Dar es Salaam. Wakala wa Ukaguzi wa Madini nchini (TMAA) imetaifisha madini aina ya Tanzanite yenye thamani ya Sh2.5 bilioni yaliyokamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wakati yakisafirishwa kwenda nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alisema madini hayo yenye uzito wa gramu 2,871 yalikamatwa Desemba 15, wakati Jain Anarungi, raia wa India alipojaribu kuyatorosha kwenda nje ya nchi kinyume cha sheria.
“Madini yana thamani ya Sh 2.5 bilioni na tumeyataifisha kwa mujibu wa kifungu namba 6(4) cha sheria ya madini ya mwaka 2010, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2015 ” alisema Dk Kalemani.
Alisema katika kipindi cha kuanzia Julai 2012 hadi Novemba 2015, ukaguzi wa madini uliofanywa katika viwanja vya ndege kwa kushirikiana na vyombo vingine vya udhibiti, umebaini madini aina hiyo, dhahabu, fedha na madini mengine ya vito yenye uzito wa kilo 2,871 yenye thamani ya Sh16.4 bilioni katika matukio 87.
“Kuanzia Julai 2012 hadi Desemba mwaka huu thamani ya madini yaliyotoroshwa kwenda nje ya nchi kupitia viwanja vya ndege ni Sh 18.9 bilioni,” aliongeza.
Dk Kalemani alisema sekta ya madini nchini inachangia asilimia 3.5 ya uchumi na kwamba hadi kufikia mwaka 2025, uchumi wa sekta hiyo utakua kwa asilimia 10.
Katika hatua nyingine, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limewasimamisha kazi watumishi wake 10 kwa kusababisha upotevu wa mapato katika mfumo wa mita kwenye minara ya simu.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba alisema jana kuwa watumishi hao, ambao ni mafundi na wahasibu, walisababisha hasara ya Sh100.2 milioni kutokana na uzembe, kujihusisha na rushwa na ukiukwaji wa maadili.
Uamuzi huo unafanyika ikiwa ni mara ya pili kwa uongozi wa shirika hilo baada ya Desemba 6, mwaka huu kuwafukuza kazi maofisa wake saba, ambao ni wahasibu, wahandisi na mameneja, kwa tuhuma za wizi na ubadhirifu.
Akifafanua kuhusu uamuzi huo, Mhandisi Mramba alisema kwa muda mrefu shirika limekuwa likifuatilia maadili ya wafanyakazi wake ili kuhakikisha wanashughulikia kero mbalimbali za wateja.
Alisema shirika litaendelea kuwachukulia hatua za kinidhamu wafanyakazi wote wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili, uzembe, rushwa na ubadhirifu.
“Hawa si watu wadogo kwa hivyo tumewasimamisha na wakati huo uchunguzi unaendelea na ukikamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisema.
Mhandisi Mramba alisema kuhusu agizo la kujisalimisha kwa wateja wote wanaodaiwa madeni au kuwa na matatizo katika mita zao, shirika hilo limewachukulia hatua wateja nane wakiwamo watu binafsi na taasisi walikamatwa kutokana na kujihusisha na mtandao wa wizi wa umeme.
Tanesco ilitoa agizo kwa wateja wake wenye matatizo katika mashine zao za luku wajisalimishe katika ofisi hizo ndani ya siku saba ambapo ni wateja 30 walikuwa wamejisalimisha.
Mhandisi Mramba alisema kutokana na kupuuzwa kwa agizo hilo walifanya oparesheni iliyokagua wateja 2,156 na kunasa wateja 138 waliopigwa faini ya Sh198 milioni.
“Wateja 37 tumewafikisha mbele ya vyombo vya sheria lakini miongoni mwa wateja hao ni msanii wa filamu za Bongo Movie, Wema Sepetu na diwani wa Chadema wa Kata ya Sinza C, Joseph Marandu.
Tunatoa onyo kwa wateja wote nchi nzima kuhakikisha wanajiondoa kwenye mtandao wa wizi wa umeme,” alisema. Awaipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Wema na diwani huyo wa Sinza hawakupatikana.MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment