BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WATU WA HOVYO, WEZI NA WANAFIKIRI KIAMA CHAO KIMEFIKA, NI DK MAGUFULI KUPEWA JUKUMU ZITO LA KUISAFISHA CCM NA SERIKALI YAKE BAADA YA....!


Katibu mkuu Taifa CCM Abdulrahman Kinana, akihutubia kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za ubunge Jimbo la Moshi mjini uliofanyika kwenye uwanja wa mashujaa Manispaa hiyo jana. Picha na Dionis Nyato


Moshi.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amesema ndani ya CCM wapo watu wa hovyo, wezi na wanafiki, lakini kama watamchagua Dk John Magufuli kuwa rais, ataisafisha CCM na Serikali yake. 


“CCM tumejitahidi kuleta maendeleo, lakini lazima nikiri ndani ya CCM kuna kasoro. Tuna mijitu hovyo, tuna wezi, tuna majambazi humo na kuna watu wanafiki ndani ya CCM,” alisema Kinana.

Kinana alitoa kauli hiyo jana mjini Moshi katika mkutano mkubwa wa hadhara wa kuzindua kampeni za ubunge katika Jimbo hilo, ambapo Davis Mosha anapeperusha bendera ya CCM.

“Magufuli atakisafisha chama akiwa mwenyekiti... si mjumbe, lakini anakijua chama.... CCM kuna majungu na ulaji, lakini Magufuli atayamaliza, hajatumia fedha kupata urais, hajaenda wilayani ama mikoani bali alienda matawini.

“Hana makundi... wapo waliochangisha fedha wamekusanya watu baadaye wanakuja kuwa mzigo. Yeye hana makundi wala hana mzigo,” alisema Kinana.

Alisema kuna watu wamefanya uozo ndani ya Serikali na ndani ya CCM na kuamua kukimbia na huko waliko wanasema wataleta mabadiliko wakati wameshindwa kufanya lolote wakiwa madarakani.

Kinana alitoa mfano wa Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ambaye amekuwa Waziri Mkuu miaka kumi, ameshindwa kufanya kitu na kwamba sasa anakuja kuahidi maajabu.

Hata hivyo katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wanachama wa CCM na wananchi, Kinana aliwaomba wamchague Dk Magufuli kwani ndiye anayeweza kubadili mfumo huo.

“Suala hapa ni mfumo. Mkipata mtu mmoja tu mzalendo kama Dk Magufuli atabadili kabisa mfumo huu. Nataka niwahakikishie kuwa Magufuli akiingia madarakani atasafisha CCM na Serikali,”alisema.

Kinana aliwataka Watanzania kutohadaika na ahadi za mabadiliko zinazotolewa na wale aliowaita “makapi” kutoka CCM ambao walishiriki kuharibu mfumo mzuri wa CCM na sasa wamekimbia.

“Halafu watu walioharibu CCM, hawa makapi hawa wanakuja Chadema, wanawapa matumaini na wengine walikuwa mawaziri kwa miaka 40 kwanini hawakufanya hayo wanayoyasema?” Alihoji Kinana.

Kinana alisema endapo wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro na nchi kwa ujumla, watampa kura Magufuli, ataunda baraza dogo la mawaziri lenye tija na litakalowajibika kwa wananchi.

Katibu mkuu huyo aliwatahadharisha Watanzania kufanya mabadiliko kwa chuki na hasira akiwataka warejee mifano ya nchi za Libya, Misri na Zambia ambapo mabadiliko hayajawasaidia sana.

Alitumia mkutano huo kumshambulia Waziri Mkuu mstaafu, Sumaye, akisema katika miaka 10 aliyokuwa madarakani kama Waziri Mkuu, hakuna kitu Watanzania wanachomkumbuka nacho.

“Sumaye amekuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 niambieni kitu kimoja tu mnachomkumbuka nacho. Sokoine (Edward) mbona anakumbukwa kwa uchapakazi na ukali katika kuendesha Serikali?” Alihoji.

Kinana alisema endapo Sumaye atapanda jukwaani mjini Moshi, wananchi wamuulize maswali 100 kwamba chini ya utawala wake amefanya nini hadi leo amuombee mtu kuwa rais.

Kwa upande wao, mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na Livingstone Lusinde wa Mtera, waliwataka wananchi wa Jimbo la Moshi kutochagua viongozi kwa ushabiki wa kisiasa.

Akizungumza katika mkutano huo Sendeka alisema ni lazima Watanzania wawapime wagombea kwa kujua ukweli si kwa kudanganyana na amewaasa kuepuka dhambi ya ubaguzi wa aina yoyote ile.

Kwa upande wake Lusinde alisema siasa zisigeuzwe kama ushabiki wa mpira kwani ni kucheza na maisha ya mamilioni ya Watanzania.

“Leo hii Askofu akibadili dini na kuwa Muislamu anaweza kukabidhiwa nafasi ya kuwa Mufti?” Alihoji Lusinde na kujibiwa “hapana” na wana-CCM walioshiriki mkutano huo katika uwanja wa Mashujaa mjini Moshi.CHANZO:MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: