BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MRADI WA MABASI YAENDAYO KASI YAMPONZA KIGOGO NA WENZAKE, WAKUMBANA NA MKONO WA SHERIA DAR ES SALAAM.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi (Dart), Asteria Mlambo, akiingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana, akikabiliwa na mashitaka matatu.

 
Vigogo watatu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), akiwamo Ofisa Mtendaji Mkuu, Asteria Mlambo, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Mbali na Mlambo, vigogo wengine ni Mkurugenzi wa Fedha, Evodius Katale na Mwanasheria Mwandamizi, Francis Kugesha. Wote hao wanakabiliwa na mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya Sh. milioni 83.5 na kuwasilisha nyaraka za kughushi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mbali na Mlambo, wengine ni, Mkurugenzi wa Fedha, Evodius Katale na Mwanasheria Mwandamizi Francis Kugesha wote wa Dart na Yuda Mwakatobe.

Washtakiwa hao, pamoja na Yuda Mwakatobe, ambaye si mwajiriwa wa Dart, walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Respicius Mwijage.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali, Jacqueline Nyantori na Asteria Wilson wakisaidiana na Waendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Vena Ndeoya na Stella Mafuru.

Nyantori alidai kuwa kati ya Septemba Mosi na Oktoba, 2013, mshtakiwa wa kwanza hadi wa tatu, wakiwa watumishi wa Dart, walishindwa kutimiza majukumu yao kwa weledi na kuisababishia serikali hasara ya Sh. 83,564,367.

Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Juni 26, 2004 katika ofisi za TRA, zilizoko Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, mshtakiwa wa nne aliwasilisha nyaraka za kughushi za taarifa ya hesabu za Kampuni ya Yukan Business Co. Ltd.

Ilidaiwa kuwa nyaraka hizo aliwasilisha kwa maofisa wa mamlaka hiyo na kumsababishia kupunguziwa kiwango cha kulipa kodi.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa Machi 26, 2005 katika ofisi ya TRA zilizoko Ilala, jijini Dar es Salaam, Mwakatobe aliwasilisha nyaraka za kughushi za taarifa ya hesabu ya kampuni hiyo kwa maofisa wa TRA na kumsababishia kupunguziwa kiwango cha kulipa kodi.

Nyantori alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi la dhamana.

Wakili wa utetezi, Yuda Thadei, kwa upande wake, aliomba mahakama kutoa masharti nafuu ya dhamana kwa kuwa washtakiwa wamepandishwa kizimbani baada ya kuitwa kutoka ofisini kwao.

Hakimu Mwijage alisema mshtakiwa wa kwanza hadi wa tatu, watajidhamini kwa hati za mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh. milioni 14 kila mmoja.

Pia alisema kila mshtakiwa atadhaminiwa na mshtakiwa mmoja atakayetia saini hati ya dhamana yenye thamani ya Sh. Milioni 15 pamoja na barua kutoka serikalini au taasisi inayotambulika.

Kwa upande wa mshtakiwa wa nne, hakimu alisema anatakiwa kuwa na mdhamini mmoja anayetoka kwenye taasisi inayotambulika au mtumishi wa serikali, atakayetia saini hati ya dhamana ya Sh. milioni tano.

Hadi Nipashe inaondoka katika viunga vya mahakama hiyo, mshtakiwa wa kwanza hadi wa tatu walitimiza masharti hayo na wako nje hadi Machi 9, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa.CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: