BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MBUNGE WA CHADEMA AONDOLEWA KWA NGUVU KATIKA KIKAO CHA BARAZA LA MADIWANI NA ASKARI POLISI KILOMBERO.

Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali akitolewa kwa nguvu katika ukumbi wa mikutano na Polisi kwa amri ya Mwenyekiti wa kikao cha Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Morogoro jana kwa kile kinachodaiwa kutokuwa mjumbe halali wa kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo. Picha na Juma Mtanda.

By Juma Mtanda, Mwananchi
Kilombero.
Mpambano wa madaraka kati ya Ukawa na CCM, umehamia katika halmashauri ya wilaya ya Kilombero na kusababisha mbunge wa Jimbo hilo, Peter Lijualikali (Chadema) kuondolewa na polisi katika kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani kwa madai kuwa si mjumbe halali.

Pamoja na kuondolewa kwa mbunge huyo, Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni ofisa tawala wa wilaya, Yahya Nania alilazimika kuahirisha kikao kwa muda usiojulikana baada ya kushindwa kuwaapisha madiwani kwa sababu ya vurugu.

Pia, Ukawa walikuwa wanapinga walichoita njama za chama tawala kuongeza wabunge wa viti maalumu kutoka nje ya halmashauri ya wilaya ya Kilombero, ili kushinda uenyekiti wa halmashauri kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa meya wa Ilala na Kinondoni, Dar es Salaam.

Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa kikao hicho kuahirishwa baada ya kile cha Desemba 15, mwaka jana kilichoahirishwa kutokana na akidi kutotimia.

Katika halmashauri hiyo kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015, Chadema ilipata wabunge wawili katika majimbo ya Kilombero na Mlimba na madiwani 22 dhidi ya CCM iliyopata madiwani 20.

Songombingo hilo lilianza saa 3.28 asubuhi, baada ya wajumbe wote kukamilisha taratibu za kujisajili na Nania kutoa mwongozo akiwataka wajumbe wakati wa kumchagua mwenyekiti na makamu wake kutumia kalamu zilizoandaliwa na halmashauri, la sivyo kura zao hazitahesabiwa.

Nania alisoma barua ya Tamisemi iliyotoa ufafanuzi wa kisheria juu ya Lijualikali kutokuwa mjumbe halali katika kikao hicho, jambo lililowafanya wajumbe wa Ukawa kupinga.

Akifafanua juu ya mbunge huyo, Nania alisema kutokana na mwongozo wa kisheria, anawajibika katika Baraza la Madiwani la Mji Mdogo wa Ifakara, ambalo kwa sasa halijaundwa.

Baada ya kauli hiyo ndipo kulitokea vurugu iliyosababisha meza na viti kudondoshwa chini na kuharibika, kabla ya kurejea hali ya utulivu iliyodumu kwa dakika nane na kuibuka upya.

Akizungumzia suala hilo alisema: “Nimechaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Kilombero na napaswa kuhudhuria vikao vya baraza la madiwani la halmashauri hiyo ya wilaya na siyo kuingia Baraza la Madiwani la mji mdogo Ifakara.”

Lijualikali alisema kuwa atapambana hadi haki yake ipatikane.

Mwanasheria wa halmashauri ya Kilombero, Faraja Nakuwa alitoa ufafanuzi wa kisheria juu ya kutolewa kwa mbunge huyo na utumiaji wa kalamu zilizoandaliwa na kikao hicho.

Nakuwa alisema mwenyekiti wa kikao anayo haki ya kisheria ya kufanya jambo kuimarisha hali ya amani, ikiwamo kuweka utaratibu wa kutumia kalamu maalumu wakati wa upigaji kura.

Alisema kutokana na sheria zilizopo, mbunge wa viti maalumu ama wa kuteuliwa na rais wanapata maelekezo kutoka kwa viongozi wao wa vyama wapi watapelekwa ili kuapa. Lijualikali alisema yeye ni mbunge halali wa jimbo la Kilombero, na kisheria anapaswa kuhudhuria vikao vya halmashauri ya wilaya ya Kilombero.

Alisema haina mantiki kwa Tamisemi kutoa mwongozo wa kumuondoa asihudhurie vikao vya halmashauri ya wilaya na kumlazimisha kushiriki vikao vya Mji Mdogo wa Ifakara, jambo ambalo alisema linapindisha sheria.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: