WAKATI mchuano wa kuwania urais ukizidi kupamba moto, mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli, amesema Serikali yake itakuwa rafiki wa wawekezaji wasafi wasio na madoa.Alitoa ahadi hiyo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Bumbuli, mkoani Tanga. Dkt. Magufuli alisema wawekezaji wa ndani na nje ya nchi watakapojenga viwanda vingi watasaidia kuongeza ajira.
"Tunahitaji ajira kwa ajili ya Watanzania wengi. Tutahamasisha Watanzania waanzishe viwanda, vikiwemo vidogo ili kuongeza ajira," alisema.
Alisema kuwa Serikali yake itakuwa rafiki wa Watanzania wote, hususan wenye maisha ya chini, kwa kuwa hawataki shida hasa zinazosababishwa na wakubwa. "Tunahitaji wawekezaji na tutaongeza viwanda vya kutosha ili kuongeza ajira kutoka asilimia 9.9 ya sasa hadi asilimia 40, hususan kwa vijana.
"Tunapokuwa na ajira nyingi kwa vijana, wanaume na wanawake tutapunguza shida mbalimbali zinazojitokeza, ndiyo maana serikali itahakikisha inaanzisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.
Ili kuhakikisha viwanda hivyo vinaanzishwa na kufanya kazi, alisema serikali yake itahakikisha unapatikana umeme wa uhakika, ikiwa ni pamoja na kuendeleza miradi ya umeme vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Kwa kufanya hivyo, alisema serikali pia itapunguza tatizo la umaskini kwa Watanzania ambao ni asilimia 28.2.
"Tunataka umaskini tuupunguze nchini zaidi na tukishaupunguza vijana itakuwa si rahisi kuwadanganya, wanapokuwa maskini na kukosa kazi ni rahisi kurubuniwa. Mtu anaweza akaja akasema mkinifanyia hivi nitawapa hiki.
Wakati mwingine vijana wanadanganyika, wanasahau kwamba asiyefanya kazi na asile, wanashindwa kuelewa kuwa hakuna cha bure," alisema.MAJIRA

0 comments:
Post a Comment