BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SHIRIKA LA TANESCO LALALAMIKIWA KWA KUTANGAZA GIZA KINYEMELA

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchesm Mramba.

Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), limeingia lawamani kutokana na usumbufu na hasara kubwa wanayowasababishia watumiaji wa nishati hiyo kufuatia tangazo lao la 'ghafla' kuwa sehemu kubwa ya nchi itakuwa gizani kuanzia jana.

Tanesco ilitoa tangazo hilo kwa kile ilichokieleza kuwa ni kutaka kuanza kujaribu mitambo ya kufua umeme wa gesi iliyopo Kinyerezi jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), Dk. Samwel Nyantahe, ameitupia lawama Tanesco kutokana na kuitangazia nchi kuingia ‘gizani’ kwa wiki nzima kuanzia jana pasipo kutoa taarifa mapema ili wananchi wajiandae kukabiliaana na hali hiyo.

Akizungumza na Nipashe jana, Dk. Nyantahe, alisema kabla ya Tanesco kufikia hatua hiyo ilipaswa kutoa 'notsi' hata ya wiki moja ili watu wajiandae.

“Sisi wenyewe tumeshtuka kusikia kwamba kutakuwa na shida ya umeme wiki nzima, ninashindwa kufahamu ni jambo gani ambalo Tanesco hawakujua mpaka wanatoa taarifa za ghafla za kukatika kwa umeme wiki nzima pasipo kuwaandaa watu waweke mambo yao sawa,” alihoji Dk. Nyantahe.

Aliongeza: “ Wangetoa notsi, ingekuwa rahisi watu kujiandaa kwa kuweka vitu vyao sawa, kama ni wenye kutafuta majenereta watafute ili mambo mengine yaendelee hasa kwa wafanyabiashara.”

Alisema Tanesco kufanya hivyo, kunarudisha nyuma uzalishaji na kwamba kama ulikuwa unapanda ni lazima utashuka na huku ukichangia kuongezeka kwa gharama za uzalishaji.

“Hii ni kuyumbisha uzalishaji kwa nchi, yaani unapoanza kupanda, unaporomoka tena kutokana na sababu ambazo zingeweza kuzuilika,” alisema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini, Johnson Minja, alisema Tanesco kukatakata umeme kutawaathiri kwa kiwango kikubwa kwa kuwa shughuli zao zinaendeshwa kwa kutegemea nishati hiyo.

Alisema wiki nzima ni kubwa kwa wafanyabiashara, hivyo kuna baadhi ya mambo yatasimama kwa muda.
Mbali na hilo, pia alisema gharama za uzalishaji zitaongezeka na kwamba ni lazima walaji nao wataumia kwa sababu bidhaa zitapanda.

“Kabla ya kufanya mambo yote haya, ni bora wangekuwa wanatoa taarifa mapema, kukata umeme bila taarifa kunatuathiri. Sasa itabidi bei za bidhaa zipande kwa sababu gharama za uzalishaji nazo zitaongezeka na hii ni kuumiza wananchi,” alisema.

Minja alisema ni bora Tanesco wangepanga ratiba zao vizuri ili angalau umeme upatikane mchana kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara kuzalisha.

Msemaji wa Tanesco, Adrian Severin, alipotakiwa kuweka bayana ratiba ya kukatika kwa umeme huo, alisema umeme huo hautakatika saa 24, huku akishindwa kuweka wazi ratiba ya kukatika itakavyokuwa.

"Umeme hautakatika kwa kila mkoa ila kutakuwa na kukatikakatika kwa baadhi ya maeneo kwenye mikoa iliyounganishwa kwenye gridi ya taifa na siyo kwa saa 24 kwa sababu kuzimwa kwa mitambo ya kufua umeme kwa gesi iliyopo ubungo bado kuna mitambo mingine itaendelea kufua umeme kwa maji na mafuta," alisema.

Tanesco ilitangaza kutakuwa na kukatika kwa umeme huo kwa wiki moja kwenye mikoa iliyoungwa kwenye grid ya taifa kutokana na kuzimwa kwa mitambo ya gesi inayozalisha umeme kutoka Songosongo na kuanza majaribio ya gesi ya Mtwara.

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchesm Mramba, juzi aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa baada ya kuanza kuzalishwa kwa umeme wa gesi kutoka Mtwara, Watanzania watapata umeme wa uhakika.

Alisema tayari gesi imeanza kuingia kwenye mtambo wa Kinyerezi I na Ubungo II na kwamba kinachofanyika sasa ni majaribio ya kusukuma mitambo ya Ubungo II na Symbion kwa ajili ya uzalishaji, hivyo kuunganishwa kwa bomba hilo kutaihakikishia nchi kuwa na umeme wa uhakika hata kama mabwawa ya maji yanayotumiwa kuzalisha umeme yatakuwa yamekauka.

Alisema hadi mwishonimwa wiki mafundi walikuwa wameunganisha bomba la gesi kutoka Mtwara na Kituo namba 15 Ubungo tayari kwa kuanza uzalishaji.

Kwa mujibu wa Mramba, mikoa itakayoathirika ni yote inayopata umeme wa Gridi ya Taifa ukiwamo Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Dodoma, Morogoro, Singida, Mwanza, Mara, Mbeya, Iringa, Tabora, Shinyanga, Manyara na Zanzibar. CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: