CUF wanadai kuwa Maalim Seif alikuwa akihutubia kwenye mkutano huo uliofanyika Jimbo la Mpendae, ghafla wakaibuka vijana wanaodhaniwa kuwa wa CCM waliokuwa kwenye gari maalumu la matangazo na lililokuwa likipiga muziki kwa sauti ya juu.
Gari hilo lilisababisha kuingiliana ka sauti na hivyo hotuba ya Maalim Seif kutosikika vizuri na kumlazimisha makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kuikatisha na kushuka jukwaani.
CUF, ambayo ina upinzani mkali na CCM kwenye siasa za Zanzibar, imesema kitendo hicho ni cha uchokozi ambacho siyo tu kilizua tafrani kubwa, bali pia kiliashiria kutishia usalama wa umati wa watu waliohudhuria mkutano huo.
Ismail Jussa Ladhu, Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa CUF, alisema kilichosaidia kunusuru hali ya hewa kuchafuka ni hekima na busara za Maalim Seif aliyeamua kukatisha hotuba yake na kuteremka jukwaani na hivyo kuuvunja mkutano huo kabla ya muda wake.
“Tunachosema ni kwamba mkutano wetu ulivunjika kabla ya muda kuepusha shari iliyokuwa ikitafutwa na CCM kwa makusudi vinginevyo mambo yangeharibika,” alisema Jussa ambaye pia anagombea uwakilishi wa Jimbo la Malindi, Unguja kwa tiketi ya CUF.
“Tumesikitishwa na kitendo cha polisi kutumia gari mbili za ulinzi mbele na nyuma ya gari hiyo ya matangazo ya CCM wakati kilichotendeka ni uchokozi wa makusudi.”
Nassor Ahmed Mazrui, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Meneja wa Kampeni wa Maalim Seif, alisema walitegemea polisi kutekeleza wajibu wao wa kusimamia amani na utulivu kwenye maeneo ya mikutano ya kampeni na kuwazuia vijana hao wa CCM kupita eneo hilo, badala yake waliwapa ulinzi na kuendesha hujuma na uchokozi huo.
“CUF tunasema tumesikitishwa na hatua ya Polisi kwa sababu Kamishna Hamdani Omar Makame ndiye aliyeitisha kikao na vyama vya CUF na CCM siku ya Ijumaa, Agosti 28, 2015 Ziwani yalipo makao makuu yao na kuzungumza namna bora ya kushirikiana ili kuepusha vitendo vya vurugu na fujo na kuhakikisha tunaendesha kampeni na harakati nyengine za uchaguzi kistaarabu kwa salama na amani,” alisema kiongozi huyo.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Omar Makame alithibitisha kupokea malalamiko ya CUF na kwamba jeshi lake, litaendelea kuwalinda wananchi kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Akizungumzia sakata hilo Ofisa Habari wa CCM Zanzibar, Ali Ndota alisema hana taarifa za tukio hilo, lakini atakapopata taarifa atalifuatilia na kuchukua hatua zinazostahili.
Kwa upande wake Ofisa Habari wa ZEC, Salha Mohammed, alisema bado hawajapata barua rasmi ya malalamiko hayo, wakipata watatoa taarifa.MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment