BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MPASUKO WAJITOKEZA NDANI YA VYAMA VYA UPINZANI UKAWA, MADIWANI WA CHADEMA WANYIMWA VITI VYA KUKALIA MKUTANO WA KAMPENI YA NCCR-MAGEUZI

Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, ambaye pia ni mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia 
Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, ambaye pia ni mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia.

MPASUKO ndani ya vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, umeanza kushika kasi baada ya madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kunyimwa eneo la kukaa kwenye mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za chama cha NCCR-Mageuzi Jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro.

Uzinduzi huo ulifanywa juzi na Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, ambaye pia ni mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Marangu (TTC), ambapo madiwani wa Chadema hawakutengewa eneo la kuketi wala kunadiwa, jambo walilodai ni kudhalilishwa.

Kutokana na mpasuko huo, Mbatia bila kumtaja mgombea na chama, alisema hawezi kumnadi mgombea anayechana mabango yake kamwe, huku madiwani hao wa Chadema wakiahidi kuendelea na kampeni zao na wana uhakika wa kushinda kwa sababu wanakubalika.

Wakizungumza na gazeti hili kwenye mkutano huo kwa masharti ya kutoandikwa majina yao, madiwani hao wa Chadema, walisema licha ya vyama vinavyounda Ukawa kuweka makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja kwenye kila jimbo na kata, NCCR wameshindwa kutekeleza agizo hilo kwa kusimamisha wagombea wa udiwani kata zote huku Chadema nao wakifanya hivyo.

Mmoja wa madiwani hao kupitia Viti Maalumu, alisema ni vigumu kukubaliana na hali kutokana na wao kutumia gharama nyingi, na kubainisha kuwa katika jimbo hilo Chadema ndicho chenye kukubalika zaidi, hivyo ingekuwa vyema wangeachiwa nafasi za udiwani kutokana na wao kuwaachia kiti cha ubunge.

Alisema licha ya kunyimwa kuketi kwenye mkutano huo na kushindwa kutambulishwa, wataendelea na msimamo wao hata kama wakipelekwa kwenye kamati ya maridhiano kama ilivyokuwa awali, hakitabadilika chochote.

“Tumetumia gharama nyingi sana kutangaza chama chetu cha Chadema, na tumeanza kuwa na mizizi muda mrefu, lakini Mbatia kaja juzi tu tena kwa sababu ya Ukawa, isitoshe mgombea urais anayefanya Ukawa uuzike yupo kwenye chama chetu, hivyo ukiona watu wanaukubali Ukawa ujue ni Chadema,” alidai mgombea huyo.

Alisema endapo wagombea udiwani kupitia NCCR- Mageuzi, hawataondolewa na wao hawatakubali kujiengua na kuwaachia nafasi hizo, watahakikisha wanapiga kampeni zao wenyewe kuhakikisha wanapata ushindi wa kishindo, kutokana na kudai wao ndio wanaokubalika.

Akizungumza wakati akihutubia wananchi, Mbatia ambaye pia ni Makamu Mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema madiwani walipewa maelekezo na makao makuu ya vyama vyao kwa maandishi, yakieleza kuangalia vigezo vya nani anayekubalika, mtandao wa mtu, uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulivyokuwa mwaka jana, na sio kila mtu kulalamikia kuwa yeye ndiye anayefaa.

Mbatia alitumia mkutano huo, kuwataka wabunge wote nchini kupitia Ukawa, kuheshimu makubaliano ya kile walichosaini kwa kutekeleza, na sio kila mgombea wa kila chama kung’ang’ania yeye wakati makubaliano yapo.

Alisema anashangazwa kuletewa malalamiko ya madiwani wakati tayari alikwishaongea na Katibu wa Chadema na kumweleza watumie busara kwa kuamua matatizo hayo, ambapo alibainisha hadi sasa wameshindwa kusuluhisha mgongano huo ina maana pia wameshindwa uongozi.

Kutokana na mpasuko huo, Mbatia bila kumtaja mgombea na chama, alisema hawezi kumnadi mgombea anayechana mabango yake kamwe. Aliwataka wananchi kuwapima madiwani wanaotaka kuchaguliwa ni vyema wakaangalia sifa za uwezo, kiongozi mkweli kwa maneno na matendo, kiongozi anayechukia uonevu na vitendo vya dhuluma katika jamii.

“Makubaliano tulishasaini na wagombea wote wanayajua kupitia vyama vyao, sasa kila mmoja anasema yeye ndiye anayekubalika….tuheshimu makubaliano yaliyowekwa na Ukawa, lakini mimi bila ushabiki sitamnadi mgombea anayechana mabango yangu…hata kidogo,” alisema Mbatia.

Wakati madiwani wa Chadema wakitengwa kwenye mkutano huo, awali Mbatia alipokewa na wananchi waliobeba mabango yaliyoandikwa “Hatuwataki madiwani wa NCCR-Mageuzi, tunamtaka Mbatia pekee.”

Kumekuwa na kutoelewana kati ya wagombea wa vyama vinne vya Ukawa - Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD kuhusu kuachiana kata na hata majimbo, kiasi kwamba licha ya makubaliano ya wakuu wa vyama hivyo, wapo wagombea waliogoma kutii maagizo hayo na sasa wamesimama kutetea nafasi walizoomba.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: