BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HAKUNA NAMNA ! WAZIRI MKUU AWAOGOPESHA WATENDAJI KUWA ATAYEBAINIKA KUTUMIA VIBAYA FEDHA ZA SERIKALI HAKUNA CHA MSWALIE MTUME BALI KUNG'OLEWA TU KAZINI.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya watendaji wa halmashauri nchini, kwamba atakayebainika ametumia vibaya fedha za Serikali atang’olewa kazini kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano haina mchezo na mtu.

Alitoa kauli hiyo jana mchana wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Ilulu uliopo Lindi mjini.

“Natoa onyo kwa watendaji wote wa halmashauri. Fedha ya Serikali itakayotumwa kwenu halafu mtu aifanyie ubadhirifu, ole wake. Yeyote atakayebainika kuzitumia kwa ubadhirifu fedha hizi tutamng’oa. Wako wasomi wengi huko nje tena wazuri tu, wanasubiri kupata ajira.

“Nataka watumishi wa umma watambue kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inajielekeza kujali wananchi. Wao wana dhamana ya kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi ili kuhakikisha wanatatua kero zinazowakabili,” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa na wengine wakisema huyu sasa ni Sokoine wa pili.

Edward Sokoine alikuwa ni Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere. 


Waziri Mkuu ambaye aliwasili Lindi jana, aliwaeleza wakazi hao kwamba amekuja kuwashukuru wazee na wana Lindi kwa dua zao na kuwaahidi kwamba hatawaangusha Rais John Magufuli na Makamu wake Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kuwatumikia Watanzania katika ngazi ya Uwaziri Mkuu.

Waziri Mkuu pia alimpa kazi Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Jordan Rugimbana ya kuhakikisha anaufufua uwanja huo na kuurudisha kwenye enzi yake ulivyokuwa maarufu katika mikoa yote ya Kusini.

“Uwanja huu lazima uboreshwe kwa sababu unanikumbusha mwaka 1984 wakati nachezea timu ya Hamli Rangers. Kulikuwa na ukoka wa nguvu hapa uwanjani. 


Kwa hiyo timu aliyoiunda Mkuu wa Mkoa itafanya kazi, lakini pia iwajumuishe Meya na Mbunge wa Lindi Mjini kwa sababu huu uwanja ni mali ya Halmashauri ya Lindi,” alisema Waziri Mkuu ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ruangwa katika mkoa huu wa Lindi.

Akielezea kuhusu mipango ya Serikali kuendeleza sekta ya viwanda, Waziri Mkuu alisema hivi karibuni mkoa huo utapata wawekezaji kwenye sekta ya gesi baada ya Kampuni ya BG kutoka Uingereza kupata umiliki wa eneo la Kikwetu ili wajenge mitambo ya kusafisha gesi.

Aliwataka wananchi wa mkoa huo wawekeze kwenye ujenzi wa hoteli na nyumba za kulala wageni ili ifikapo Agosti mwakani, watu wanaokuja kushiriki Maonesho ya Nanenane kitaifa mkoani humo wasipate taabu ya malazi kama ambavyo imekuwa ikitokea huko nyuma.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: