BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAKALA: MABADILIKO YASIJE KULETA MASIKITIKO !.



Na Sheikh Mohamed Iddi Mohamed
Kwa tafsiri ya haraka haraka, kwa sasa neno ‘mabadiliko’ katika mustakbali wa siasa za kitanzania linamaanisha kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani kwa kupitia sanduku la kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.


Wengi wanaohubiri juu ya neno hili (mabadiliko) bado hawajaweka bayana kati ya udhaifu wa kinachobadilishwa na ubora wa hicho kipya. Lakini yapo maswali mengi sana yanayoingia kati katika kadhia hiyo ya kampeni ya mabadiliko.


Kwa bahati mbaya sana, wanaohubiri hayo mabadiliko wanaendelea kuyafafanua kwa jazba zaidi badala ya hoja zaidi, jambo ambalo ni muhimu sana kwa Watanzania kutahadharishana mapema kwamba, mabadiliko yasije kuleta masikitiko!!!


Ni vizuri sote tukakubaliana kwamba mabadiliko kwa tafsiri ya maboresho ya maisha, hakuna hata mmoja miongoni mwetu asiyeyahitaji. Lakini mabadiliko kwa tafsiri ya kuiondoa CCM madarakani, yanahitajia sana angalizo kwani ni lazima kwanza tuichunguze hiyo CCM halafu tukichunguze hicho chama tunachotaka kiwe ndicho mbadala wa CCM.


Tukiamua kutumia kura zetu kwa jazba tu bila ya kutafakari kwanza, tutajuta majuto yasiyo na mwisho kwani inajulikana kwamba watawala wakikamata madaraka ni vigumu sana kuwanasua.


Tukiangazia mabadiliko kwa maana ya kuiondoa CCM ndipo tunapolazimika kuitazama CCM kwanza na kisha kukitazama na kukitafakari hicho chama ambacho kitakuwa mbadala wa CCM. Na tukimaanisha mabadiliko ni kumkataa mgombea wa CCM, ni lazima tuangalie ubora na udhaifu wa mgombea wa CCM halafu tuangalie ubora na udhaifu mgombea wa chama kingine.


Baada ya kufanya uchambuzi wa aina hiyo kisha tukakubaliana na uhalisia wa uwezekano wa kiakili, hapo ndipo tuamue kwa hiyari zetu kuiondoa au kuibakisha CCM. 


Kama Watanzania tutaamua tuinyime kura zetu CCM kwa sababu tu ya ‘kutamani’ mabadiliko kama wenzetu wa nchi kadhaa za jirani namna walivyomudu kubadilisha vyama vyao vya siasa vya zamani na sasa wanaongozwa na vyama vipya, tutajutia sana uamuzi wetu huo kwani Mtanzania anazifahamu vyema kero na matarajio yake kwa viongozi wake.


Hebu tuangalie dhana ya mabadiliko kwa kuiangalia CCM na vyama vingine ili tujiridhishe kwanza kabla ya kufanya maamuzi.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mwenyekiti wake kwa sasa ni Mheshimiwa Jakaya Kikwete ambaye kwa sasa ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayemaliza muda wake. 


Chama ambacho kwa sasa ndicho chenye nguvu ya upinzani ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho Mwenyekiti wake ni Mheshimiwa Freeman Mbowe. Tukiutazama wasifu wa Mheshimiwa Kikwete na wa Mheshimiwa Mbowe, inatosha kujenga nguvu ya hoja kichama juu ya nani abakie, ni nani atoke au asiingie.

Katibu Mkuu wa CCM ni Mheshimiwa Abdulrahman Kinana, na Katibu Mkuu wa chama chenye nguvu ya upinzani msimu huu (CHADEMA) ni Mheshimiwa Dokta Wilbrod Slaa ambaye amejiondoa kwenye ukatibu mkuu, na kwa sasa CHADEMA ni chama ambacho kina Katibu Mkuu anayekaimu.


Kama tunapohitaji mabadiliko tunakusudia kubadilisha chama, basi maana yake ni kwamba tukikatae chama ambacho Mwenyekiti wake ni Rais wa nchi hii ili twende kwenye chama ambacho Mwenyekiti wake hatoshi katika wasifu wake. 


Tukiache chama ambacho wasifu wa Katibu Mkuu wake na historia yake ya utumishi katika ngazi mbalimbali za serikali na chama ‘vinatosha’, halafu twende katika chama ambacho hakina kabisa Katibu Mkuu mpaka sasa.

Ni vizuri kama lengo letu tunapozungumzia mabadiliko kwa tafsiri ya kubadilisha chama, tukavilinganisha hivi vyama viwili (CCM na CHADEMA) kabla ya kufanya maamuzi. 


Lakini pia inatupasa kujiuliza tena na tena kwamba lengo letu katika kubadilisha chama ni nini?! Je, hatutaki jina lake la CCM? Je, hatutaki rangi za sare zake za kijani na njano? Je, hatutaki majina ya viongozi wake? Ni lazima tubainishe ni nini hatutaki katika CCM ili hata tukibadilisha chama huko tuendako tusiyarudie hayo yaliyotutoa huku. Vinginevyo, tukiendelea na hizi jazba za siasa tutajuta sana baadaye.


Ni vipi leo hii mwana CCM akitoka katika chama chake na akahamia upinzani tayari ameshapata ‘utakatifu’ bila ya kufafanua ameupataje huo usafi au tumempaje usafi huo? Na Je, sisi tunaomtakasa tunazo nguvu hizo kwa mtazamo wa jamii hii tunayoiongoza? 


Hivi ni kweli kwamba mabadiliko ambayo Watanzania wanayahitajia ni kuja kuongozwa na wana CCM wale wale walioamua kubadili sare na jukwaa?!! Je, hayo ndio malengo yetu na tafsiri yetu ya msamiati wa mabadiliko?!! Kama kweli ni hivyo, Watanzania tutakuwa tumefunikwa akili na uelewa wetu na wanasiasa, na hilo ni jambo la hatari sana.


Kama lengo letu katika kuhitajia mabadiliko ni ubora wa mgombea urais, ukweli ni kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hakiwezi kumuelezea katika jamii ya Watanzania mgombea wake kwa sababu ni mgeni kwao na hawamfahamu vizuri. 


Kwa muktadha huo, CHADEMA kinamnadi na ‘kumuuza’ katika jamii mgombea ambaye wao wenyewe kama chama hawana majibu sahihi kuhusu mgombea huyo. CHADEMA hawawezi kujibu ni kwanini CCM walimkataa mgombea huyo asigombee kupitia chama hicho? Na Je, sababu za CCM kumkata na kumkataa ni za kichama au ni za kijamii? 


Hivi chama makini chenye viongozi makini wenye nia njema kwa Watanzania, kinatuomba tumpe kura mgombea wake katika ngazi ya urais wakati wao wenyewe hawajui kwanini amejiunga nao muda si mrefu? Hata hiyo timu ya taifa ya mpira wa miguu pamoja na kuwa na wachezaji hodari na wenye uzoefu, bado wanahitajia muda wa kujuana na kuzoeana. 


Madhara ya kutojuana na kuzoeana ndio haya tunayoyashuhudia yakijitokeza. 


Mheshimiwa Edward Lowassa ambaye ndiye mgombea wa urais wa Tanzania kupitia CHADEMA, anakilalamikia CCM kwa namna kilivyoua elimu kwa miaka hamsini ya utawala wa CCM (ingawa yeye amesoma ndani ya miaka hiyo hiyo). 

Baada ya yeye kumaliza kuzungumza, mgombea mwenza kupitia CHADEMA, Mheshimiwa Juma Haji Duni akasema kwamba yeye amesoma elimu ya msingi, sekondari mpaka chuo kikuu na hatimaye kwenda Ulaya kimasomi, na yote hayo kafanyiwa na Serikali bure.


Hayo ndiyo madhara ya wachezaji wazuri na hodari wa timu ya taifa waliokosa muda wa kukaa pamoja kujuana na kuzoeana, hatimaye mgombea urais na mgombea mwenza wanapingana kiuelewa wakiwa jukwaani.


