Dar es Salaam. Jumla ya watoto 79 wamezaliwa katika mkesha wa Sikukuu ya Krismasi katika hospitali za rufaa za mkoa wa Dar es Salaam.
Kati ya idadi hiyo, watoto wawili wamezaliwa njiti katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hali zao zinaendelea vizuri.
Afisa Muuguzi Msaidizi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mwanne Yusuph alisema wanawake waliojifungua usiku wa mkesha wa Krismasi walikuwa 12 na kati ya hao, 10 walifanyiwa upasuaji.
Alisema kati ya watoto 13 waliozaliwa Hospitali ya Muhimbili, watoto wawili walikuwa njiti na hali zao zinaendelea vizuri.
"Kati ya watoto 13 waliozaliwa katika mkesha wa sikukuu yĆ Krismasi wanaume ni sita na wanawake saba na wote wanaendelea vizuri hakuna aliyepoteza maisha," alisema Yusuph.
Kwa upande wa Hospitali ya Temeke watoto waliozaliwa ni 12 ambapo kati yao wanawake ni nane na wanaume wanne.
Afisa muuguzi kiongozi kutoka Hospitali ya Temeke, Dk Rashidi Nyombiage amesema kati ya wanawake 12 waliojifungua, wawili walifanyiwa upasuaji.
"Wote waliojifungua wanaendelea vizuri pamoja na watoto wao na mpaka sasa hatujapata changamoto yoyote iliyojitokeza katika hospitali yangu," amesema Dk Nyombiage.
Kwa upande wa Hospitali ya Amana iliyoko wilaya ya Ilala, jumla ya watoto 33 wamezaliwa kati ya watoto wanaume ni 18 na wanawake ni 15.
Afisa Muuguzi Kiongozi kutoka hospitali ya Amana, Florence Ndumbaro amesema changamoto kubwa wanayoipata ni kwamba idadi ya wanawake wanaokwenda katika hospitali hiyo kujifungua wakitokea wilaya nyingine.
“Sisi tunazalisha wanawake kutoka wilaya nyingine tofauti na Ilala na hili linatupa changamoto kutoka na mahitaji kuwa makubwa kuliko uwezo wetu wa kuhudumua" alisema Ndumbaro.
Naye Ofisa Muuguzi Kiongozi wa zamu kutoka Hospitali ya Mwananyamala, Halima Mbano alisema Jumla ya watoto 21 wamezaliwa katika mkesha huo.
Mbano alisema watoto watano kati ya hao walizaliwa kwa njia ya upasuaji na watoto 16 walizaliwa kwa njia ya kawaida. "Kati ya watoto hao wanawake ni 15 na wanaume ni sita na wote wanaendelea vizuri," alisema Mbano.MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment