BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

JESHI LA POLISI LAWASHIKILIA WATU 21 KWA TUHUMA ZA KUHUSIKA MAUAJI YA MBUZI NA KONDOO MVOMERO

1AA 
Mbuzi na Kondoo wakiwa wamekufa baada ya kukatwakatwa na vitu vyenye ncha kali wilayani Mvomero.

By Lilian Lucas na Hamida Shariff, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz
Morogoro.
Polisi Mkoa wa Morogoro wanawashikilia watu 21 akiwamo mtendaji mmoja wa Kijiji cha Mkindo na mwenzake wa Dihombo kwa tuhuma za kuua, kujeruhi wanyama na kulisha mifugo mpunga kwenye shamba za la ekari moja wilayani Mvomero.

Wakati watuhumiwa hao wakishikiliwa, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Betty Mkwasa kuhakikisha mmiliki wa mifugo iliyouawa na kujeruhiwa, Ketepoi Nuru anaingizwa katika mfuko wa maafa ili asaidiwe na kupatiwa ulinzi.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Leonard Paulo amesema leo kuwa mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Mkindo ulianza Februari 7, lakini walifanikiwa kuutatua.

Amesema kundi la ng’ombe zaidi ya 50 liliingizwa na wachungaji zaidi ya watatu wa jamii ya kimasai katika shamba hilo la Rajabu Issa (31) na kula mpunga.

Paulo amesema Issa, mkazi wa Dihombo aliwazuia ng’ombe hao kula mpunga bila mafanikio.

Amesema wakati mkulima huyo akijaribu kuwaswaga ng’ombe hao, walijitokeza vijana wanaosadikiwa kuwa ni morani wa Kimasai na kuondoa mifugo hiyo ikiwa imefanya uharibifu wa zao hilo.

Paulo amesema mkulima huyo alitoa taarifa kituo cha polisi cha Mvomero kuhusu uhalifu huo.

Amesema Jumatatu wiki hii wakati polisi wakishughulikia suala hilo, kikundi cha ulinzi wa jadi wa wakulima ‘Mwano’ kilivamia nyumbani kwa Nuru Kipande (79) na kumkuta mwanaye (Ketepoi Nuru) na kumnyang’anya simu ili asiwasiliane na mtu yoyote kuomba msaada. 


Amesema kundi hilo liliingia zizini na kuswaga mifugo iliyokuwamo na kuipeleka porini kisha kuikatakata kwa vitu vyenye ncha kali.

Paulo amesema katika tukio hilo mbuzi 50 walijeruhiwa, kati yao 28 walikufa. Amesema vilevile kondoo 27 walijeruhiwa na nane kufa.

Amesema ndama wawili walikufa na mmoja kujeruhiwa katika tukio hilo.“Kutokana na tukio hilo, mifugo 38 imekufa huku mifugo 42 ikiwa imejeruhiwa,” amesema Paulo. 


Paulo amesema watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa huku wengine wakitafutwa kuhusiana na matukio hayo.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: