Makala hii ni tamu kundelea kuisoma hadi mwisho upate uhondo wake.Mtoto aliachwa pekee nyumbani. Jikoni alikuwa ameachiwa chakula cha kutosha, asusa, soda na juisi. Ghafla akajipa cheo cha baba mwenye nyumba.
Akawaalika watoto wenzie ili wafanye sherehe ndogo ya kumpongeza kwa kuukaimu u-baba. Watoto nao waliposikia mwaliko huo hawakuwa na simile, dakika hiyohiyo walijaa sebuleni.
Kamati ya chakula na vinywaji ikaingia jikoni. Dogo akawasha TV na punde wakawa wakicheka pamoja na katuni: Tom na Jerry. Kinywaji kiliendelea:
soda, juisi na maji. Lakini watoto ni watoto tu; wakakumbuka baba zao hunywa mvinyo kwenye hafla kama hizo. Likatolewa na kupitishwa wazo la kujaribu mvinyo kidogo.
Mambo yaliendelea na vicheko kuongezeka. Haikuchukua muda watoto wote wakawa walevi. Wakakumbuka kuwa mvinyo huenda pamoja na asusa nyepesi kama kuku wa kuchoma.
Bandani kulikuwa na koo mmoja aliyetamia, akakamatwa na kuchinjwa bila utaratibu wa kibla. Akaingizwa motoni na punde watoto walikunywa huku wakimgegeda kuku yule maskini.
Chakula kililetwa, kila mmoja alijipakulia kwa nafasi yake. Lakini baba mwenye nyumba aliwaka baada ya kuona menyu haina kuku. Kamati ilijibu kuwa kuku pekee aliyekuwapo nyumbani alishafanywa asusa. Mlevi (oh sorry), mtoto mmoja akatoa wazo: “Kuku hupatikana kwenye yai; tuwatafute kwenye mayai ili kila mmoja ale wa kwake.” Baba na jopo lake walikwenda kwenye banda.
Basi kazi ya kumtafuta kuku kwenye yai ikaanza. Liliokotwa yai, likatingishwa sikioni kama nazi na kuvunjwa. Kilichoonekana ni ute na kiini tu. Likachukuliwa lingine na kutendwa sawasawa na lile la kwanza. Mayai yakaisha bila kuku kupatikana.
Wazazi waliporudi walishuhudia uharibifu mkubwa. Ni bora banda lingekuwa tupu, lakini lilitawanywa mabaki ya mayai yaliyovunjwa. Mtoto aliingia lawamani na kubeba adhabu kubwa kwa niaba ya wenzie waliokwesha kusepa. Alifundwa kuwa ukikata mti kamwe huwezi kuokota matunda.
Asilimia kubwa ya binadamu wanaishi kwenye nyumba. Wapo wengine wanaoishi kwenye mapango na wengine misituni. Nyumba hujengwa kulingana na mahitaji ya mtu anayetaka kuishi humo.
Kwa kuwa anahitaji hewa safi, huacha matundu anayoyaita madirisha ili hewa hiyo iingie kwa wingi. Pia hujenga dohani ili kutoa hewa taka inayotoka jikoni. Huweka mabomba yatakayoingiza majisafi na mengine yatakayotoa maji taka.
Dunia iliumbwa kwa mtindo huo. Iliumbwa mimea kuwa chanzo cha hewa na majisafi, lakini mimea hiyohiyo ikapewa jukumu la kuondoa taka na hewa chafu.
Inakula uchafu a.k.a. mbolea, inavuta hewa chafu a.k.a. kaboni daioksaidi na kupumua hewa safi a.k.a. oksijeni. Mimea hiyo hutoa umande unaovutwa angani na jua kuzalishwa mvua. Sijawahi kusikia mvua ya kinyesi ikinya duniani.
Mungu alimuumba binadamu wa kwanza na kumweka bustanini. Leo tungelikuwa na hadithi nyingine kama binadamu huyu aliyeumbwa kwa tope la ardhi angewekwa kwenye tope. Lakini alitunzwa bustanini kwenye hewa safi na kuagizwa aitunze dunia.
Kwa imani yangu ndogo kabisa, hiyo ndiyo ibada kuu na muhimu zaidi kwa binadamu. Hainiingii akilini ninapoona binadamu akifunga, kukesha na kupiga kelele za kumtukuza Mungu huku aking’oa miti na kuzalisha sumu inayoharibu mazingira alioamriwa kuyatunza.
Kwa mara ya kwanza Dunia imeshuhudia jaribio la kwanza la Idara ya Anga Marekani (Nasa) kulipua sehemu ya mwezi. Wanasema kuwa wanahisi yapo maji kwa kiwango kikubwa kwenye ardhi ya mwezi.
Kwao ni maendeleo makubwa kisayansi na kwamba yanaweza kuwa masaada mkubwa kwa dunia inayokabiliwa na uchakavu wa kutisha kwa kukosekana kwa maji na hewa safi.
Kwangu hii ni dhambi kubwa zaidi ya mauaji. Wakati Farao alipoamuru ujengwe mnara ili aende kuonana ng’adu kwa ng’adu na Mwenyezi Mungu, yeye pamoja na wengi waliona alikuwa sahihi.
Hawakuweza kusikiliza maagizo na kutawaliwa kiimla pasipo demokrasia. Lakini wengi ukijumlisha na wachache ni sawa na wengi, Mungu hakutaka wengi waangamie kwa kosa la mmoja. Akalisimamisha zoezi zima.
Binadamu wa sasa anafanana na mtoto aliyewaacha wazazi. Hana adabu kwa chochote kilicho mbele yake, na anafanya vyovyote anavyoona sawa.
Adam hakuwa na wazazi lakini alikuwa chini ya usimamizi thabiti wa muumba wake. Ninaamini kama angelifanya kazi ya kuharibu kila alichokikuta, sisi tusingelikuwapo. Lakini pia Mwenyezi Mungu asingalimuachia kwa sababu alimtunza ili sisi tuwepo.
Mungu alitoa adhabu kila alipoona dhambi zikikithiri. Kumbuka gharika kuu, moto wa Sodoma na Gomora na mengi yaliyowakumba mafarao wa Misri.
Lakini baada kuona binadamu akizidiwa na tamaa kwa kila kipya kwake, akasema “Sitamuadabisha kwa maji wala moto, ila atajiadabisha kwa tamaa zake”.
Ndipo tunapotamani kung’oa misitu yote ili tujenge maghorofa ya kibiashara. Maji yanapokosa chanzo tunaenda kuukoboa mwezi! Sasa tunatamani kuhamisha dhahabu yote ya Kongo na gesi yote ya Mtwara.
Kweli ngurumbili amekosa akili. Mimi mlevi ninaona, werevu wana macho lakini hawaoni?MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment