Picha ya maktaba: ikionyesha ajali ya pikipiki.Jeshi la Polisi nchini limetoa tahadhari kadhaa zikiwamo tano muhimu zinazopaswa kuzingatiwa na kila Mtanzania katika mfululizo wa Sikukuu za Maulid, Krismasi na Mwaka Mpya ili kujihakikishia usalama wao na mali zao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba, alisema jeshi lao linawatakia Watanzania wote kheri ya sikukuu za Maulid, Krismasi na Mwaka Mpya.
Huku likiwataka Watanzania kuzingatia tahadhari hizo katika mfululizo wa mapumziko ya sikukuu yanayoanza leo kwa kusherehekea Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) na kesho kufurahia siku ya Krismasi aliyozaliwa Yesu Kristo.
Bulimba aliyataja maeneo hayo muhimu ya kuzingatia katika kipindi hiki cha sikukuu kuwa ni kuendesha magari kwa kasi inayozingatia usalama; kutojaza abiria kwenye magari kupita kiasi, kuepuka mrundikano kwenye kumbi za starehe, kutowaacha watoto bila ungalizi, bodaboda kuendeshwa kwa staha na pia watu kuepuka kulewa kupita kiasi.
KUJAZA ABIRIA
Akizungumzia jambo hilo, Bulimba alisema ni marufuku kwa wenye magari, hasa wa mabasi yanayotoa usafiri wa daladala, kujaza abiria kupita uwezo wa magari yao kwani jambo hilo ni hatari kwa usalama wa raia na mali zao.
“Kila mmoja azingatie jambo hili. Kwa yeyote atakayekiuka, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” alisema Bulimba, akiongeza kuwa operesheni ya kukamata magari yanayojaza abiria kupita kiasi ni endelevu na hivyo itakuwapo mara zote hata baada ya sikukuu.
MRUNDIKANO KUMBI ZA STAREHE
Bulimba alisema mojawapo ya maeneo ambayo husababisha madhara makubwa kwa watu wakati wa sikukuu, hasa watoto, ni pamoja na mrundikano mkubwa wa watu unaozidi uwezo wa kumbi za starehe.
Bulimba aliwataka wote wenye kumbi za starehe kudhibiti idadi ya watu watu watakaoingia kulingana na uwezo wa kumbi zao ili kuepuka mkanyagano na matukio mengine yanayohatarisha usalama wa watumiaji.
KULEWA KUPITA KIASI
Tahadhari nyingine muhimu katika kipindi hiki cha mfululizo wa sikukuu ni kila mmoja kuepuka unywaji wa pombe kupita kiasi. Hili ni angalizo muhimu kwani kuna matukio mengi ya ajali husababishwa na ulevi kupindukia, hasa katika siku za sikukuu.
UENDESHAJI BODABODA KWA FUJO
Eneo jingine lililozungumziwa na Bulimba ni lile la uendeshaji wa pikipiki maarufu kama bodaboda, pasi na kuzingatia sheria.
Uendeshaji huu wa hatari katika siku za sikukuu huhusisha pia kupakia abiria wengi kwa wakati mmoja kwa mtindo maarufu wa ‘mishikaki’ na pia kuendesha kwa kasi kubwa bila kuzingatia usalama.
Alisema dereva wa bodaboda atakayebainika kukiuka sheria atakamatwa yeye pamoja na abiria wake na wote watawekwa rumande kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria.
KUACHA WATOTO BILA UANGALIZI
Kwa mujibu wa Bulimba, eneo jingine la kuzingatia katika kipindi hiki cha sikukuu ni kuhakikisha kuwa watoto wanaangaliwa vyema wakati wote na kamwe wasiachwe bila uangalizi.
Hili ni muhimu kuzingatia, hasa kwenye maeneo ya fukwe kama ‘Coco Beach’ jijini Dar es Salam, ili kuwaepusha na hatari zinazoweza kuepukika pindi wazazi au walezi wanapowahakikishia uangalizi katika matembezi yao.
RAI YA POLISI
Bulimba aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi kwa kutoa taarifa mara moja pale wanapobaini viashiria vya uhalifu, huku akiongeza kuwa jeshi lao limejipanga vya kutosha kuhakikisha kuwa ulinzi unaimarishwa katika maeneo ya mikusanyiko ikiwamo kwenye fukwe na pia kwenye nyumba za kuabudia.
Kadhalika, alitaka wamiliki wa hoteli na masoko makubwa kuweka vifaa vitakavyokuwa vinafuatilia mienendo ya wateja wao.CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment