NDANI YA SIKU 105 SERIKALI YA AWAMU YA TANO YAGUDNUA UFISADI WA Sh245 BILIONI
Dar es Salaam. Hakuna shaka kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kutimiza ahadi ya kutumbua majipu aliyotoa Rais John Magufuli katika hotuba yake ya kwanza bungeni, baada ya kuanika ufisadi wa jumla ya Sh245 bilioni katika matumizi yasiyo ya lazima, ukwepaji wa kodi na wizi.
Upotevu wa fedha hizo umefichuliwa katika siku 105 tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani Novemba 5 na kujikita kwanza kwenye kubaini mianya ya wizi wa fedha, ukwepaji kodi, ukiukwaji sheria ya manunuzi, ukwepaji ushuru na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma.
Kiwango hicho cha fedha hakijumuishi ufisadi mwingine uliobainika kwenye sekta kama ya mafuta, ambako imebainika kuwa mita ya kupimia mafuta ilizimwa kwa takribani miaka mitano na hivyo sehemu kubwa ya mafuta kutolipiwa kodi, huku sehemu nyingine ikinyonywa na wajanja kabla ya kufika kituo cha kampuni ya Tipper.
Wakati takribani wizara zote zilikuwa hazipewi fedha zote za matumizi zinazoidhinishwa na Bunge, kama fedha hizo zingedhibitiwa, zingeweza kukidhi bajeti za wizara tatu kama Viwanda na Biashara iliyopangiwa Sh116.5 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2015/16. Wizara hiyo ni moja ya sekta zinazotegemewa kuchochea maendeleo na kuchukua sehemu ya kundi la vijana wasio na ajira.
Pia, fedha zilizosalia zingeweza kukidhi mahitaji ya bajeti ya Wizara ya Ardhi, iliyopangiwa Sh83 bilioni, na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto (Sh31.4 bilioni).
Kama Sh245 bilioni zikigawanywa katika maeneo matano tofauti zinaweza kujenga kilomita 50 za barabara ya lami, kununua magari ya wagonjwa 167, kujenga zahanati 83, vyumba vya madarasa 6,000 na kutengeneza madawati 714,286, au kununua ndege mbili aina ya airbus kwa bei ya Sh120 bilioni kuliwezesha Shirika la Ndege (ATCL) kuzinduka.
Kutokana na kubainika kwa ufisadi huo, wapo watumishi waliosimamishwa au kufukuzwa kazi na wengine kufikishwa mahakamani.
Kufichuliwa kwa ubadhilifu huo kwa mtindo wa kutumbua majipu ni utekelezaji wa ahadi ambazo Rais Magufuli alitoa kwenye hotuba yake ya kwanza bungeni Novemba 2, 2015 mjini Dodoma, alipoahidi kupambana na rushwa bila kigugumizi wala haya. Kasi hiyo imekuwa ikikolezwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambaye amefichua uovu mkubwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam, na mawaziri wake.
“Dawa ya jipu ni kulitumbua na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu lakini bahati mbaya halina dawa nyingine,” alisema Rais Magufuli kwenye hotuba hiyo bungeni.
Hadi sasa, taasisi zilizopewa jukumu la kuwachunguza na kuwafikisha mahakamani watumishi walioonekana na matatizo, bado zinaendelea na shughuli hiyo, huku maofisa waandamizi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) wakifikishwa mahakamani.
Ubadhirifu
Miongoni mwa kashfa zilizoibuliwa ni ile ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ambako Januari 25, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa mkurugenzi wake mkuu, Dickson Maimu na watendaji wengine wa taasisi hiyo na kuagiza vyombo mbalimbali kufanya uchunguzi wa matumizi ya fedha katika mamlaka hiyo.
Katibu Mkuu kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema Nida imetumia Sh179.6 bilioni, lakini bado watu wengi hawajapata vitambulisho, huku Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga akieleza kuwa baadhi ya waliotumbuliwa walikutwa na mali nyingi “kupita maelezo”.
Pia Februari 10, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alimsimamisha kazi meneja wa fedha wa ATCL, Steven Kasubi baada ya upotevu wa Sh715.8 milioni.
Mbarawa alisema meneja huyo amesimamishwa kazi kutokana na kukiukwa kwa taratibu za uuzaji tiketi kwa kuongeza uwezo wa mawakala kuuza tiketi kupitia kiwango walicholipia.
Waziri huyo wa Ujenzi pia aliwasimamisha kazi wafanyakazi 15 wa TPA kwa tuhuma za upotevu wa Sh48 bilioni kutokana na ukwepaji wa kodi na tozo mbalimbali, na pia wakuu wanne wa idara wa kampuni ya huduma za meli (Marine) kwa tuhuma ya ubadhirifu wa zaidi ya Sh600 milioni.
Kashfa nyingine ni ile iliyoibuliwa Februari 15 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliyewasimamisha kazi wakurugenzi wanne wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwa tuhuma za ubadhirifu wa Sh1.5 bilioni.
Wakurugenzi hao wanadaiwa kukiuka taratibu za manunuzi na za utumishi wa umma.
Katika sakata la Februari 17, Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako alisitisha mkataba wa mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi (HELSB), George Nyatega kwa tuhuma za ukiukwaji wa kanuni za utoaji mikopo, kutosimamia vizuri fedha, uzembe na ubadhirifu wa Sh3.1 bilioni.
‘Mtumbua majipu’ alitekeleza kazi hiyo Januari 29, alipomfukuza kazi mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Erica Mussika kwa kushindwa kusimamia mradi mkubwa wa barabara wa Sh9.192 bilioni, uliofanikishwa kwa mkopo wa Benki ya Dunia na amemfukuza kazi mhandisi wa ujenzi, Ruben Muyungi.
Jipu jingine liliibuliwa Januari 17, mwaka huu wakati ufisadi uliomuhusisha Miss Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare uliisababishia Benki Kuu (BoT) kuitoza faini ya Sh3 bilioni Benki ya Stanbic baada ya kuhusishwa katika miamala iyoisababishia Serikali hasara ya Sh1.3 trilioni kati ya mwaka 2012 na 2013.
Sinare, ambaye alikuwa ofisa mwandamizi wa Stanbic, kwa kushirikiana na aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Bashir Awale walitajwa kuhusishwa na mpango huo wa ufisadi uliotokana na Serikali kuhitaji mkopo wa dola 600 milioni za Marekani.
Matumizi ya Sh245 bilioni
Ufisadi huo wa fedha za walipa kodi uliifanya Serikali ishindwe kutekeleza wajibu wake wa kutoa huduma kwa wananchi kama ujenzi wa miundombinu ya usafiri, hospitali, ununuzi wa dawa, utoaji wa elimu bura na uwezeshaji wa kilimo cha kisasa ambacho kinaajiri kundi kubwa la vijana.
Kama Sh50 bilioni zingeelekezwa katika kutekeleza ilani ya CCM ya kugeuza jembe la mkono kuwa zana ya kuwekwa Makumbusho ya Taifa, fedha hizo zingeweza kununua matrekta 3,125 ya kuanzia aina ya Massey Fergusson kwa bei ya juu ya Sh16 milioni, kwa mujibu wa mtandao wa mauzo wa alibaba.com.
Aidha, Sh50 bilioni nyingine zingeweza kununua magari 167 ya kubebea wagonjwa kwa gharama ya Sh300 milioni kwa kila moja na kuwezesha kila mkoa kupata magari sita.
Pia, zahanati moja yenye vifaa vyote muhimu ujenzi wake unagharimu kati ya Sh600 milioni na Sh700 milioni. Hivyo, fedha Sh 50 bilioni zingeweza kujenga zahanati 83 yaani kila mkoa ungepata zahanati tatu.
Vilevile, wakati maelfu ya wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari wanasoma kwa kukaa chini kutokana na kukosa madawati, Sh 50 bilioni zinaweza kutengeneza madawati 714, 286 ya miguu ya chuma kwa gharama ya Sh70,000 kwa kila moja na kuwezesha kila mkoa kupata madawati 28,571.
Kiasi cha Sh45 bilioni kinaweza kutumika kujenga vyumba 6,000 vya madarasa kwa bei ya Sh7.5 milioni, hatua ambayo ingewezesha kujengwa kwa vyumba vya madarasa 240 kila mkoa nchini.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment