Dar/Mikoani. Kuombea kudumishwa amani, kumwombea Rais John Magufuli katika kutimiza majukumu yake, pamoja na utatuzi wa suala la kisiasa Zanzibar ni mambo ambayo yalitawala mahubiri ya mkesha na ibada za sikukuu ya Krismasi katika maeneo mbalimbali nchini. Maaskofu, wachungaji na mapadri wa makanisa mbalimbali, waliendesha ibada ya sikukuu hiyo na walitumia muda mwingi kuhimiza amani pamoja na kuiombea Serikali katika mapambano dhidi ya ufisadi na uhujumu uchumi.
Serikali ya JPM
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo alisema Watanzania wanyonge na maskini, hawatakiwi kuogopa kuonyesha uwezo wao kwa kuwa sasa wana nguvu kubwa ya kuleta mabadiliko kwa jamii kuliko matajiri.
Akitoa mafundisho katika mkesha wa Krismasi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph juzi usiku, Kadinali Pengo alisema zama za kusadikishwa kwamba matajiri pekee ndiyo wenye uwezo wa mkubwa wa kuongoza na kuleta mabadiliko ya kidini, kisiasa na uchumi, zimekwisha.
Kadinali Pengo aliyetumia ujumbe wa Krismasi wa ‘msiogope’ katika mahubiri yake, alisema waumini wa Kikristo na Taifa, hawatakiwi kujenga hofu wakati huu wa habari njema kwa watu dhaifu, wanyonge na maskini ambayo itawafanya wasijisikie watu duni tena.
“Katika siasa na mabadiliko, watu wa kawaida tumesadikishwa kuwa hatuwezi kutoa msaada mbele za watu.
Tulisadikishwa wale wenye fedha pekee wanaweza kuleta mabadiliko, lakini sasa wale wasio na nafasi ndiyo wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha hali ya binadamu inakuwa nzuri,” alisema Pengo aliyekuwa akihubiri huku amekaa.
Alisema hata katika maandiko ya Biblia, malaika aliwatokea watu na wachungaji waliotakiwa kuwa wanyonge na duni mbele ya wanadamu na Mungu na kuwaambia “msiogope” kwa kuwa aliwapelekea habari njema ya kuzaliwa masiha Yesu Kristo ambaye ndiyo mkombozi wao.
Hata hivyo, Kadinali Pengo katika mahubiri yake ya dakika 12, hakutoa mifano ya moja kawa moja inayohusiana na michakato ya kisiasa na mabadiliko nchini ambayo amesema kwa sasa imeanza kuonyesha watu duni na maskini wameanza kuonyesha kutatua matatizo ya jamii kwa kujituma kufanya kazi usiku na mchana.
Akizungumzia Serikali ya Awamu ya Tano, Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa alisema: “Kuna jambo limeanza kuonekana.
Tunaanza kuona uamuzi na maelekezo yanayoweza kulifanya Taifa hili kuheshimika. Kazi yetu viongozi wa dini ni kuiombea nchi ili viongozi wasikate tamaa na wasimame imara maana kuna mamilioni ya watu nyuma yao.”
Askofu wa Kanisa la KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dk Abednego Keshomshahara ametaka kila mwananchi kutafakari wajibu wake katika juhudi za kumuunga mkono Rais Magufuli.
Katika mahubiri ya Kanisa Kuu mjini Bukoba, Askofu huyo alisema kila mwananchi ana wajibu kufanikisha vita dhidi ya umaskini.
Alisema waumini pamoja na wananchi wote wanatakiwa kuunga mkono kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi tu’ na kwamba kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu pia inagusa maisha ya kimwili.
Pia Dk Keshomshahara ambaye amewekwa wakfu miezi miwili iliyopita, aliwataka waumini kupiga vita uzembe na ubadhirifu.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Titus Mdoe amesema Watanzania hawatakiwi kuwa na hofu ya utawala mpya ambayo ni mkali kwani lengo lake ni kurudisha nidhamu.
Akihubiri katika misa ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa Katoliki na Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam, Askofu Mdoe alisema Serikali ya sasa ni kali lakini hakuna haja ya kuwa na hofu kwa sababu watu watashindwa kufanya mambo kwa ufanisi wakitawaliwa na hofu.
“Utawala mpya ni mkali, je una hofu na kazi yako?” alihoji Askofu Mdoe.
Mjini Singida, waumini wa Kanisa la Pentekoste (FPCT) Tanzania la mjini kati Singida, wametumia maadhimisho ya Krismasi kumwombea Dk Magufuli mafanikio katika utendaji kazi, wakiomba Mungu aendelee kumpa afya, nguvu na ujasiri wa kutumbua majipu.
Kabla ya maombo hayo, Mchungaji Philipo Sospeter alisema: “Haya mafisadi ndiyo yaliyosababisha uhaba wa dawa katika vituo vya afya, barabara kujengwa chini ya kiwango na huduma mbovu katika Serikali yenyewe na taasisi zake.
Kwa kweli kila Mtanzania anapaswa kumwombea Rais Magufuli ili aendelee kuisafisha nchi na hatimaye, ipige hatua kubwa zaidi ya maendeleo ya kweli.” Aliwahimiza waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini, kutekeleza kwa vitendo falsafa ya Rais Magufuli ya Hapa Kazi Tu, ili kuipaisha Tanzania kimaendeleo.
Katika salamu zake kwenye ibada ya Krismasi mjini Dodoma, Askofu wa Kanda ya Kati wa Kanisa la PHAM, Julius Bundala alisema Tanzania ilishajaa rushwa na ufisadi hivyo maombi ya watumishi wa Mungu yanahitajika ili kuirudisha katika mstari mnyoofu.
Alisema nchi imejaa ulevi na vijana kujiingiza katika dawa za kulevya jambo ambalo linatakiwa kupigwa vita na wote bila ya kuwaonea huruma.
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk Dickson Chilongani alisema harakati, jitihada na nguvu ya mapambano dhidi ya ufisadi, ubadhirifu, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka zinazofanywa na Rais Magufuli hazitafanikiwa endapo atasimama peke yake.
Alisema kuwa upasuaji wa kile kinachoitwa majipu unaofanywa na Dk Magufuli ni harakati nzito na ngumu kufanikiwa endapo hazitaungwa mkono hasa kwa sala na maombi.
Dk Chilongani alisema hata utawala wa Rais Magufuli utafanikiwa endapo utamtegemea Mungu maana hata upasuaji wa majipu anaofanya si wote watakaofurahishwa nao na kwamba watakuwapo maadui kutaka kumkwamisha katika jitihada zake hizo za kuwatumikia wananchi.
Mjini Moshi, Mkuu Mteule wa KKKT, Dk Frederick Shoo amesema hakuna haja ya baadhi ya watu kuendelea kuwa na kinyongo baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu.
Katika uchaguzi huo, Dk Magufuli alishinda matokeo ambayo yalipingwa na aliyekuwa mgombea wa Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa.
Katika ibada ya Krismasi iliyofanyika katika kanisa kuu Usharika wa Moshi Mjini, Askofu Shoo alisema hakuna haja ya kuendelea kubaki na kinyongo.
“Krismasi ni wakati wa tangazo la Mungu la amani. Iko Mioyo iliyojaa hofu na chuki. Leo tunasikia juu ya mapigano juu ya utengano katika nyumba zetu, kati ya ndugu na ndugu. Ni wakati wa kutangaziana amani,” alisema.
Wahubiri amani
Mkoani Iringa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Tarrcisius Ngalalekumtwa amewataka waumini wa kanisa hilo na Watanzania kwa ujumla kulinda na kutunza amani iliyopo kwani bila ya kufanya hivyo Taifa haliwezi kuendelea.
Ngalekumtwa ambaye pia ni Askofu wa Jimbo la Iringa, alitoa kauli hiyo juzi katika kanisa la kiaskofu lilipo Kihesa mkoani hapa.
“Bila ya kulinda amani iliyopo hapa nchini na kuitunza Tunu hii ya Taifa, nchi haiwezi kusonga mbele ndiyo maana tunasema ulinzi wa amani ni jukumu la kila mtu,” alisema Ngalalekumtwa.
Katika ibada hiyo ya mkesha, askofu huyo aliwaasa waumini kutolipiza visasi kwa wengine, bali wadumishe upendo na mshikamano na kufanya toba ya kweli ili kuendana na mafundisho ya Biblia.
Akiongoza ibada ya mkesha kwa waumini wa makanisa ya KKKT, AICT na Roman Mjini Geita, iliyofanyika katika Katoliki Jimbo Kuu la Geita, Askofu, Anjelo Shikombe aliwataka wananchi kutunza amani ya nchi kwa kuimarisha upendo na uvumilivu katika familia zao.
Pia, aliwataka watumishi wa Serikali kutimiza wajibu wao na kuacha kujilimbikizia mali, kwani kwa kufanya hivyo ni kurudisha nyumba maendeleo ya Taifa.
Tofauti na miaka ya nyuma, polisi mkoani Geita, iliimarisha ulinzi katika makanisa mbalimbali wakati wa ibada ya Krismasi. Mwandishi wetu alitembelea makanisa mbalimbali na kushuhudia askari wenye silaha wakiimarisha ulinzi.
Mjini Mwanza, Katekista wa Kanisa Katoliki Mabatini, Elias Philipo alisema, Watanzania wanatakiwa kuienzi na kuidumisha amani iliyopo kwani siku ikiponyoka, watatumia muda mwingi kuirudisha.
Zanzibar
Kwa nyakati na mazingira tofauti mjini Zanzibar, maaskofu, Michael Hafidhi na Augustine Shao walisikika wakiwakumbusha waumini umuhimu wa kulinda amani katika jamii.
“Tunaishi katika zama ambazo amani imejaribiwa, ni wajibu wetu waumini kuilinda kwa kila hali ili dunia iendelee kubaki kuwa mahali bora pa kuishi,” alisema Askofu Shao.
Aliwakumbusha waumini kuishi kwa amani miongoni mwao na kujali misingi ya haki, uadilifu, utekelezaji wa ibada, umoja, upendo na kuyakimbia maasi yote.
Askofu Hafidhi aliwatahadharisha waumini juu ya kujiingiza katika mazingira ya upotevu wa amani akisema thamani ya jambo hilo ni kubwa kama zilivyo gharama zake.
“Ninawaasa na kila viashiria vya upotevu wa amani, tuishi kwa upendo tukijali maisha ya kila mmoja miongoni mwetu,” alisema.
Misa hiyo ya Krismasi iliyofanyika katika makanisa ya Tibirinzi, Makangale, Vitongoji na Kizimbani kisiwani Pemba.
Mgogoro wa Zanzibar
Akizungumza na mwandishi wetu baada ya misa ya mkesha wa Krisimasi iliyofanyika katika Kanisa la Azania Front, Dar es Salaam, Askofu Malasusa aliwataka viongozi wakuu wa nchi kukaa meza moja na kumaliza hali ya sintofahamu inayoendelea Zanzibar, baada ya kufutwa kwa uchaguzi.
Alisema Tanzania ni kisiwa cha amani na tayari wananchi wameonyesha ukomavu kwa kuwa watulivu baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu na kusisitiza kuwa ukomavu huo unapaswa kuendelezwa na viongozi wa Serikali kuhakikisha Zanzibar inakuwa shwari.
“Siku zote tatizo hutatuliwa kwa mazungumzo. Hatuhitaji namna yoyote ya kuweza kusukuma (suala la Zanzibar) lakini tunachosisitiza ni kuwapo kwa mazungumzo na wale wanaowajibika waweze kuiweka amani kwanza ili Taifa hili iendelee kuwepo,” alisema.
Kijamii
Mjini Mbeya, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya, Mhashamu Evarist Chengula alionekana kukerwa na tabia ya utoaji mimba, utumiaji wa dawa za kulevya unaofanywa na wananchi wakiwamo waumini wa Kikristo huku akivitupia lawama vyombo vya dola kwa kutotimiza wajibu wake ipasavyo.
Alisema hivi sasa barani Afrika, kuna kasumba ya kuacha utamaduni wa kuthamini uhai wa binadamu na badala yake watu kuwa vinara wa utoaji mimba na vijana wengi wakijihusisha na uvutaji wa dawa za kulevya kuharibikiwa maisha yao.
“Vitendo vya kutoa mimba, havikubaliki kamwe na ni dhambi kubwa kwa Mungu. Hata hapa Jijini (Mbeya) kuna zahanati zimewekwa maalumu kwa ajili ya kutoa mimba wanawake, hivi kweli tuseme hatuvijui?.... lakini tunakaa kimya wakati maovu yanazidi kutendeka. Vyombo vya usalama vipo wapi?” alisema Askofu Chengula.
Askofu KKKT, Dayosisi ya Mashariki Ziwa Victoria (DMZV), Andrew Gulle alisema jamii inaishi kwa kulipizana visasi maisha hivyo kuwataka Watanzania kutumia sikukuu hiyo ya Krismasi kufanya yanayompendeza Mungu na si kinyume chake.
Alisema migongano na chuki inayotokea kwenye jamii ndicho chanzo cha kuleta mifarakano na kusababisha vita vinavyotokea mataifa mbalimbali hiyo ni kwa sababu ya kutokuwa na hofu ya Mungu na kutokufuata mafundisho yake.”
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, Issac Amani aliwapa mamlaka mapadre wa kanisa hilo ya kuwaondolea dhambi wanawake waliotoa mimba kwa makusudi.
Lakini Askofu Amani alisema wataondolewa dhambi hiyo baada ya kuwapatia ushauri wa kina kuhusu ubaya wa tendo na umuhimu wa kufanya toba ya kweli inayompendeza Mwenyezi Mungu.
“Watambue na kukiri kuwa walifanya kosa kubwa sana la uonevu kwa hao vichanga waliopewa uhai na Mungu lakini wakawaangamiza kikatili wangali tumboni,” alisema Askofu Amani na kuongeza:
“Dhambi hiyo humtenga mtu na kanisa moja kwa moja mpaka iondolewe na askofu peke yake. Kwa tamko hili natangaza mapadre wanapewa mamlaka ya kuwaondolea dhambi hiyo wahusika.”
Askofu Amani alisema si ajabu baadhi ya wahusika waliendelea kukomunika kama vile wao siyo wauaji, akisisitiza kuwa kushiriki dhambi ni dhambi ikiwamo hiyo ya kushawishi na kusaidia kutoa mimba.MWANANCHI

0 comments:
Post a Comment