuwa na mbwembwe katika hilo, wala hakuzungumza na waandishi wa habari hali iliyotafsiriwa kuwa amewakimbia.

Juni 22, Dk Magufuli alirejesha fomu hizo kuomba kugombea urais kupitia CCM baada ya kukamilisha kazi ya kupata wadhamini katika mikoa 23 ya Tanzania Bara na Visiwani.

Julai 10, jina la Dk Magufuli liliendelea kung’ara, baada ya kuwamo katika majina matano yaliyopitishwa na Kamati Kuu ya CCM kwenda katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho ili kujadiliwa na kupata matatu yatakayopelekwa katika Mkutano Mkuu na kupata jina moja ambapo pia Magufuli aliibuka mshindi.

Dk Magufuli aliingia tano bora pamoja na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Bernard Membe, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Balozi Amina Salum Ali na baadaye akaingia tatu bora na kuibuka kidedea baada ya kupata kura zilizowazidi mabalozi Asha Rose Migiro na Amina Salum Ali. CHANZO:MWANANCHI.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: