Kivuko cha mto Kilombero maarufu kama MV Kilombero ll juzi usiku kilishindwa kuhimili upepo mkali ulioambatana na mvua ya radi, na kufanya kigonge nguzo za pembeni ya mto na kukosa mwelekeo hivyo kupinduka ndani ya maji.
Kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba watu 100 kilipata dhoruba ya upepo mkali na kupinduka majira ya saa 1:30 usiku kikiwa na abiria kati ya 35 hadi 50 baada ya kupoteza mwelekeo kutokana na upepo na kusombwa umbali wa mita 40 kutoka eneo la njia ya kivuko hicho.
Pamoja na abiria waliokuwepo pia Kivuko hicjo kilikua na magari matatu na Bajaji mbili kikitokea upande wa wilaya ya Ulanga kwenda Wilya ya Kilombero.
Akizungumza na Mwananchi eneo la feli ya mto Kilombero katika mji mdogo wa Ifakara, mmoja wa waokoaji wa wahanga hao, Stanley
Mlongola (33) alieleza kuwa kazi ya kuokoa abiria ilikuwa ngumu kutokana na idadi kubwa ya abiria waliokua waking’ang’ania kupanda katika boti moja ya iliyokua ikitumika kwa uokoaji.
Mlongola ambaye anafanya kazi ya kuvusha abiria kutumia boti ndogo katika mto huo, alieleza kuwa baada ya kuona Kivuko cha MV11 Kilombero kikipoteza mwelekeo na kusukumwa na upepo mkali kisha kugonga nguzo za daraja la muda lililoko pembeni ya njia kuu ya kivuko hicho.
“Upepo ulikuwa mkali na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha ulichangiwa kusukuma Kivuko umbali wa mita 40 kisha kugonga nguzo za daraja la muda la wachina kisha kupinduka majini na watu kuanza kupiga kelele ya kuomba msaada wa kuokolewa.”alisema Mlongola.
Waziri wa ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa aliyefika eneo la tukio majiya mchana jana alisema kuwa serikali tayari imemlipa mkandarasi kiasi cha sh825 milioni za kuendelea na ujenzi wa daraja la kudumu ambalo litakuwa suluhisho la wakazi wa wilaya za Ulanga, Kilombero na Malinyi mkoani Morogoro ili kuepukana na ajali za vivuko hivyo katika mto Kilombero.
Mbarawa alisema kuwa Serikali imepokea kwa masikitiko taarifa za ajali hiyo na kuahidi kuwa baada ya kukamilika kwa daraja hilo litakuwa mkombozi kwa wakazi hao na watanzania kiujumla, kuangalia namna ya kurejesha mawasiliano kati ya Ulanga na Kilombero linapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Naye Meneja wa wakala wa ufundi na umeme (Temesa) Mhandisi Margreth Mapela alisema kuwa kivuko cha MV11 Kilombero kina uwezo wa kubeba tani 50 za mizigo yote huku kikiwa na uwezo wa kubeba idadi ya watu 100 hadi 150 kwa wakati mmoja.
"Tulipata taarifa kutoka kwa nahodha amenieleza kuwa watu waliopanda katika kivuko hicho ni kati ya 30 na 35 lakini mpaka sasa hivi bado hatujapata maafa."alisema Mapela
Mmoja wa wahanga hao, Habiba Ngakongwa alisema baada ya kupanda kivuko hicho na kuanza safari na wakati chombo kipo katikati ya mto huo ghafla kulitokea upepo mkali na mvua kubwa na kuanza kuyumba hali iliyowafanya abiria kukumbwa na taharuki.
Alisema baada ya upepo ule kuwa mkali, dereva wa kivuko hicho aliweza kupambana na hali ile kwa zaidi ya dakika 50 kabla ya kuzidiwa nguvu na kuvutwa na maji kabla ya kugonga nguzo za daraja la muda la wachina na kuanza kulala kwenye maji.alisema Habiba.
“Tulitangaziwa kivuko kupoteza mwelekeo na nahodha akatusihi tuvae maboya ya kujiokoa na asiwepo mtu wa kuruka kutoka ndani ya kivuko” alisema Habiba.
Tukio la kivuko hicho cha mto kilombero kushindwa kumudu upepo sio la mara ya kwanza kutokea katika eneo hilo la mpakani mwa wilaya za kilombero na ulanga,ambapo kila mwaka nyakati kama hizi kumekuwa na tatizo la kupoteza maisha kwa watumiaji wa kivuko hicho na mali nyingi kupotea.
Hali ya dhoruba na kuyumba kwa kivuko kikiwa katikati yam to huo kilianza tangu juzi na kushuhudiwa ambapo kivuko hicho kilishindwa kuhimili upepo kikiwa kati kati ya maji na kulazimika kurudi kilipotoka na saa chache baadaye kiliendelea na safari.
Magari yaliyozama baada ya kivuko hicho kuzama ni pamoja na Gari moja aina ya Fuso,Toyota land cruiser mbili ikiwemo mali ya banki ya CRDB tawi la Ifakara na nyingine mali ya kampuni ya Mitiki(KVTC).
Baadhi ya watumiaji wa kivuko hicho wakizungmza na gazeti hili,walilalamikia hitilafu za mara kwa mara za kivuko hicho, hivyo kuiomba serikali kuwaangalia kwa jicho la kipekee wananchi wa wilaya za Ulanga na Kilombero.
Richard Lucas alisema ni vyema serikali ikaharakisha ukamilishaji wa daraja linaloendelea kujengwa eneo hilo, ambalo kwa sasa ujenzi wake umesimama.
Alisema kumekuwa na daraja la muda linalotumiwa na wajenzi wa daraja hilo ambalo limeondolewa eneo hilo,kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha hivyo kuwafanya wananchi kushindwa hata kuvuka kwa njia ya miguu.
Hafidh Mohamed na Ally Mohamed wakazi wa Kilombero walisema kivuko hicho ndio tegemeo la la wakazi wa pande mbili ambao wengine wamekuwa wakifanya shughuli za kibiashara hivyo kuwalazimu kuvuka mara mbili ama tatu kwa siku.

0 comments:
Post a Comment