Sasa kama neno ‘mabadiliko’ ni kuwapa thamani wagombea kwa wagombea, hapo lipo tatizo la wagombea ambao wapo katika chama kipya huku kila mmoja akitokea kwenye chama tofauti. Je, ndio CCM tuiondoshe kwa kura na tubadilike kwa kuwapa hao wagombea wapya ambao wao wenyewe hawajabadilika kwa kuacha kila mmoja sera za chama chake cha zamani?


Hivi hapo hatuoni kama na sisi pia tunataka kubadilisha gia angani?!!

Lakini Mtanzania kuwa makini pale unapoambiwa kwamba elimu itakuwa bure kuanzia shule ya awali hadi chuo kikuu, bila ya kusikia vyanzo vya mapato ya serikali yatakayoweza kukidhi gharama za utekelezaji wa sera hiyo ya elimu ili iendane na mfumo wa kisasa wa elimu!


Tukumbuke kwamba idadi ya wanafunzi kwa sasa ni kubwa kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu. Je, bure hiyo itaendana na ubora au ni bure kwa maana ya bureee?!! Mgombea anayeahidi elimu bora bila ya kuelezea pato litakalokidhi gharama za uendeshaji wa sera yake hiyo, tunahitaji umakini mkubwa sana katika kuyapokea anayoyazungumza. 


Kutaja tu mapato kutokana na gesi na mafuta hakutoshi bila ya kuweka bayana mpango mkakati wa kuiepusha nchi na sera za kinyonyaji za kimataifa zinazoongozwa na wachumi na wafanyabiashara wa kimataifa wakishirikiana na serikali na asasi zao (Multi-nationals), ikizingatiwa kuwa hata mahusiano ya kimataifa na diplomasia kwa ujumla yamegeuka kuwa ya kiuchumi zaidi (Economic Diplomacy) na maana yake ni kuwa kipaumbele kikuu cha siasa za kimataifa ni kuangazia namna ya kunufaika kiuchumi wakati mwengine hata bila ya kujali utu wa mwanadamu.

Kwa upande mwingine, Watanzania tukubali kwamba kitendo cha mgombea urais wa CHADEMA ambaye ni kada aliyelelewa na kufundishwa siasa ndani ya CCM kuendesha mchakato wake wa kuelekea Ikulu kwa kutumia kinachoitwa ‘Timu ya Lowassa’ na kuwaacha kimkakati makada wa upinzani (UKAWA), hiyo ni dalili kwamba masamiati wa ‘mabadiliko’ umekusudiwa kubadili jina tu la kiongozi pamoja na sare za chama, na hapo ndipo pa kutafakari sana. Hivi kwani sare ya chama inachosha? 


Au kama tatizo ni jina la mgombea, basi hakuna haja ya kwenda kwenye mabadiliko kwani hata CCM ‘wamebadilika’ kutokea mgombea wao ndugu Jakaya Kikwete na sasa anayenadiwa ni ndugu John Magufuli. 


Nihitimishe Kalamu yangu kwa kuuliza: hivi kuiondoa CCM madarakani kama tatizo sio sare za chama bali ni ‘mfumo’; Je, hawa wana CCM waliohamia upinzani ambao baadhi yao wamesema wanakwenda ‘kutia nguvu’, nao wataongoza kwa mfumo upi? 


Kwani kimantiki waahamiaji hawa kutoka CCM hawaujui mfumo usiokuwa wa CCM iliyowalea na kuwakuza, ni vipi tutarajie uongozi mpya katika mfumo wa zamani?
Jamani tuwe makini sana na ‘mabadiliko’ tunayoyahitaji. Isije mwisho wa siku mabadiliko yakaleta masikitiko!!!
Naomba kuwasilisha.

Mwandishi wa makala haya ni Mwenyekiti wa ARRISAALAH ISLAMIC FOUNDATION. 


Unaweza kuwasiliana naye kwa namba: +255 754 299 749, +255 784 299 749. Makala hii pia inapatikana katika gazeti la Umma Tanzania ukurasa wa 11.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: